Mtumiaji:Kipala/Mateso ya Wakristo
Mateso ya Wakristo ni ukandamizaji wa kiserikali au wa kijamii kwa Wakristo kwa sababu ya dini yao. Kuna mifano mingi ya kihistoria na ya kisasa ya madhulumu inayoathiri jumuiya hiyo, pamoja na mateso dhidi ya dini nyingine.
Jina
haririKatika historia ya Kanisa, mateso ya kidini katika Dola la Roma hadi Hati ya Milano ya mwaka 313 yanajulikana kama mateso ya Wakristo.
Historia ya Kale
haririDola la Roma
haririTaarifa kuhusu mateso ya Wakristo zilipatikana tangu karne ya 1. Pale mwanzoni Ukristo ulionekana kama kundi katika Uyahudi lenye mafundisho yasiyokubalika. Hivyo Wakristo wa kwanza walitazamwa kama wakosaji Wayahudi waliovumiliwa mara nyingi (linganisha Mdo 5:34 n.k.) au kuadhibiwa (linganisha Mdo 7, hukumu ya Stefano) kulingana na utaratibu wa jumuiya hiyo. Ndani ya jumuiya za Kiyahudi walitengwa katika miji kadhaa na kuadhibiwa, ingawa kwa jumla walivumiliwa.
Mateso ya Wakristo mikononi mwa vyombo vya Dola la Roma yalianza pia katika karne ya 1 yakaendelea hadi mwanzo wa karne ya 4, wakati Kaizari Konstantino alikubali Ukristo kuwa dini halali.
Wakristo walionekana si watu wa kawaida kwa sababu walikaa mbali na sadaka na ibada za miungu mahekaluni. Katika miaka ya kwanza walivumiliwa kiasi kwa sababu walitazamiwa kama kundi la Kiyahudi na Wayahudi walitambuliwa na serikali kuu kama dini halali na kuruhusiwa kutoshiriki katika ibada za miungu. Hata hivyo walitazamiwa na wengine kwa mashaka na chuki, sawa na Wayahudi. Mashambulio yaliweza kutokea kutokana na chuki hiyo. Mateso ya aina hii yanatajwa katika Waraka wa Kwanza wa Petro[1].
Mateso chini ya Nero na Domitiano
haririMateso ya kwanza mkononi mwa serikali yalitokea mjini Roma chini ya Kaizari Nero (54–68). Nero aliogopa hasira ya watu wa Roma kwa sababu ya moto ulioteketeza sehemu kubwa ya mji ambayo wengi waliona aliwahi kuusababisha. Hapo alishtaki Wakristo kuwa waanzilishi wa moto huu. Mwanahistoria Mroma Tacitus aliandika:
- Kwa hiyo, ili kuondoa uvumi (kuwa yeye mwenyewe alisababisha moto ule) Nero alistaki kundi liliochukiwa kwa sababu ya machukizo yao, lililoitwa „Wakresto“ na watu, na kuwatesa sana. Kristo, ambaye jina hilo lilitokana naye, alipatwa na adhabu kuu wakati wa utawala wa Tiberio mikononi mwa mmoja wa magavana wetu, Pontio Pilato. Imani potovu kabisa iliyodhibitiwa kwa muda huo, ilizuka tena si katika Yudea pekee, penye chanzo cha kwanza cha uovu huo, lakini hata huko Roma, ambapo mambo yote ya kuchukiza na ya aibu kutoka kila sehemu ya dunia hupata kituo yao na kuwa maarufu.
- Kwa hiyo, kwanza walikamatwa wote waliokiri hatia; basi, kwa habari yao, umati mkubwa sana ulitiwa hatiani. Walishtakiwa si kwa sababu ya jinai ya uchomaji tu bali chuki dhidi ya ubinadamu. Kejeli za kila namna ziliongezwa kwenye vifo vyao.
- Walifunikwa kwa ngozi za wanyama, wakararuliwa na mbwa hadi kufa, au walipigiliwa misumari kwenye misalaba, au walitupwa motoni na kuchomwa, ili kutumika kama nuru ya usiku, wakati mwanga wa mchana ulikwisha.[2].
Hakuna dalili kwamba mateso hayo yalienea nje ya mji wa Roma. Katika mapokeo ya Wakristo wa kale inafuata taarifa kuhusu wimbi la madhulumu chini ya Kaizari Domitiano (81-96) linaloakisiwa katika Waraka wa Kwanza wa Petro[3]. Katika madhulumu hayo Wakristo hawakutafutwa lakini ilitosha kushtakiwa kama Mkristo. Kutoka nyaraka za Plinio Kijana (61 - 113) inaonekana kwamba walihukumiwa wakisisitiza kuwa Wakristo hata kama hakuna kosa lingine; walipewa nafasi ya kukana imani hiyo na kutoa sadaka mbele ya miungu halafu walisamehewa. Kaizari alithibitisha alifanya vizuri, kama Mkristo akionekana hadharani mbele ya hakimu anapaswa kufa, menginevyo wapewe nafasi ya kutubu na wasitafutwe. [4]
Mateso ya aina hii yaliendelea chini ya makaizari waliofuata, yakitegemea uhusiano baina ya Wakristo na wananchi katika mazingira yao na pia msimamo wa mahakimu na magavana wa Kiroma katika maeneo mbalimbali. Kwenye maeneo kadhaa Wakristo waliishi bila matatizo, katika maeneo mengine waliona matatizo na madhulumu.
Kwa jumla, kadri idadi ya Wakristo ilivyoongezeka, chuki kati ya wananchi dhidi yao ilikua katika maeneo mengi. Wakristo walitazamiwa kama wakanamungu, kama watu wanaojitenga na jamii na kawaida zote, wenye desturi mbaya na hatari kwa jamii na dola. Uvumi mbalimbali zilisambaa, eti Wakristo wana mikutano ya siri ambako wanalevya, kushiriki katika ngono kati ya wote hata wanachinja watu na kula nyama yao. Makaizari wa kipindi kile walisisitiza mara kadhaa si halali kama Wakristo wanapigwa na kuuawa na umati wa watu bali baada ya kuendesha kesi kwa utaratibu pekee. [5]
Mnamo mwaka 200 gavana wa Afrika Kaskazini alihukumu Wakristo wafe katika uwanja wa michezo waliporaruliwa na wanyama wa pori mbele ya watazamaji maelfu. Mwandishi Mkristo Tertuliani aliandika kuhusu hasira dhidi ya Wakristo katika mji wake Karthago: “Kama mto Tiber unafurika mji, kama Mto Nile haifuniki mashamba kama kawaida, mvua isiponyesha au tetemeko ikitikisika, kama kuna njaa au majanga, mara moja tunasikia kilio: Wakristo mbele ya simba!“[6]
Mateso chini ya Decius na Valerian
haririMnamo mwaka 249 Decius alifaulu katika uasi dhidi ya kaizari aliyekuwepo. Mwaka 250 , akilenga kuimarisha utawala wake, aliagiza raia wote washiriki katika ibada za kuombea dola na utawala wake. Kushiriki kulithibitishwa kwa hati. Wakristo waliokataa walikamatwa na kufungwa gerezani, wakisisitiza wakapokea hukumu ya mauti. Maaskofu wa Yerusalemu, Antiokia na Roma walikufa gerezani. Wengi walitoa sadaka hizo baada ya kutishwa, wengine walikimbia, walijificha au kuhonga maafisa ili wapate hati ya uthibitisho bila kushiriki hali halisi. Amri ya Decius haikulenga Wakristo[7] lakini ilikuwa pigo kubwa kwao. Idadi ya wahanga haikuwa kubwa sana kwa sababu Decius alikufa mapema vitani.[8]
Valerian aliyemfuata alitazamiwa mwanzoni kirafiki na Wakristo lakini aliendelea kuanzisha mateso upya[9] akilenga kanisa moja kwa moja. Maaskofu na mapadre walitafutwa, majengo ya makanisa na makaburi ya Wakristo kukamatwa. Katika awamu la kwanza adhabu ya maaskofu na makasisi waliokataa sadaka ilikuwa uhamisho kwa gereza ya mbali na kwa njia hiyo kaizari alilenga kutenganisha sharika na viongozi wao. Baada ya mwaka mmoja amri mpya iliagiza adhabu ya mauti kwa hao waliokataa sadaka[10].
Pia hapa ilikuwa kifo cha mapema ya kaizari kwenye mwaka 260 wakati wa vita dhidi ya Uajemi iliyomaliza mateso na mwana wake alibatilisha amri zake.
Mawimbi hayo mawili yalisababisha mafarakano ndani ya sharika za Wakristo; wale waliokataa sadaka lakini hawakuawa bado walitoka gerezani baada ya mateso na kudai kipaumbele juu ya hao waliowahi kujificha, kuhonga maafisa au kutoa sadaka. Kwa jumla maaskofu walisisitiza hao wote wasamehewe wakitubu lakini hata hivyo makundi kadhaa walijitenga na umoja wa Wakristo, maarufu kati yao alikuwa Novatiano wa Roma.
Milki ya Uajemi
haririKatika Milki ya Wasasani, Ukristo ulienea kwa nguvu katika Mesopotamia lakini pia kwenye nyanda za juu za Iran. Katika milki hiyo, dini rasmi ilikuwa Uzoroasta. Uajemi ilikuwa na mashindano na mara kwa mara uhusiano wa kiadui na Dola la Roma. Tangu utawala wa Kaizari Konstantino Ukristo ulianza kuwa muhimu zaidi upande wa Roma na hii ilisababisha hofu upande wa watawala wa Uajemi kuhusu ushirikiano wa raia zao wa Kikristo na adui aliye Mkristo. Kutokana na hofu hiyo mfalme Shapur II alianza kudhulumu Wakristo katika mji mkuu wake. [11]
Tanbihi
hariri- ↑ J. N. D. Kelly (1969), A Commentary on the Epistles of Peter and of Jude, London, A. & C. Black 1969, ISBN 0-7136-1285-1, uk. 10, online hapa
- ↑ Tacitus, Annales
- ↑ Die Lage der Christen im römischen Reich nach dem 1. Petrusbrief: Zum Problem einer Domitianischen Verfolgung Author(s): Joachim Molthagen, Source: Historia: Zeitschrift für Alte Geschichte, Bd. 44, H. 4 (4th Qtr., 1995), pp. 422-458, Stable URL: http://www.jstor.org/stable/4436394
- ↑ https://faculty.georgetown.edu/jod/texts/pliny.html Pliny, Letters 10.96-97, tovuti ya Chuo Kikuu cha Georgetown, iliangaliwa Oktoba 2022
- ↑ Origins to Constantine, ed. by Frances M. Young, Margaret M. Mitchell ; assistant editor K. Scott Bowie. (The Cambridge history of Christianity; v. 1) ISBN 0 521-81239-9, uk 508 ff
- ↑ Origins to Constantine, uk 511
- ↑ Kinyume aliona Eusebi wa Kaisarea kwamba sababu ya amri ya Decius ilikuwa chuki yake dhidi ya mtangulizi wake Kaizari Filipo, lakini wataalamu hawakubali. Ona Eusebius Caesariensis – Historia ecclesiastica - The Church History Of Eusebius, online http://www.ccel.org/ccel/schaff/npnf201.html , ukurasa 590 Mhariri Schaff anaeleza kwamba sababu inayotajwa hapa na Eusebio si sahihi.
- ↑ Origins to Constantine, uk 513 f.
- ↑ Eusebio uk. 632 anaeleza badiliko la msimamo wa kaizari ulisababishwa na ushawishi wa "wamagi" wa Misri.
- ↑ Origins to Constantine, uk. 515
- ↑ Ona Persian Martyrs katika Encyclopedia Iranica.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mtumiaji:Kipala/Mateso ya Wakristo kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |