Johannes Kepler
Johannes Kepler (27 Desemba 1571 – 15 Novemba 1630) alikuwa mtaalamu wa astronomia, hisabati, theolojia na muziki kutoka nchini Ujerumani.
Amekuwa maarafu hasa kwa sababu alitambua kanuni za mwendo wa sayari zikilizunguka Jua.
Kazi yake
Alianza masomo yake kwenye chuo kikuu cha Tuebingen katika fani ya theolojia akilenga kuwa mchungaji. Pamoja na theolojia alisoma pia hisabati halafu akafuata mwito wa kuwa mwalimu wa hisabati kwenye chuo cha Kiprotestanti mjini Graz (Austria). Baadaye aliitiwa Praha (leo nchini Ucheki) kama msaidizi wa Tycho Brahe aliyekuwa mwanahisabati rasmi wa Kaisari Rudolph II. Baadaye Kepler alipewa wajibu huu.
Kepler alitambua ya kwamba makadirio ya Nikolaus Kopernikus yalionyesha hali halisi, maana yake sayari pamoja na dunia zinazunguka jua. Hadi wakati ule wataalamu waliamini ya kwamba dunia yetu iko katikati ya ulimwengu na jua pamoja na sayari zinazunguka dunia.
Kanuni za mwendo wa sayari
- Kanuni ya kwanza inasema sayari inatembea njia yenye umbo la duaradufu, si duara kamili, ikizungukia jua. Kabla ya Kepler wanaastronomia waliona njia ya sayari ni duara kamili.
- Kanuni ya pili inasema ya kwamba sayari inaongeza mwendo ikikaribia Jua, lakini inapunguza mwendo ikienda mbali na Jua.
- Kanuni ya tatu inaeleza ya kwamba sayari iliyo karibu na Jua ina kasi kubwa kuliko sayari ambayo ipo mbali.
Kwa kanuni zake aliweza kutabiri mahali pa sayari angani vizuri kushinda wataalamu wote waliomtangulia.
Sala yake
“Kwako wewe, ambaye kwa mwanga wa uasilia unachochea ndani mwetu hamu ya neema yako ili tuweze kufurahia utukufu wako, kwako natoa shukrani, Bwana wangu na Mungu wangu, kwa sababu umenifanya kuonja furaha na raha katika vile vyote ulivyoviumba, katika vile vyote vilivyo kazi ya mikono yako azizi. Tazama, ee Bwana, nimemaliza kazi hii iliyokuwa wito wangu. Ili kuifanya nimetumia ile nguvu ya akili uliyonijalia wewe. Nimewaonyesha binadamu ukuu wa kazi yako, au walau sehemu ile ya ukuu wako usio na mipaka ambayo akili yako imeweza kuelewa.”[1]
Tanbihi
- ↑ Mwishoni mwa kitabu Harmonices mundi, 1618.
Viungo vya nje
- Annotation: Posner Family Collection in Electronic Format Archived 31 Januari 2009 at the Wayback Machine. Harmonices mundi ("The Harmony of the Worlds") in fulltext facsimile; Kilatini
- Electronic facsimile-editions of the rare book collection at the Vienna Institute of Astronomy
- Kepler and the "Music of the Spheres"
- Gale E. Christianson- Kepler's Somnium: Science Fiction and the Renaissance Scientist
- Kepler's Belief in Astrology by Nick Kollerstrom
- References for Johannes Kepler
[[Jamii:{{ #if:1571|Waliozaliwa 1571|Tarehe ya kuzaliwa