Washambaa

(Elekezwa kutoka Wasambaa)

Washambaa (au Wasambaa, kama wanavyojulikana sana) ni watu wa kabila kutoka eneo la Milima ya Usambara, kaskazini-mashariki mwa nchi ya Tanzania.

Mwaka 2001 idadi ya Washambaa ilikadiriwa kuwa 664,000.[1].

Washambaa wanaishi kwenye milima ya Usambara na lugha yao kubwa ni Kisambaa.

Historia hariri

Kuna uhakika na kuaminika kwamba, Wasambaa ni moja ya makundi ya Wabantu wanaotokea Afrika Magharibi na Kaskazini wakipitia nchi za Ethiopia na Kenya. Wasambaa ni tawi lilomegega kutoka kwa Waasu/Wapare. Wachaga n.k. pindi wakiwa safarini kuja Tanganyika miaka zaidi ya mia nane (800) iliyopita. Haya majina ya Wasambaa, Wachaga, Wapare n.k. hayakuwepo pindi hao Wabantu walipokuwa wanaingia Tanganyika, isipokuwa wamepeana wenyewe kundi na kundi kupitia utani na umaarufu au asili ya eneo.

Utawala wa Wasambaa ulikuwa imara sana na ngome maarufu ni huko Vugha ikawa Bumbuli pia kulikuwa na chifu, ila Vugha ndiyo inaonekana makao makuu ya Wasambaa hata kabla ya Mbegha kuingia Usambara.

Huyo miaka ya 1800 alitoroka huko Kilindi na kuja Usambaani kupitia Zia Bumbuli.

Mbegha (pia: Mbega baada ya 1700) ni jina la mtu muhimu katika historia ya Washambaa anayekumbukwa kama mfalme wao au mwene mkuu wa kwanza katika kundi hili. Familia ya watawala iliyoanzishwa naye hujulikana pia kama nasaba ya Kilindi.

Kufuatana na "Habari za Wakilindi, Mbegha kiasili alikuwa mtoto wa Mwarabu aliyetoka Pemba na kuhamia Kilindi na mke wake Mngulu. Inaonekana ya kwamba waliishi baadaye kati ya Wangulu. Mbegha anakumbukwa kama mtoto kigego aliyetangulia kupata meno ya juu iliyotazamiwa kama ishara mbaya kati ya makabila mbalimbali na mara nyingi waliuawa. Labda kwa sababu babake alikuwa Mwislamu mtoto aliruhusiwa kuishi lakini baada ya kifo cha wazazi na kakaye alinyimwa urithi wake na nduguye waliomkumbuka kama kigego na kumshtaki kuwa ni mchawi.

Mbegha aliamua kuondoka katika ukoo uliomkataa akawa mwindaji aliyeishi msituni. Alikuwa stadi sana kwa sababu alikuwa kati ya watu wa kwanza waliotumia mbwa wa kuwinda akampenda hasa mbwa wake " Chamfumu". Alipata umaarufu kwa sababu alifaulu kupunguza nguruwe mwitu waliokuwa tishio kubwa kwa wakulima na mazao kwa hiyo walimheshimu na kumpenda. Vijana walikuja kukaa naye akawafundisha mbinu za uwindaji.

Alisemekana kujua pia mbinu za uganga zilizomsaidia kuwinda, kuwashinda maadui na pia kuponya watu.

Baada ya kuondoka katika Ungulu alihamia kwanza Kilindi alipokumbukwa kutokana na babake na pia umaarufu wake kama mwindaji. Chifu wa mji akampatia nyumba akawa rafiki wa mwana wa chifu. _*Siku moja walipoenda pamoja kuwinda huyu kijana aliuawa na nguruwe mwitu na Mbegha aliona hawezi kurudi Kilindi akiogopa hasira ya chifu akaamua kuhama tena akiongozana na vijana 14 na mbwa zake.*_ (Hapa ndio palipoweka alamu mpya kwa wasambaa hadi leo, kifo cha mtoto wa chifu wa Kilindi)

Pamoja na kundi lake walizunguka wakapiga kambi huko Zirai kando ya Usambara. Wazee wa Bumbuli wakamkaribisha kuja kwao (Kama kawaida ya ukarimu wao) na chifu Mbogho wa Bumbuli alimpa binti yake kama mke akampandisha kuwa chifu pamoja naye.

Sifa zake zilisambaa kati ya Washambaa. Wakati ule Washambaa wa Vuga walikuwa na _vita dhidi ya Wapare_ wakaona wapate usaidizi wa Mbegha. Kiongozi wa Vuga akamwendea akamwomba kuhamia kwao na kuwa mwene wao (Mfalme). Mbegha aliomba kibali cha mkwe wake chifu Mbogho, akaongozana na watu wa Vuga pamoja na mke na shemeji yake.

Huku Vuga alikaribishwa kwa mapigo ya ngoma kubwa watu wengi wakaja kumkaribisha wakamjengea nyumba alipoingia. Mkewe alikuwa mjamzito tayari, akamwandalia kitanda kilichofunikwa kwa ngozi ya simba aliyowahi kuua safarini kuelekea Vuga. Mtoto aliyezaliwa juu ya ngozi ya simba akapewa jina la Simba akawa mrithi wake wa baadaye akipewa pia jina rasmi la Buge. Kutokana na jina hili watawala wa Vuga waliendelea kutumia cheo cha Simba Mwene. Baadaye huyu mwana wa kwanza alikuwa chifu wa Bumbuli kwa kibali cha baba.

Mbegha aliendelea kuoa mabinti kutoka koo za Washambaa mbalimbali na kuweka wanawe kutoka kio hizi kama watawala na wawakilishi wake juu ya vijiji vya mama zao. Kwa njia hii aliunganisha Usambara na koo za Washambaa na kuweka msingi kwa utawala wa kifalme katika Usambara uliosimamia sehemu kubwa ya Tanzania ya kaskazini kabla ya kuja kwa Wazungu.

Watawala wa nasaba yake waliomfuata Vuga waliendelea kuoa wake wengi na kuweka wana wao kama watawala wadogo mahali pa mama.

Mzee Mbegha alipoumwa alikaa pamoja na wazee watano pekee waliomtunza siku tatu hadi alipoaga dunia. Hao wazee hawakutangaza kifo chake (sababu za kiusalama) waliendelea kuandaa mazishi na ufuasi wake kimyakimya. Walituma ujumbe kwa Buge - Simba aje haraka babake ni mgonjwa. Mbegha alizikwa katika kaburi ndani ya ngozi ya ng'ombe dume mweusi pamoja na paka mweusi. Buga alipofika alitangazwa mara moja kuwa mwene mpya (mfalme mteule)

Habari za Mbegha zimehifadhiwa katika masimulizi ya watu na kuandikwa mara ya kwanza na Al-Ajemi mwishoni mwa karne ya 19. Wataalamu wa historia waliokusanya historia ya Usambara tangu wakati wa ukoloni walikamilisha historia ya Al Ajemi kwa habari za kieneo.

Hata Mbegha akikumbukwa kama mfalme wa kwanza wa Washambaa kuna wasiwasi kama yeye mwenyewe alitawala kwelikweli au kama alikuwa tu na athira athira kubwa kama mpatanishi na mshauri wa koo mbalimbali. Lakini kilichopoonekana, Mbagha wala hakuwa mtawala wa kwanza wa wasambaa, sema alikuwa wa kwanza kujulikana habari zake na wanahistoria, lakini upo ufalme wa kwanza kwa miakaa zaidi ya 500 ya kuishi kwao wasambaa katika nchi ya usambaa kabla ya ujio wa Mbegha!

Lakini kwa hakika alianzisha nasaba ya Kilindi iliyoungansha na kutawala Usambara pamoja na maeneo jirani hadi ukoloni. Wengine wanaona mtawala kamili wa kwanza alikuwa Buga aliyemwua babu yake Mbogho na hivyo kushika utawala kamili juu ya Vuga na Bumbuli. Mwana wa Buge aliyeitwa Kinyashi alianza kupanusha himaya yake kwa njia ya vita, na mtoto wake _Kimweri ye Nyumbai_ alisimamia kilele cha uwezo wa nasaba hii mnamo 1850 akitawala Usambara, Usegeju, Digo na Bondei pamoja na sehemu za Useguha, Upare na tambarare za Maasai. Hata maliwali wa Pangani na Tanga waliokuwa chini ya Sultani wa Zanzibar walilipa kodi za kuthibitishwa vyeo vyao kwa mtawala wa Vuga.

Baadaye biashara iliyopita bondeni iliongeza utajiri wa machifu wa Mazinde waliofaulu kuvunja kipaumbele cha Vuga baada ya 1860.

Koo hariri

Wasambaa wamegawanyika katika koo mbalimbali ndani ya jamii zao ambazo ndizo utambulisho wao. Ukoo ni jambo muhimu sana katika maeneo ya Usambaa kwani wanajamii wa Kisambaa wanatambuana kwa majina ya ukoo.

Alama maarufu ya koo za Kisambaa ni majina yanayoanza na "She" kama Shelukindo, Shemhina, Shekusa, Shekiango, Shekimwei, Sheiza, Shembilu, Shekinyashi, Sheshe n.k. Koo nyingi za Kisambaa zinajulikana kwa majina yao kuanza hivyo.

Tanbihi hariri

  Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Washambaa kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.