Open main menu

Mtaguso Mkuu

(Elekezwa kutoka Mtaguso mkuu)

Mitaguso saba na umuhimu wakeEdit

Mitaguso ya kiekumene (kutoka Kigiriki oικουμένη oikumene yaani dunia inayokaliwa na watu) ni jina linalotumika hasa kwa mikutano saba ya namna hiyo iliyofanyika kati ya mwaka 325 hadi 787 upande wa mashariki wa Dola la Roma (ulioendelea baadaye kama Milki ya Bizanti).

Orodha yake ni kama ifuatavyo:

1. Mtaguso wa kwanza wa Nisea (mwaka 325)

2. Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381)

3. Mtaguso wa Efeso (431)

4. Mtaguso wa Kalsedonia (451)

5. Mtaguso wa pili wa Konstantinopoli (553)

6. Mtaguso wa tatu wa Konstantinopoli (680-681)

7. Mtaguso wa pili wa Nisea (787)

Mitaguso hiyo, iliyofanyika wakati wa Mababu wa Kanisa, ilitoa maamuzi ya msingi juu ya mafundisho ya imani na sheria za Kanisa yaliyokuwa muhimu kwa maendeleo ya Ukristo ya baadaye.

Mapokezi ya mitaguso sabaEdit

Mitaguso hiyo saba inakubaliwa hasa na Kanisa Katoliki na Waorthodoksi, kutokana na msisitizo wao wa mapokeo na wa mamlaka ya kufundisha ya waandamizi wa Mitume.

Makanisa ya kale ya mashariki hukubali mitaguso mitatu ya kwanza tu, na Kanisa la Asiria ile miwili ya kwanza. Kukataa maamuzi ya mitaguso iliyofuata ndiyo sababu ya mafarakano yao.

Madhehebu kadhaa ya Kiprotestanti (hasa Walutheri, Waanglikana, Wamethodisti, Wamoraviani) yanakubali mitaguso hiyo kadiri inavyolingana na uelewa wao wa Biblia.

Hivyo Waprotestanti wengi wanashikilia imani juu ya Yesu Kristo, juu ya Roho Mtakatifu na juu ya Utatu mtakatifu kama ilivyofundishwa rasmi katika mitaguso ya kwanza.

Mitaguso ya baadayeEdit

Kutokana na umuhimu wa mitaguso mikuu kwa Kanisa Katoliki na kwa Waorthodoksi, mikutano mikuu ya maaskofu iliendelea kufanyika ikatazamwa pengine kama mitaguso ya kiekumene.

Yafuatayo ni mitaguso mikuu inayohesabiwa katika kanisa katoliki. Karibu yote ilifanyika katika milenia ya pili magharibi (Italia, Ufaransa na Ujerumani wa leo):

8. Mtaguso wa nne wa Konstantinopoli (869-870)

9. Mtaguso wa kwanza wa Laterano (1123)

10. Mtaguso wa pili wa Laterano (1139)

11. Mtaguso wa tatu wa Laterano (1179)

12. Mtaguso wa nne wa Laterano (1215)

13. Mtaguso wa kwanza wa Lyon (1245)

14. Mtaguso wa pili wa Lyon (1274)

15. Mtaguso wa Vienne (1311-1312)

16. Mtaguso wa Kostansa (1414-1418)

17. Mtaguso wa Firenze (1439-1445)

18. Mtaguso wa tano wa Laterano (1512-1517)

19. Mtaguso wa Trento (1545-1563)

20. Mtaguso wa kwanza wa Vatikano (1869-1870)

21. Mtaguso wa pili wa Vatikano (1962-1965)

Lengo la mitagusoEdit

Mitaguso mikuu ya kwanza ilifanyika hasa ili kubainisha katika mafundisho yaliyogongana yapi yanalingana na imani sahihi. Mwisho wake ulikuwa kutangaza dogma fulani na kutenga na Kanisa watakaokataa kuiamini na watakaofundisha tofauti.

Kumbe mitaguso iliyofanyika baada ya farakano la mwaka 1054 kati ya Kanisa la Mashariki na Kanisa la Magharibi, pamoja na kulenga umoja uliovunjika na kufundisha dogma mpya, ilishughulikia zaidi urekebisho wa Kanisa katika ngazi na nyanja zote.

Kwa namna ya pekee mtaguso wa pili wa Vatikano tangu uitishwe ulijulikana kuwa wa kichungaji, yaani usio na lengo la kufundisha dogma mpya wala kulaani mafundisho mengine.

Msingi wa imani kuhusu mtaguso mkuuEdit

Kadiri ya imani ya Kanisa Katoliki, Yesu aliwakabidhi Mitume kumi na wawili uongozi wa Kanisa wakiwa kundi moja lenye mkuu wake, yaani Mtume Petro.

Vilevile waandamizi wao, yaani maaskofu wote, ni kundi moja na Papa wa Roma ndiye mkuu wao. Huyo peke yake, na kundi la maaskofu likiwa pamoja naye na chini yake, ndio wenye mamlaka ya juu katika Kanisa lote.

Mamlaka hiyo inatumika kwa namna ya pekee unapofanyika mtaguso mkuu, yaani mkutano maalumu wa maaskofu uliokubaliwa na Papa kuwa unawakilisha kundi hilo lote.

Kwa kiasi fulani ndiyo imani ya Waorthodoksi pia, ingawa hao wanapunguza umuhimu wa mchango wa mamlaka ya Papa.

Viungo vya njeEdit