National Rainbow Coalition

(Elekezwa kutoka NARC)

National Rainbow Coalition (NARC) ni chama cha kisiasa nchini Kenya kilichoanzishwa kabla ya uchaguzi wa mwaka 2002.

NARC kama muungano ya vyama

hariri

Ilikuwa muungano wa vyama mbalimbali vya upinzani dhidi ya KANU na rais Daniel arap Moi. Ilikuwa hasa na pande mbili:

Memorandum of Understanding

hariri

Msingi wa ushirikiano ulikuwa mapatano kati ya pande za NARC yaliyoitwa "Memorandum of Understanding" (MoU). Hapo walipatana ya kuwa:

  • Kibaki atakuwa rais, Michael Wamalwa makamu wake
  • NAK na LDP zitapewa kila upande nusu ya mawaziri katika serikali
  • katika muda wa siku 100 katiba itabadilishwa itakayopunguza mamlaka za rais
  • sehemu ya mamlaka za rais zitakabidhiwa kwa ofisi mpya ya waziri mkuu
  • Raila atakuwa waziri mkuu wa serikali ya NARC, Charity Ngilu makamu wake.

Ushindi na mwanzo wa farakano

hariri

NARC ikashinda uchaguzi wa 2002 na Kibaki akawa rais mpya. LDP ilikuwa na wabunge wengi kati ya vyama vya NARC. Lakini Kibaki hakutekeleza azimio la pamoja katika Memorandum of Understanding kupatia LDP nusu ya mawaziri wala kuwezesha mabadiliko ya katiba ya kumpa Odinga nafasi ya waziri mkuu. LDP iliendelea kudai mapatano yafuatwe, ikakataliwa na polepole kuelekea upande wa upinzani hata kama bado ilikuwa sehemu ya serikali.

NARC kutoshikamana kuhusu katiba 2005

hariri

Katika miaka iliyofuata farakano ilikua. Mwaka 2005 Kibaki alijaribu kupitisha katiba mpya isiyopunguza sana mamlaka za afisi ya rais. Hapa sehemu kubwa ya LDP pamoja na KANU wakiungana kwa harakati ya machungwa (ODM) walipinga pendekezo la katiba katika kura maalumu ya wananchi, na pendekezo likakataliwa na wananchi.

Kuondoka kwa LDP

hariri

Kibaki alijibu kwa kufuta serikali akiwaachisha mawaziri wote. Serikali mpya ilikuwa bila wawakilishi wa LDP tena. Sasa Raila pamoja na Uhuru wa KANU waliunda harakati mpya ya ODM (Orange Democratic Movement) kwa kusudi la kugombea uchaguzi wa 2007.

Hii ilikuwa mwisho wa NARC kama chama tawala.

Mabaki ya NARC

hariri

Kiongozi wa kisheria alikuwa Charity Ngilu asiyekubaliwa na sehemu ya viongozi waliokuwa karibu na rais. Hivyo walianzisha 2006 kitengo kipya kwa jina la NARC-Kenya iliyoingia 2007 katika maungano ya PNU ya Kibaki. Ngilu aliamua Septemba 2007 kusimama upande wa Raila Odinga. Katika uchaguzi wa 2007 NARC iliweza kusimamisha wagombea wachache nje ya maungano ya Orange Democratic Movement na watatu walichaguliwa.