Usimbishaji[1] (kwa Kiingereza: precipitation) ni maji yanayonyesha kutoka hewa hadi ardhini.

Dhoruba ya mvua
Dura ya maji duniani inaundwa na usimbishaji na uvukizaji

Maji hayo ni pamoja na mvua, theluji, mvua ya mawe na umande.

Usimbishaji unaanza pale ambapo hewa yenye joto na mvuke hupanda juu. Juu zaidi halijoto yake inapungua na mvuke ndani ya hewa unaanza kuwa matone ya maji. Kila wingu hufanywa na matone mengi madogo yanayoendelea kuelea hewani pamoja. Upepo unakoroga matone yale madogo mpaka yanagongana na kuunganika na hivyo kukua.

Kama matone ni makubwa ya kutosha yanaanza kuanguka chini kama mvua, theluji au mvua mawe. Hali inategemea halijoto katika mawingu na hewani pale matone yanapotelemka.

Kiasi cha usimbishaji ni muhimu kwa ajili ya tabia za hali ya hewa katika nchi au eneo fulani.

Kufanya mvua kwa mitambo hariri

Watu wameanza kufanya mvua kwa kukamua mawingu. Hapo punje ndogo za iodidi ya fedha zinatupwa mawinguni kwa njia ya ndege au makombora. Punje hizo zinakuwa viini vya kutonesha mvuke na kusababisha matone kukua hadi mvua kunyesha.

Teknolojia hiyo inatumika katika maeneo makavu. Inatumika pia katika maeneo ya kilimo ili kuzuia mvua mawe isiharibu mavuno.

Marejeo hariri

  1. Istilahi ni pendekezo la KAST
  Makala hiyo kuhusu "Usimbishaji" inatumia neno ambalo si kawaida na matumizi yake ni jaribio kwa jambo linalotajwa.
Wasomaji wanaombwa kuchangia mawazo yao.

Kamusi za Kiswahili ama zinatofautiana kuhusu matumizi ya neno hili au hazieleweki au hazina neno kwa jambo linalojadiliwa.