Sun Yat-sen
Sun Yat-sen (12 Novemba 1866 – 12 Machi 1925) alikuwa kiongozi wa kisiasa nchini China aliyeshiriki katika mapinduzi ya China ya 1911 yaliyoondoa utawala wa kifalme nchini akawa rais wa kwanza wa Jamhuri ya China na mwanzilishi wa chama cha Kuomintang.
Maisha ya mapema na masomo Hawaii
haririAlizaliwa 1866 wakati wa utawala wa nasaba ya Qing katika kijiji cha Cuiheng kwenye jimbo la Guangdong karibu na pwani la Bahari ya Kusini ya China. Alipokuwa mtoto alisikia habari nyingi za mapinduzi ya Taiping kutoka kwa mwanajeshi wa zamani wa Taiping. Wakati wa kufikia umri wa miaka 10 alisafiri Hawaii alipojiunga na kakaye Sun Mei aliyewahi kuhamia huko na kuwa mfanyabiashara mtajiri aliyemwezesha mdogo wake masomo akaendelea kumsaidia hata baadaye. Sun alijifunza Kiingereza, hisabati na sayansi.
Kurudi China na kuwa daktari
haririMwaka 1883 alirudishwa China na kakaye aliyeogopa ya kwamba mdogo angeweza kugeukia Ukristo. Baada ya kurudi China alitambua hali ya nchi kuwa nyuma. Akajiunga na shule ya wamisionari Waanglikana mjini Hongkong akaendelea kusoma uganga na kuwa mtibabu mwaka 1892. Wakati wa masomo yake alibatizwa akawa Mkristo.
Kugeukia siasa ya mapinduzi
haririMaarifa yake katika nchi za nje yalimwonyesha jnsi gani China ilikuwa nyuma akasikitika juu ya siasa ya makaisari wa nasaba ya Qin. Aliandika mapendekezo ya matengenezo lakini tabaka ya viongozi haikutambua elimu yake yasiyofuata mapokeo ya Kichina hakusikiwa.
Mwaka 1894 Sun alianzisha vikundi vya Wachina wasioridhika na hali ya nchi kama yeye na kujadili mipango ya mapinduzi.
Miaka ya ugenini
hariri1895 kundi lake lilipanga mapinduzi mjini Kanton yaliyokandamizwa vikali na serikali; wenzake kadhaa waliuawa. Hapa Sun alilazimishwa kuondoka katika China. Miaka 16 iliyofuata alikaa nje huko Ulaya, Marekani, Kanada na Japani. Alikusanya fedha kwa mipango ya mapinduzi na kukusanya Wachina waliopinga serikali ya Qing.
1905 nchini Japan aliunda kundi la Tongmenghui lililokuwa mtangulizi wa chama cha Kuomintang cha baadaye. Kwa hatua alifukuzwa Japan akaenda Marekani. Wakati ule aliacha kuvaa nguo za Kuchina akakata nywele zake ndefu.
Rais wa kwanza wa China
haririTar. 10 Oktoba 1911 yalianza mapinduzi ya China kwa uasi wa jeshi la Wuchang. Aliposiki habari hizi Sun alirudi China katika Desemba 1911. Mkutano wa wawakilishi wa wanamapinduzi kutoka majimbo mengi ya China uliamua kumaliza utawala wa kifalme ukamteua Sun kama rais wa kwanza wa Jamhuri ya China iliyotangazwa tar. 1 Januari 1912.
Mwaka ule 1912 aliunganisha vikundi kadhaa akaunda chama cha Kuomintang. Vilevile akaita mkutano wa wawakilishi wa majimbo yote ya China waliokutana kama bunge la muda na kukubali sheria za kwanza.
Lakini mamlaka ya serikali ya mapinduzi ilikuwa dhaifu mno; haikuwa na jeshi kubwa, majimbo ya kusini yalitangaza uhuru kama nchi za pekee na jeshi kubwa la kialme katika kaskazini likasubiri jinsi gani mambo yangeendelea. Sun alilazimishwa kupatana na mkuu wa jeshi wa China kaskazini jenerali Yuan Shikai. Yuan aliahidi msaada wa jeshi lake kumaliza wafuasi wote wa Kaisari Pu Yi na kumlazimishi kukubali mwisho wa utawala wake. Sun alikubali kumwachia nafasi ya rais wa jamhuri. Kwa hiyo akajiuzulu tayari katika Februari 1912 na Yuan akachaguliwa rais mpya tar. 14 Februari 1912 aliyehamisha serikali mjini kwenda Beijing.
Majaribio ya kurudisha shabaha za mapinduzi
haririAlipoona mwaka 1913 ya kwamba Yuan alianzisha udikteta Sun alijaribu kumpindua akashindwa akapaswa kukimbilia Japan tena alipoongoza matengenezo ya chama cha Kuomintang. China penyewe vikundi na viongozi mbalimbali vikaendelea kupasua nchi kwa hiyo Sun alirudi 1917 akaanzisha serikali ya kieneo mjini Kanton iliyokuwa na mamlaka katika sehemu kubwa ya China kusini.
Alipanga kuwafukuza watawala wa kijeshi wa China ya kaskazini akaanzisha chuo cha kijeshi cha Whampoa alipomfanya Chiang Kai-shek mkuu wa chuo. Wakati ule aliamua kukubali pia wakomunisti Wachina katika chama cha Kuomintang kwa hiyo hata Zhou Enlai alikuwa mwalimu huko baada ya kifo cha Sun.
Sun aliandaa vita ya kupindua viongozi wa kijeshi wa kaskazini lakini 1925 alisafiri Beijing kwa majadiliano juu ya maungano ya China na viongozi wa huko.
Kifo na urithi
haririHapa mjini Beijing alikufa kutokana na kansa tarehe 12 Machi 1925 akiwa na miaka 58.
Anakumbukwa na kuheshimiwa China yote kama baba wa China ya kisasa.
Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Sun Yat-sen kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |