Washirika Tanzania Stars
Washirika Tanzania Stars (al-maarufu Watu-Njatanjata) ilikuwa bendi ya muziki wa dansi kutoka jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Washirika Tanzania Stars | |
---|---|
Pia anajulikana kama | Watu-Njatanjata |
Asili yake | Dar es Salaam, Tanzania |
Aina ya muziki | Muziki wa dansi |
Historia ya bendi
haririBendi ya Washirika Tanzania Stars ilianzishwa rasmi Agosti 1989 ikiwa inarithi jina la bendi ya Tanzania Stars ambayo ilikuwa chini ya Vyama vya Msingi vya Ushirika ikiwa inafanya maonyesho yake kwenye Hoteli ya Maggot pale Mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam. Bendi hiyo ilibadili jina mara tu ilipoanza kumilikiwa na Muungano wa Vyama vya Ushirika Tanzania (CUT). Tanzania Stars iliyokuwa imeongezewa nguvu kwa kuwachukua wanamuziki kadhaa kutoka Vijana Jazz Band kama Adam Bakari, Eddy Sheggy, ‘Komandoo’ Hamza Kalala na fundi mitambo Salum Pongwe, ilishindwa kuvilipia vyombo vilivyokuwa vimeletwa na Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata) na hivyo kuamua kuomba msaada kutoka CUT.
Vifaa hivyo viliagizwa na Chamudata ambapo vilikuwa miongoni mwa seti nne. Seti nyingine zilichukuliwa na Mwenge Jazz Band ‘Paselepa’, Polisi Jazz Band ‘Vanga Vanga’ na Kurugenzi Jazz. Huo ulikuwa ni wakati wa ‘uhai’ wa Chamudata chini ya uenyekiti wa Kassim Said Mapili, ambapo chama kilikuwa na nguvu kweli kweli tofauti na sasa ambapo kimedorora. CUT ilitoa fedha hizo kwa makubaliano kwamba zitakuwa zikilipwa kidogo kidogo, lakini bendi hiyo haikuweza kutimiza ahadi hiyo kutokana na mapato yake kuwa hafifu. Ndipo Hamza Kalala akamwendea Mwenyekiti wa CUT, Phillip Ndaki na Katibu wake, David Holela, na kuwapa wazo la kuanzisha bendi, ambalo lilikubaliwa. Wanamuziki waliokuwa wakiunda Washirika Tanzania Stars ni Adam Bakari, Hamza Kalala, Eddy Sheggy na fundi mitambo Salum Pongwe (wote kutoka Vijana Jazz), Christian Sheggy, Madaraka Morris, Noordin Athumani, Hassan Athumani, Kejeli Mfaume, Abdul Salvador ‘Father Kidevu’ na Juma Shaaban.
Wanamuziki wengine waliopitia hapo ni Mhina Panduka 'Toto Tundu' na Emma Mkelo 'Lady Champion'. Kibao cha kwanza walichoibuka ni ‘Penzi la Ulaghai’ kilichoimbwa na Eddy Sheggy katika sauti ya kwanza na Adam Bakari katika sauti ya tatu. Gitaa la solo lilikuwa likicharazwa na Hamza Kalala, solo namba mbili alipiga Robert Mabrish, Noordin Athumani alipiga rhythm, gitaa la bass lilipigwa na Juma Shaaban, Hassan Athumani (tumba), Kejeli Mfaume (drums) na kinanda kilikuwa kinapapaswa na Abdul Salvador. Onyesho la kwanza la bendi lilifanyika Novemba 1989 kwenye ukumbi wa Dodoma Hotel kwa ajili ya kuwaburudisha Wabunge na liliingiza jumla ya Shs. 17,000, yakiwa ni mapato makubwa zaidi kuingizwa na bendi yoyote ya dansi nchini kwa wakati huo.
Wakati huohuo Eddy Sheggy naye aliibuka na kibao chake cha ‘Kisa’, ambacho nacho kilikuwa matata sana. Baadaye Hamza Kalala akatunga kibao cha Yaliyopita si Ndwele' au 'Nimekusamehe Lakini Sitokusahau’, kilichopigwa katika miondoko ya reggae ndani ya dansi. Kibao hicho kisemacho ‘, Komandoo Hamza Kalala, ambaye inaelezwa kwamba alitunga makusudi kueleza msimamo wake kuwa alikuwa amemsamehe ‘rafiki yake’ Hemedi Maneti Ulaya, kiongozi wa Vijana Jazz enzi hizo. Inaelezwa kwamba, Komando Kalala aliondoka Vijana Jazz baada ya Maneti kumpata Bwa’mdogo Shabani Yohana ‘Wanted’ kutoka bendi ya Tancut Almasi Orchestra ya Iringa. Hiyo ilikuja baada ya Kalala kupata ajali ya gari na kuruhusiwa kupumzika kwa muda wa miezi mitatu, ambapo Maneti alilazimika kumtafuta mpiga solo mwingine.
Wanted alikuwa mtundu wa gitaa, halafu ikatokea akawa anamudu kupiga nyimbo zote ambazo Kalala alikuwa anazipiga. Mara baada ya kupata nafuu na kurejea, inasemekana Maneti alimkataza Kalala asipande jukwaani na muda mwingi akautumia kama ‘mtazamaji’ tu. Komandoo akaamua kuondoka na kujiunga na Tanzania Stars hadi kuanzisha Washirika. Mara nyingi kisa hiki Komando Kalala huwa hapendi kukizungumzia… “Yaliyopita yamepita…” ndivyo husema daima. Washirika Tanzania Stars iliendelea kujipatia umaarufu mkubwa hasa baada ya kuibuka na vibao ningine maridadi kama ‘Julie’ ukiwa utunzi wake Madaraka Morris, vibao vya ‘Watoto Wamekuja Juu’ na ‘Mjumbe Nimekuja’ ukiwa ni utunzi wa Sauti ya Zege. Wakati huo ilikuwa pia imewapata wanamuziki wengine mahiri kama Mhina Panduka 'Toto Tundu', Emma Mkelo 'Lady Champion', na wengineo wengi.
Awamu ya Pili "Njata One" chini ya CUT
haririIkiwa chini ya CUT, bendi ilikuwa ikishiriki kwenye mambo mengi, yakiwemo kuhamasisha shughuli za ushirika, kwenye sherehe mbalimbali kama za Wakulima, sherehe za Chama cha Mapinduzi enzi hizo za mfumo wa serikali ya chama kimoja, na shughuli mbalimbali za serikali. Kutokana na bendi hiyo kuwa kipenzi cha wengi na kukusanya mashabiki lukuki kwenye maonyesho yao, viongozi wa CUT wakaifanya kitegauchumi kwa kukusanya mapato mengi. Hata hivyo, badala ya kumpa ng’ombe majani na maji ndipo umkamue, wao walikuwa ‘wanaikamua’ bendi bila kuihudumia. Walikusanya mapato yote na kusahau kuwapa wanamuziki haki zao, ambao ndio wazalishaji. Hali hiyo ikawalazimu baadhi ya wanamuziki kuondoka ambapo Eddy Sheggy na mdogo wake Christian walikwenda Bima Lee Orchestra, Hamza Kalala akaanzisha bendi yake ya HK & Bantu Group na Abdul Salvador akaanzisha bendi yake ya The Hisia Sounds.
Mgawanyiko huo ulitokea mwaka 1991. Awamu hii ya pili ya wanamuziki waliosalia ikaifanya bendi ibadilishe hata mtindo wake, ambapo badala ya Watunjatanjata, ambao maana yake ni ‘Wakulima Tuondoe Njaa Tanzania’, sasa ikaibuka na mtindo wa ‘Njata One’. Pamoja na kubakia na wanamuziki wengi, bendi hiyo ikaongezewa nguvu na wanamuziki kadhaa wakiwemo Mohammed Shaweji kutoka Vijana Jazz na Toffi Mvambe kutoka Super Matimila. Vibao kadhaa vikatungwa ambapo Adam Bakari akaibuka na vibao viwili – ‘Penzi la Kusuasua’ na ‘Utamaduni’, ambavyo kwa hakika vilionekana kama ndiyo mwisho wa bendi hiyo.
Awamu ya Tatu
haririMambo yakaenda yakiongezeka! Lakini si kwa mema. Kizaazaa kwenye bendi hiyo kikatokea mwaka 1993 wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, ambao mara nyingi huwa ni likizo kwa wasanii wote kutokana na watu wengi kufunga, hususan waumini wa Kiislamu, hivyo burudani zote hupungua. Wanamuziki wa bendi hiyo walipoanza kudai ‘mafao’ yao ili waende likizo, viongozi wa Ushirika wakaweka ngumu na kutaka waendelee kutumbuiza! Wanamuziki walijitahidi kuuelewesha uongozi kwamba kipindi hicho mapato huwa haba kutokana na wapenzi wengi wa dansi kuwa katika funga ya Ramadhan. Lakini viongozi hao hawakusikia la Muadhini wala Mnadi Swala! Wakwaambia wanamuziki, kwamba mlango uko wazi, anayetaka kuondoka aondoke, anayetaka kubaki, apige kazi kama kawaida. Waliobaki wakabaki, walioondoka wakaondoka. Mwaka wa 1994, Adam Bakari, mwanamuziki huyo alisema kwamba aliamua kumwendea rafiki yake aitwaye Mwakibinga na kumshawishi waanzishe bendi, naye bila hiyana akaridhia na kutafuta vyombo Sinza kwa Mzee Mbaga, ambavyo walivinunua kwa Shs. 2 milioni tu. Kama masikhara vile, wakaanzisha bendi ya MCA International mwaka 1994, ambayo iliundwa na yeye Sauti ya Zege, Said Makelele (tarumbeta), Abdallah Kimeza (sax), Noordin Athumani (rhythm), George Kessy Omojo (bass), na Kassim Rashid Kizunga (solo), ambaye alikuwa amechukua nafasi ya Kalala kule Washirika katika awamu ya pili. Bendi ya MCA International ikaweka kambi yake Bagamoyo. Washirika Tanzania Stars ikabaki ikisuasua tu pamoja na jukumu la kuiendeleza kukabidhiwa Zahir Ally Zorro na Hassan Show. Zorro akaibuka na kibao cha ‘Mikufu ya Dhahabu’, lakini juhudi zake hazikuzaa matunda na hatimaye bendi hiyo ikatoweka kwenye anga la muziki wa dansi. Baada ya serikali kuvunja Vyama vya Ushirika na kuamuru kila mkoa ujitegemee, CUT ikaamua kuja na mtindo wa kuiunda au kuikusanya bendi hiyo kila mwaka inapokaribia sikukuu ya Wakulima (Nane Nane), ambao walikuwa wakiwashawishi baadhi ya wanamuziki waliopata kuimbia bendi hiyo na kwenda kwenye sherehe hizo. Hata hivyo, juhudi hizo zilikoma mwaka mwaka 1996 na mpaka sasa hakuna anayeikumbuka. Imekufa kama zilivyokufa Urafiki Jazz, UDA Jazz, Bima Lee Orchestra, na nyinginezo zilizokuwa zikimilikiwa na mashirika ya umma.
Tazama pia
haririViungo vya Nje
hariri- Washirika Tanzania Stars Ilihifadhiwa 18 Juni 2017 kwenye Wayback Machine. katika Wavuti ya Saluti5