Simeon Nyachae (6 Februari 1932 - 1 Februari 2021) alikuwa mwanasiasa na mfanyabiashara nchini Kenya.

Maisha hariri

Alizaliwa katika kata ndogo ya Nyaribari, Wilayani Kisii Mkoani Nyanza. Amehudumu katika nyadhifa mbali mbali katika serikali za Kenyatta, Moi na Kibaki.

Kwa miaka mingi Nyachae alionekana kama kiongozi wa Kisii hadi alipong'atuliwa kutoka bungeni katika uchaguzi wa Bunge la Kenya 2007.

Nyachae alizaliwa katika familia kubwa ya chifu Musa Nyandusi. Nyachae alipata fursa ya kupata elimu kutokana na ushawishi kutoka kwa babake, ambaye alifaidika na elimu ya wakoloni hadi alipoteuliwa chifu. Mnamo mwaka wa 1941, Nyachae alijiunga na shule ya Nyanchwa Seventh Day Adventist School na kisha mwaka wa 1947, akajiunga na Kereri Intermediate School. Miaka miwili baadaye, akajiunga na shule ya Kisii Government African School. Ilipofikia mwaka wa 1953, kabla ya kufanya mtihani wake wa Ordinary Level School Certificate, akaajiriwa katika kambi ambako babake alipofanyia kazi kama karani wa wilaya.

Mtumishi wa Umma hariri

Katika (mwaka wa 1957) Nyachae akaenda Uingereza kwa masomo ya utawala wa jamii (Public Administration) na aliporudi Kenya mwaka 1960, akawa Mkuu wa wilaya katika divisheni ya Kangundi. Alirudi Uingereza kwa masomo zaidi katika chuo cha Churchill huko Cambridge na kupata cheti cha Utawala wa Jamii. Aliporudi tena Kenya aliendelea kupanda ngazi katika Utawala wa Mikoa hadi kuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma katika serikali za Kenyatta na Moi.

Mwanasiasa wa KANU hariri

Nyachae alistaafu kutoka kwa utumishi wa umma mnamo mwaka wa 1987 akaanza kujenga maisha yake ya kisiasa. Katika mwaka 1992 alichaguliwa mara ya kwanza kama mbunge wa Nyaribari Chache na Rais Moi akamteua kuwa Waziri wa Kilimo. Mwaka wa 1997 akawa Waziri wa Fedha. Mwaka mmoja baadaye, Rais Moi alimteua kama Waziri wa Usitawi na Nyachae akakataa na kujiuzulu kama Waziri na pia kutoka chama cha KANU, na akjiunga na Ford-People, chama kidogo cha upinzani, kilicho na ushawishi wa wanasiasa wa kutoka katika mkoa wa Kati.

Kiongozi wa Ford-People hariri

Katika uchaguzi wa 2002 Nyachae alikataa kujiunga na muungano wa National Rainbow CoalitionNARC ambao ulihusisha chama cha LDP kilichoongozwa na Raila Odinga, DP kilichoongozwa na Mwai Kibaki kama vyama vikuu. Katika uchaguzi huo chama cha Ford-People kilishinda viti 14 vingi vikiwa ni vya kutoka sehemu za Kisii. Kando na Ford-P chama kingine kilichokuwa na ushawishi bungeni upande wa upinzani kilikuwa chama cha KANU.

Waziri katika serikali ya Kibaki hariri

Wakati NARC ilianza kuporomoka kuanzia mwaka 2004 kutokana na tofauti za kisiasa, Rais Kibaki alitafuta kura za wabunge wa Ford-P na kumteua Nyachae Serikalini kama Waziri wa Nishati baadaye wa Barabara.

Katika uchaguzi wa 2007 wimbi la ODM lilibomoa mipango yake pamoja na nafasi ya Ford-P katika Kisii. Nyachae pamoja na idadi kubwa ya mawaziri wa Kibaki hakuchaguliwa tena.

Viungo vya nje hariri

  Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Simeon Nyachae kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.