Kindi-miamba

(Elekezwa kutoka Petromus typicus)
Kindi-miamba
Kindi-miamba (Petromus typicus)
Kindi-miamba (Petromus typicus)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mammalia (Wanyama wenye viwele wanaonyonyesha wadogo wao)
Oda: Rodentia (Wagugunaji)
Nusuoda: Hystricomorpha (Wanyama kama nungunungu)
Familia: Petromuridae (Kindi-miamba)
Jenasi: Petromus
A. Smith, 1831
Spishi: P. typicus
A. Smith, 1831

Kindi-miamba (Petromus typicus) ni mnyama mgugunaji mdogo na spishi pekee ya familia Petromuridae. Kinyume na jina lake mnyama huyu si kindi lakini jamaa ya nungunungu. Spishi hii inatokea Namibia na sehemu za Angola na Afrika Kusini katika maeneo yenye miamba. Jina la “Petromus” linatoka kwa Kilatini petra = mwamba na mus = kipanya.

Kindi-miamba wanafanana na kindi lakini mkia wao mrefu si mnono kama ule wa kindi. Mwili wao una urefu wa sm 13-18 na mkia ni sm 14 kadiri. Wana miguu mifupi yenye vidole vinne mbele na vitano nyuma. Nyayo zao ni tupu kabisa na zina mafumba. Kichwa chao ni chembamba juu-chini na masikio ni madogo na ya duara. Rangi yao ni kahawia, kijivu au takriban nyeusi ili kuchukuana na rangi ya miamba, lakini pua ni njano na ijitokeza. Hawana malaika. Chuchu zipo mbavuni ili kunyonyesha watoto kutoka upande wakati wamesongamana katika mwanya wa mwamba.

Usambazaji na mwenendo

hariri

Kindi-miamba wanatokea miamba ya Namibia, ya kusi ya Angola na ya kaskazi-magharibi ya Afrika Kusini. Wanyama hawa hujulikana kwa uwezo wao wa kujibanza katika mianya myembamba sana. Hii inafanikishwa kwa sababu ya fuvu lao jembamba juu-chini na mbavu yao kinamo.

Hula manyasi hasa lakini pengine matunda, mbegu na majani pia. Wana meno yenye kichwa kirefu na mizizi mirefu. Jike huzaa jozi ya watoto mara moja kwa mwaka, kiwango kidogo cha kuzaa kisicho kawaida baina ya wagugunaji. Watoto hulikizwa baada ya wiki tatu lakini waendelea kutegemea wazazi wao muda wa miezi tisa[1].

Kindi-miamba ni mwana abakiye peke yake wa familia ya spishi nyingi ambayo ilionekana wakati wa Oligocene ya Afrika. Uchunguzi wa mofolojia na filojenetiki unadokeza kwamba ndezi ni jamaa wa karibu kabisa wa kindi-miamba. Familia hizi mbili, pamoja na familia Phiomyidae iliyokwisha sasa, ni mfano wa mtawanyiko mapema wa wagugunaji katika Afrika.

Marejeo

hariri
  1. Bishop, Ian (1984). Macdonald, D. (mhr.). The Encyclopedia of Mammals. New York: Facts on File. uk. 703. ISBN 0-87196-871-1.

Soma pia

hariri
  • Kingdon, J. 1997. The Kingdon Field Guide to African Mammals. Academic Press Limited, London.
  • McKenna, Malcolm C., and Bell, Susan K. 1997. Classification of Mammals Above the Species Level. Columbia University Press, New York, 631 pp. ISBN 0-231-11013-8
  • Nowak, R. M. 1999. Walker's Mammals of the World, Vol. 2. Johns Hopkins University Press, London.

Viungo vya nje

hariri