Upimaji ni kazi ya kutambua tabia za kitu kwa umakinifu. Mara nyingi tabia hizi zinatazamiwa kwa njia ya makadirio lakini kila kadirio hutegemeana na mtu mwenyewe anayekadiria. Pale ambako watu mbalimbali wanataka kulinganisha vitu viwili wakati wanatofautiana katika makadirio yao upimaji unaweza kuamua juu ya ukubwa, uzito na tabia nyingine.

Mwnazo wa vipimo ilikuwa biashara yaani tendo la kubadilishana vitu na bidhaa. Kazi hii ilihitaji vizio vya kulinganisha vitu mbalimbali.

Haiwezekani kupima kila tabia ya kitu fulani kwa mfano urembo au uzuri. Lakini tabia za kifizikia kama urefu, uzani, ujao, kasi n.k. zinapimika.

Taratibu asilia za vipimo

hariri

Kila utamaduni ulianzisha utaratibu wake wa vizio vya upimaji ukawa na vipimo vyake. Mara nyingi vizio vya kulingana na mwili wa kibinadamu vilitumiwa kama vile kidole, mkono, mguu au hatua. Isipokuwa kutokana na tofauti katika maumbile ya watu ilionekana ya kwamba vipimo asilia hivi vilikuwa tofauti kati ya eneo na eneo au nchi na nchi. Kwa mfano katika Ujerumani ya karne ya 19 palikuwa na vizio vya futi makumi kati ya urefu wa sentimita 25 hadi sentimita 33.5.

Nchi kadhaa zilisanifisha vipimo hivi na mfano wake ni muundo wa vipimo vya Uingereza vilivyoenea katika nchi nyingi wakati wa ukoloni na vingine kama futi au maili vinatumiwa mahali pengi hadi leo.


Utaratibu wa vipimo sanifu vya kimataifa

hariri

Baada ya mapinduzi ya Ufaransa ya 1789 utaratibu mpya ulianzishwa uliolenga kutumia vizio vya kisayansi vilivyolingana na muundo wa dunia yote. Mwanzo wake ulikuwa mita iliyoamuliwa ni sehemu moja kati ya sehemu milioni 40 za meridiani ya Paris (mstari kutoka ikweta hadi ncha ya kaskazini unaopita mji wa Paris). Vipimo vingine vilikuwa sehemu ya 10 (desimita), ya 100 (sentimita), ya 1000 (milimita) na kadhalika ya mita hii au kizidisho yake mara 10, 100 na 1,000 (kilomita).

Kizio hiki kilikuwa chanzo cha utaratibu wa vipimo sanifu vya kimataifa ulioendelezwa hata kwa tabia nyingine za kifizikia kama uzani, ujao, kasi na kadhalika. Matumizi na maendeleo ya utaratibu huo huangaliwa na Ofisi ya Kimataifa ya Vipimo mjini Paris.