Afrika Mashariki ya Kiingereza
Afrika Mashariki ya Kiingereza au Afrika Mashariki ya Kibritania ilikuwa eneo lililodhibitiwa na Uingereza katika Afrika ya Mashariki mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20. Eneo hili lilijumuisha hasa Kenya ya sasa na eneo la Jubaland (ambalo sasa ni sehemu ya Somalia). Liliundwa kama Himaya ya Ulinzi ya Afrika Mashariki ya Kiingereza mwaka 1895 na baadaye kubadilishwa jina kuwa Koloni na Himaya ya Ulinzi ya Kenya mwaka 1920. Waingereza walidhibiti eneo hili kwa sababu za kimkakati, ikiwa ni pamoja na kulinda njia za biashara, kupanua ushawishi wao barani Afrika, na kudumisha udhibiti wa pwani ya Bahari ya Hindi.
Afrika Mashariki ya Kiingereza British East Africa (Kiingereza) | |
---|---|
Wimbo wa taifa: God Save the Queen (1895–1901) God Save the King (1901–1920) | |
Mji mkuu | Mombasa (1895-1905) Nairobi (1905-1920) |
Mji mkubwa | Nairobi |
Lugha rasmi | Kiingereza |
Lugha za kikabila | Kiswahili Kikikuyu Kiluo Kikamba |
Serikali | Nchi lindwa ya Uingereza |
• Malkia | Viktoria (1895–1901) |
• Mfalme | Edward VII (1901–1910) |
• Mfalme | George V (1910–1920) |
Eneo | |
• Jumla | km2 696,400 |
Idadi ya watu | |
• Kadirio la 1904 | 4,000,000 |
Sarafu | Rupia ya Uhindi (1895–1906) Rupia ya Afrika Mashariki (1906–1920) |

Reli ya Uganda, iliyokamilika mwanzoni mwa karne ya 20, ilikuwa na mchango mkubwa katika utawala wa Uingereza, kwani ilirahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu. Hata hivyo, sera za Waingereza, hasa nchini Kenya, zilisababisha unyanganyaji wa ardhi, ambapo wakulima Wazungu walichukua nyanda za juu zenye rutuba, na kuwafukuza wenyeji. Hali hii ilisababisha upinzani mkali, uliokuja kuonekana katika vuguvugu kama Maasi ya Mau Mau (1952–1960). Kufikia katikati ya karne ya 20, harakati za utaifa ziliongezeka, zikisababisha Kenya kupata uhuru mwaka 1963, huku Jubaland ikiingizwa katika Somaliland ya Italia mnamo miaka ya 1920, na hatimaye kuwa sehemu ya Somalia ya sasa.
Historia
haririWakati wa mashindano ya kugawa Afrika kati ya madola ya Ulaya, Kampuni ya Kifalme ya Kiingereza kwa Afrika ya Mashariki ilianza shughuli zake katika eneo hili kwa kibali cha sultani wa Zanzibar kuanzia mwaka 1888.
Kampuni hiyo ilitakiwa kuwa na mamlaka juu ya eneo hili kwa kusudi la kufanya biashara, lakini uwezo wake haukutosha kutimiza shughuli, hasa maandalizi ya kujenga reli ya Uganda kati ya Mombasa na Kampala.
Baada ya kuazimia kujenga reli, Uingereza iliona haja ya kulinda eneo la reli hiyo: ndipo ikatangaza eneo lote kati ya Mombasa na Uganda kuwa chini ya ulinzi wake kuanzia tarehe 1 Julai 1895. Huo ndio mwanzo wa Afrika ya Mashariki ya Kiingereza ambaye baadaye iliitwa Kenya.
Eneo hilo baadaye lilipanuliwa zaidi hadi kukutana na maeneo yaliyokuwa chini ya utawala wa Italia (Somalia) na Ethiopia upande wa Kaskazini, utawala wa ushirikiano wa Misri na Uingereza (Sudan). Upande wa kusini mpaka ulifuata mapatano na Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.
Mpaka na eneo chini ya utawala wa ulinzi wa Uganda ulisahihishwa mwaka 1905; hadi wakati ule sehemu kubwa ya eneo la Kenya ya Magharibi ya leo ilihesabiwa kuwa upande wa Uganda.
Baada ya vita kuu ya kwanza hali ya eneo ilibadilishwa kuwa koloni la Kenya kuanzia 1920.
Marejeo
haririMakala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Afrika Mashariki ya Kiingereza kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |