Schutzstaffel - SS

(Elekezwa kutoka SS)

Schutzstaffel (Kikosi cha ulinzi) -kwa kifupi SS- ilikuwa jina la kitengo cha Chama cha Nazi au NSDAP nchini Ujerumani kilichoanzishwa mwaka 1925kama kundi la walinzi wa kiongozi wa chama Adolf Hitler. SS ilishiriki katika maangamizi makuu dhidi ya Wayahudi wa Ulaya na kutawala makambi ya mauti. Kutoka kundi dogo la walinzi wa binafsi iliendelea kuwa tawi la kijeshi la Chama cha Nazi lililoshiriki pia kwenye mapigano ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Ikapigwa marufuku kama chama cha kihaini mwaka 1945.

Alama ya SS zilikuwa S mbili kwa mwandiko wa Kigermanik

Kuundwa kwa SS

hariri

SS iliundwa kama kitengo cha wanamgambo wa NSDAP waliojulikana kama SA. Awali kazi ya wanamgambo 8 walioteuliwa ilikuwa kumlinda kiongozi wa chama Adolf Hitler kwenye maandamano na mikutano ya chama. Tangu 1929 iliongozwa na Heinrich Himmler. Wakati ule kikosi kilikuwa na wanachama 280. Himmler aliendelea kupanua kikosi. Hadi mwisho wa 1929 alikuwa wanamgambo 1,000 chini yake waliongezeka kuwa 52,000 mwaka 1932.

Baada ya Hitler kuwa chansela wa Ujerumani 1933 kikosi kilikua kuwa na watu 204,000.

Mapigano ndani ya NSDAP na SS kuwa kitengo cha pekee

hariri

Mwaka 1934 Hitler aliamua kuwaondoa viongozi wa wanamgambo wa SA waliokuwa na mawazo yao ya pekee kuhusu maendeleo ya utawala wa Kinazi katika Ujerumani. Hitler alitumia SS kwa kazi hiyo. Tarehe 30 Juni na 1 Julai 1934 vikundi vya SS walikamata na kuua viongozi wengi wa SA.

Wiki chache baadaye SS ikapandishwa cheo kuwa kitengo cha pekee ndani ya chama cha NSDAP. Himmler alipewa cheo cha "Reichsführer" au kiongozi wa kitaifa wa SS.

Ndani ya SS vikajitokeza matawi matatu:

  • SS ya kawaida iliyounganisha wana-SS wote wasioshiriki katika vitengo vingine
  • SS ya fuvu walipewa kazi ya ulinzi katika makambi ya KZ kwa wafungwa wa kisiasa
  • kikosi cha ulinzi wa Hitler kilichojengwa kuwa tapo la kijeshi lililolinda majengo na mahali alipokaa Hitler lakini nje ya muundo wa jeshi la Ujerumani

Itikadi ya SS

hariri

Himmler alijenga tangu mwanzo itikadi mpya wa SS. Yeye alikuwa katika mstari wa mbele wa wanaitikadi wa kimbari ndani ya NSDAP. Itikadi hii iliamini kuwa watu wa mbari wa "Kiarya" walikuwa watu bora duniani. Hiyvo alipokea katika SS watu pekee waliotosheleza mafundisho haya ya kimbari. Kila mwana-SS alipaswa kuonyesha ya kwamba hapakuwa na Wayahudi katika ukoo wake na kuwa na afya nzuri.

Wana-SS wote walipaswa kuhudhuria mafundisho ya mara kwa mara walipopewa mafundisho ya kisiasa na kiitikadi.

Idadi kubwa ya wana-SS bado walikuwa na kazi za kawaida lakini kadi ya SS ilikuwa kiingilio katika vyeo vya juu serikalini. Vilevile idadi ya kazi za kulipwa ndani ya kikosi ikaongezeka.

Sehemu kubwa ya kazi ya SS ilikuwa kusambaza itikadi ya "mbari safi" ya Kiarya. Himmler aliota ndoto ya kuongeza idadi ya watu wenye mbari safi hadi kuwafuga hata akachukua hatua za kwanza za kuteua vijana waliolingana na imani zake za kimbari na kuwapa nafasi ya kuzaa hata pasipo na ndoa. Kuna watoto maelfu kadhaa waliozaliwa katika nyumba za pekee na kulelewa kama watoto wa SS ama katika nyumba hizi au katika familia zilizoteuliwa. Nje ya Ujerumani alitafuta hasa vijana wa Norwei kwa sababu walilingana na itikadi yake ya mbari ya Waarya.

SS na Polisi

hariri

Tangu 1936 Himmler alipewa pia cheo cha mkuu wa kitaifa wa polisi. Hadi wakati ule polisi iliwahi kuwa chini ya serikali za majimbo ya Ujerumani. Hata kama majimbo haya yote yalikuwa chini ya NSDAP hatua hii iliongeza athira ya moja kwa moja wa uongozi wa kitaifa wa chama juu ya maafisa wa usalama. Maafisa wakuu wa polisi walipaswa kujiunga na SS. Maafisa wa SS walisimamia shughuli za polisi hasa idara za CID na idara za polisi ya usalama wa kisiasa. Pia vikosi vya kupambana na ghasia vikawekwa chini ya usimamizi wa SS.

Uongozi mkuu wa polisi pamoja idara ya usalama wa SS vikaunganishwa katika ofisi kuu ya usalama (RSHA au "Reichsicherheitshauptamt").

SS na Vita Kuu

hariri

Mwanzoni wa vita kuu ya pili ya dunia SS iliomba na Hitler kupewa kibali cha kuanzisha vikosi "SS silaha"" (Waffen-SS) vilivyoshiriki katika mapigano vitani. Kitengo hiki cha Waffen-SS kikaongezewa katika miaka iliyofuata hadi kufikia wanajeshi 900,000 mwaka 1944. Shabaha ya Himmler ilikuwa kupata jeshi lake kwa sabau hakuwa na imani katika itikadi ya majenerali wa jeshi la kawaida.

Tangu 1933 chama cha Kinazi kilianza kuwabagua Wayahudi wa Ujerumani. 1933 walifukuzwa katika ajira ya serikali na tangu 1935 waliondolewa uraia wa Ujerumani. 1939 baada kuanzisha vita viongozi waliamua kuwaondoa Wayahudi wote waliobaki katika Ujerumani. Mwanzoni walikuwa na mpango wa kuwahamisha mahali popote nje ya Ujerumani. Mipango hii pamoja na yale yaliyofuata ikakabidhiwa mkononi mwa SS iliweza kudai usaidizi wa idara mbalimbali za serikali ya Ujerumani, polisi, huduma za reli na vitengo vingine.

Kati ya mipango mbalimbali ilikuwa mipango ya kuwapeleka Madagaska (baada ya kuteka Ufaransa iliyotawala kisiwa kama koloni) na hasa Poland iliyotwaliwa na Ujerumani 1939.

Baada ya kuanza vita dhidi ya Urusi imeshaonekana ya kwamba Wanazi walishindwa kushughulika idadi kubwa ya Wayahudi katika maeneo ya Ulaya ya Mashariki yaliyotekwa na Ujerumani. Kufuatana na itikadi yao walitaka kuwatenga Wayahudi na watu wengine lakini walishindwa kuwapatia nyumba na kuwalisha. Pia ilionekana kwa viongozi wa juu ya kwamba vita dhidi ya Urusi haikuenda jinsi ilivyopangwa na kuingia kwa Marekani vitani kuliongeza matatizo. Katika hali hii wakati wa mwisho wa 1941 / mwanzo wa 1942 walichukua hatua ya kuamua kile walichoita "usuluhisho wa mwisho wa swali ya Kiyahudi" yaani mauaji wa Wayahudi wote wa Ulaya.

Mpango huu ulikabidhiwa mkononi wa SS iliyochukua hatua za kuanzisha mauaji makubwa katika historia ya binadamu. Mwanzoni Wayahudi wengi waliuawa kwa kuwapiga risasi maelfu. Baada ya kuona ya kwamba kuwaua watu malakhi na mamilioni kwa njia hii kulishinda uwezo wao mpango wa makambi ya mauti ulianzishwa.

Makambi yalijengwa ambako watu walipelekwa kwa treni kutoka Ulaya kote. Baada ya safari ndefu waliangaliwa na madaktari. Wenye afya waliwekwa kando na kupelekwa katika sehemu ya kambi ambako walipaswa kufanya kazi kama watumwa katika viwanda vilivyojengwa huko hasa. Wengine kama wagonjwa, wazee na watoto pamoja na wakinamama walitengwa na kuambiwa kuingia katika chumba kikubwa cha bafu chenye 210 m² walipotakiwa kujisafisha baada ya safari ndefu. Milango ikafungwa na gesi ya sumu badala ya maji ikaingizwa katika chumba kupitia vifaa vya manyunyu. Waliokufa walikuwa watu 500-700 kila safari. Maiti zikatolewa; midomo ikachunguliwa kama mtu alikuwa na dhahabu kwenye meno iliyotolewa halafu maiti zikachomwa katika meko makubwa.

Katika makambi sita za aina hii jumla ya watu milioni 4-5 waliuawa. Pamoja na wale waliouawa nje ya makambi ni mnamo watu milioni sita waliouawa kikusidi. Walio wengi sana walikuwa Wayahudi lakini pia vikundi vingine visivyolingana na itikadi ya kimbari kama vile Wasinti, walemavu, shoga na wafungwa wakomunisti.

 
Maiti ya Himmler 1945

Mwisho 1945

hariri

Mwisho wa vita SS ikatangazwa na washindi kuwa kundi la kigaidi na kupigwa marufuku. Himmler alijiua tar. 23 Mei 1945 baada ya kukamatwa na Waingereza. Viongozi wengi walijaribu kujificha au kujiua kabla ya kukamatwa. Wengine walifaulu kujificha wakikimbia hadi Amerika Kusini.