Reli ya Kenya-Uganda
Makala hii yaeleza habari za njia ya reli ya kihistoria kati ya Mombasa na Uganda. Kwa habari za Shirika ya Reli ya Uganda ya kisasa tazama Uganda Railways Corporation.
Reli ya Kenya-Uganda ni jina kwa reli kati ya Mombasa na Kampala iliyojengwa na Waingereza kuanzia mwaka 1896. Mwanzoni ilijulikana kwa jina la "Reliya Uganda" tu. Reli hii ilisababisha Uingereza kutafuta utawala juu ya eneo ambako njia ya reli ilipita. Eneo hili lilikuwa baadaye koloni na nchi ya Kenya. Hali halisi njia ya reli hii ilijengwa katika Kenya pekee hadi ziwa Viktoria Nyanza ambako usafiri uliendelea kwa njia ya meli hadi Uganda. Tangu 1931 kulikuwa na nyongeza ya njia ya reli hadi Uganda yenyewe.
Utanguliza wa kujenga reli
haririBiashara ya Uganda
haririReli ilijengwa kwa sababu Kampuni ya Kifalme ya Uingereza kwa Afrika ya Mashariki IBEA (Imperial British East Africa Company) ilitaka kuboresha usafiri wa kwenda Uganda baada ya Uganda ilitangazwa nchi lindwa na Uingereza na kampuni ilitaka kuchukua nafasi hii ya kuanzisha mashamba ya kibiashara huko yasiyokuwa na faida bila usafiri wa kupeleka mazao kwenye masoko ya dunia.
Mwenye kampuni ya IBEA William MacKinnon alianzisha biashara kati ya Mombasa na Uganda lakini safari hizi kwa magari ya maksai zilikuwa ngumu na ghali sana. MacKinnon alianza kushawishi Serikali ya Uingereza na kudai reli ijengwe. Awali serikali ya Uingereza ilisitasita kwa sababu faida ya kiuchumi haikuonekana pia Uingereza wakati ule haikupenda kuongeza idadi ya koloni zake ikipendelea kuwaachia watu binafsi na makampuni yao shughuli za kufungua masoko mapya katika nchi kama Uganda.
Maeneo ambayo ni Kenya ya leo yalifikiriwa wakati ule kukosa thamani ya kiuchumi kabisa.
Mashindano na Wajerumani
haririMipango hii ya kujenga biashara ya kampuni ilikuwa hatarini kutokana na uenezaji wa Ujerumani katika Afrika ya Mashariki. Mwaka 1890 mwakilishi wa kampuni kikoloni ya kijerumani Karl Peters alifaulu kusaini mapatano na Kabaka; wakati uleule Wajerumani walionekana kupanusha eneo la Witu kwenye pwani la Kenya na Somalia. Hapo serikali za nchi zote mbili ziliamua kumaliza mashindano kati ya makampuni haya kwa kuelewana juu ya mipaka ya maeneo katika Afrika kwa mapatano kati ya Uingereza na Ujerumani ya 1890.
Azimio la kujenga reli na mwanzo wa Kenya
haririMkataba huu ulifanya shughuli za Afrika ya Mashariki kuwa rasmi chini ya serikali ya Uingereza. Kutokana na azimio hili Uingereza iliamua 1894 kuitangaza Uganda kuwa chini ya ulinzi wake na pia kujenga reli kama njia ya kuhakikisha utawala wake na kuweka msingi wa uzalishaji mali huko Uganda kwa ajili ya soko la dunia.
Baada ya azimio la kujenga reli Uingereza iliona haja ya kulinda njia ya reli yenyewe hivyo ikatangaza eneo lote kati ya Mombasa na Uganda kuwa chini ya ulinzi wake kuanzia tar. 01.07.1895. Kwa njia hii mipango ya kujenga reli ilikuwa mwanzo wa koloni ya Afrika ya Mashariki ya Kiingereza iliyokuwa Kenya baadaye.
Ujenzi wa reli
haririMwezi wa Mei 1896 ujenzi ulianzishwa Mombasa chini ya uongozi wa mhandisi George Whitehouse. Alikuwa na bajeti ya BP 3,250,000. Kazi ilionekana ngumu sana kwa sababu ya maeneo magumu kama vile jangwa, kinamasi, milima, Bonde la Ufa na mtelemko wake, kwa ujumla zaidi ya 1000 km.
Wafanyakazi kutoka Bara Hindi
haririWaingereza waliamua kuchukua wafanyakazi kutoka Bara Hindi kwa sababu katika majaribio ya kwanza Waingereza hawakuelewana na wenyeji wa pwani ambao waliajiria awali. Kwa ujumla zaidi ya Wahindi 13,000 walichukuliwa kufanya kazi ya reli. Kwa jumla walitoka hasa katika mikoa ya Gujarat na Panjab, na lugha hizi zinatumika hadileo katika Afrika ya Mashariki. Wengi walikuwa wafanyakazi wa mkono,lakini wengine pia mafundi na makarani. Wengi walikufa kwa sababu ya ugumu wa kazi, magonjwa, ajali na wanyama witu kama vile simba walioitwa wala-watu wa Tsavo walioua wafanyakazi 135.
Mwanzo wa Nairobi
haririMwaka 1899 reli ilifika eneo la Nairobi ya leo. Whitehouse aliamua kujenga hapa kambi kubwa kwa sababu mahali palikuwa na maji, tena takriban katikati ya Mombasa na Kampala, halafu kabla ya njia kupanda juu kwa milima inayoongozana na Bonde la Ufa. Kambi hii ilidumu ikawa mji wa Nairobi.
Tar. 20.12.1901 reli imefika Port Florence (leo: Kisumu)ufukoni wa ziwa la Viktoria Nyanza. Kutoka hapa bidhaa zilipelekwa kwa meli hadi Port Bell / Kampala. Njia ya reli yenyewe ilifika Kampala mw. 1931 kutoka Nakuru.
Mafanikio na matatizo
haririNi sawa kabisa kusema ya kwamba reli hii ilikuwa mwanzo na mbegu wa Kenya. Biashara ya Uganda haikuleta kabisa faida ya kiuchumi za kurudisha gharama za ujenzi lakini reli ilifungua sehemu kubwa za Kenya kwa ajili ya biashara ikawezesha kilimo ya kibiashara. Hivyo reli ilikuwa msingi kwa ajili ya mipango ya baadaye ya "White Highlands" ya kuunda koloni ya walowezi kama Afrika ya Kusini. Wahindi wengi walibaki wakawa mwanzo wa jumuiya ya Wakenya na Wauganda wenye asili ya kiasia.
Gharama zilikuwa kubwa. Bajeti ya kifedha haikutosha kabisa iliongezeka mara mbili. Gharama za maisha zilikuwa nzito zaidi. Wafanyakazi wahindi walikuwa wa kwanza kulipa bei hiyo. Magonjwa yaliyokuja nao yalisababisha vifo vingi kati ya wenyeji hasa Wakikuyu; makabila kama Wanandi waliopinga ujenzi wa reli yalikandamizwa vikali na Waingereza.
Viungo vya Nje
hariri- History of the Uganda Railway Ilihifadhiwa 26 Januari 2010 kwenye Wayback Machine.