Nyota nova
Nyota nova (lat. stella nova kwa maana ya "nyota mpya", ing. nova) ni ongezeko la ghafla la mwangaza wa nyota. Ilhali idadi kubwa za nyota hazionekani kwa macho matupu ongezeko hili linatokea mara nyingi kama "nyota mpya" angani inayoweza kung'aa sana hata kushinda nyota zote nyingine. Hivyo inaonekana kwa muda tu na kupotea tena kwa mtazamaji asiye na darubini.
Historia ya utazamaji
Zamani nyota zote zilizowaka hivi ziliitwa kwa jina lilelile "nova". Jina hili lilitumiwa mara ya kwanza na Tycho Brahe ambaye katika mwaka 1572 aliona nyota mpya katika eneo la kundinyota Mke wa Kurusi (Cassiopeia) na kueleza utafiti wake katika kitabu cha "De stella nova"(Kuhusu nyota mpya) [1]. Wakati huo Tycho Brahe alianzisha majadiliano kuhusu mafundisho ya wataalamu wa kale walioamini kwamba hakuna mabadiliko yoyote kwenye anga ya nyota[2].
Hata kabla ya Tycho kulikuwa na taarifa kuhusu nyota zilizotokea angani. Taarifa ya kale zaidi ni ya wanaastronomia nchini China kwenye mwaka 185 baada ya Kristo kuhusu "nyota geni" iliyoonekana karibu na Rijili Kantori (α Centauri). Nova nyingine ilitazamiwa mwaka 1054 na kurekodiwa na wanaastronomia Wachina, Wajapani na Wakristo wa Baghdad. Mabaki yake huonekana hadi leo kama "Nebula ya Kaa" katika eneo la Tauri (Taurus).
Tofauti kati ya Nova na Supanova
Tangu karne ya 20 vipimo na elimu iliyopanuka vilifanya wanaastronomia kutofautisha kati ya "nova" na "supanova" ambazo zote ni "nyota mpya" zinazotokea angani kwa muda ila kwa sababu tofauti.
- Nova ya Tycho Brahe pamoja na ile ya mwaka 1054 siku hizi zinaitwa "supanova" maana zilikuwa ni milipuko ya nyota zilizoharibiwa wakati wa matukio haya. Kiini cha nyota kinajikaza hadi kutokea kwa shimo jeusi au nyota ya nyutroni. Sehemu za nje zinarushwa mbali. Inayobaki ni wingu la mata yake iliyosambaa katika eneo kubwa kama ile ya Nebula ya Kaa. Nishati inayopatikana katika mlipuko wa supanova inazidi ile ya kuwaka kwa nova mara nyingi, hivyo uteuzi wa jina la "supa"-nova (yaani nova kuu).
- Neno "nova" linafahamika sasa ni kuwaka kwa muda kwa nyota ndani ya mfumo wa nyota maradufu. Katika hali ya nova, nyota huongeza mwangaza ghafla mara elfu kadhaa ya kawaida yake hadi kurudi tena baada ya wiki au miezi katika hali yake kama kabla ya kuwaka. Pia hapa inawezekana kwamba wingu linabaki lakini nyota yenyewe bado iko.
Tabia za nova
Nyota nova za kawaida zinatokea katika mfumo wa nyota maradufu. Nadharia inayokubalika na wengi inasema: nyota kibete cheupe na nyota kubwa, hasa jitu jekundu, zinazungukana kwa umbali wa karibu. Kibete cheupe kimeshamaliza hidrojeni yake na kujikaza, hivyo graviti yake bado ni kubwa ingawa mjao wake ni mdogo, pia ina joto. Jitu jekundu la jirani linaendelea kupanuka. Hapa sehemu ya mata ya tabaka za nje ya nyota kubwa inavutwa na graviti ya nyota ndogo na kuhamia upande wake. Sehemu ya mata hii ni hidrojeni inayokusanyika kwa umbo la diski ya uongezekaji[3] inayozunguka Kibete Cheupe na hatimaye kufikia karibu zaidi na kuunda angahewa. Hidrojeni hii inapashwa moto na uso wa Kibete Cheupe hadi kufikia halijoto ya kutosha ya kuanzisha myeyungano wa kinyuklia (nuclear fusion).
Mchakato huu unazalisha kiasi kikubwa cha nishati na kurusha sehemu ya hidrojeni inayowaka kwenye anga ya nje. Hii inaongeza mwangaza wa nyota inayoonekana sasa kama nyota nova. Kiasi cha masi inayorushwa angani wakati wa kuwaka inalingana takriban na 1/10,000 ya masi ya Jua.
Maendeleo ya nova inafuata hatua kama hizi:
- wakati myeyungano wa kinyuklia unaanza usoni mwa Kibete Cheupe mwangaza wake unaongezeka takriban mag 9 katika kipindi cha siku chache.
- mara nyingi mwangaza unabaki huohuo kwa siku kadhaa; hatua hii haikutazamiwa kwa kila nova
- baada ya siku hadi wiki kadhaa mwangaza unaongezeka tena kiasi cha mag 2.
- kutoka kilele hiki mwangaza unaanza kupungua kwa kiai cha mag 3.5
- katika hatua inayofuata kuna kupoa tena, kwa mag 3, katika muda wa miezi hadi miaka kadhaa
- katika miaka au miongo inayofuata mwangaza unaendelea kupungua hadi kufikia tena hali ya awali.
Kugunduliwa kwa nova
Kila mwaka kuna takriban nyota nova 10 zinazotazamwa katika Njia Nyeupe[4]. Lakini wanaastronomia hukadiria kwamba idadi halisi ni kubwa zaidi, labda takribani 50 zinazotokea kila mwaka katika galaksi yetu[5].
Nyota nova zinagunduliwa pia katika galaksi nyingine, kwa mfano katika galaksi ya Andromeda (M31) na penginepo[6].
Nova za kurudia
Kinadharia mchakato huu unaweza kurudia mara kadhaa kwa sababu baada ya mlipuko wa angahewa ya nyota ndogo, mata kutoka jirani inaanza kuvutwa tena. Nyota RS Ophiuchi katika kundinyota ya Hawaa ilitazamwa kuwaka mara sita[7]: 1898, 1933, 1958, 1967, 1985 na 2006.
Hadi sasa kuna nyota nova 10 zilizotazamwa kuwaka tena kati ya takriban 400 zilizogunduliwa katika Njia Nyeupe[8]; kwa hiyo hakuna uhakika bado kuhusu muda wa kawaida uliopo baina ya kuwaka kwa nyota. Kama nyota kibete imeendelea kukusanya mata nyingi kuna uwezekano kwamba inalipuka mwishoni kama supanova [9]
Tanbihi
- ↑ Kilatini kwa "Kuhusu nyota mpya", linganisha Tycho's Supernova Remnant Archived 7 Agosti 2016 at the Wayback Machine., tovuti ya NASA, iliangaliwa Februari 2108
- ↑ Majadiliani yaliendelezwa na Johannes Kepler aliyeandika mwaka 1606 pia kuhusu "Stella Nova in pede Sagitarii" (kuhusu nyota mpya mguuni pa kundinyota Kausi)
- ↑ ing. "accretion disk"
- ↑ List of Novae in the Milky Way, tovuti ya Central Bureau for Astronomical Telegrams, iliangaliwa Februari 2018
- ↑ Shafter, A.W. (January 2017). "The Galactic Nova Rate Revisited". The Astrophysical Journal. 834 (2): 192–203
- ↑ M31 (Apparent) Novae Page, tovuti ya Central Bureau for Astronomical Telegrams, iliangaliwa Februari 2018
- ↑ Brandi, E.; Quiroga, C.; Mikołajewska, J. (2009). "Spectroscopic orbits and variations of RS Ophiuchi". Astronomy and Astrophysics. 497
- ↑ M. J. Darnley, V. A. R. M. Ribeiro1,2, M. F. Bode, R. A. Hounsell, and R. P. Williams, ON THE PROGENITORS OF GALACTIC NOVAE, The Astrophysical Journal, Volume 746, Number 1, Published 2012 January 25
- ↑ Sababu yake ni ya kwamba graviti yake inaweza kuzidi shinikizo ya mnururisho ndani yake ambayo kwa kawaida inatunza uwiano ndani ya nyota
Marejeo
- Tichonis Brahe De nova et nullius aevi memoria prius visa stella, ("Kuhusu nyota nova ambayo haikuwahi kutazamiwa katika maisha au kumbukumbu ya mtu yeyote", mwaka 1573) , kwenye tovuti ya archive.org