Kassim Said Mapili (1937 - 2016) alikuwa mwanamuziki maarufu wa muziki wa dansi kutoka nchini Tanzania.

Kassim Mapili
Kassim Mapili enzi ya uhai wake
Kassim Mapili enzi ya uhai wake
Maelezo ya awali
Jina la kuzaliwa Kassim Mapili
Amezaliwa 1937
Nachingwea, Lindi, Tanzania
Asili yake Lindi, Tanzania
Aina ya muziki Muziki wa dansi
Miaka ya kazi 1950-2016

Historia

hariri

Maisha na muziki

hariri
 
Kassim Mapili ya enzi ujana wake akiwa anatumbuiza.

Mzee Mapili alizaliwa katika kijiji cha Lipuyu, Tarafa ya Lionya, Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi mwaka 1937. Hivyo mauti ilimkuta Mzee Mapili akiwa na umri wa miaka 79. Alipata elimu ya msingi huko kwao Lipuyu, sambamba na kupata elimu ya dini na mwenyewe aliwahi kusema alianza kupata mapenzi ya kuimba wakati alipokuwa Madrasa akighani Kaswida. Mwaka 1958 alijiunga na White Jazz Band iliyokuwa na masikani yake huko Lindi.

Mwaka mmoja baadaye akahamia Mtwara na kujiunga na Mtwara Jazz Band, lakini mwaka 1962 akajiunga na Honolulu Jazz Band ambayo nayo ilikuwa hapo hapo Mtwara. Mwaka 1963, Mzee Mapili akachukuliwa na TANU Youth League ya mjini Lindi, na kujiunga na bendi ya Jamhuri Jazz Band ya hapo Lindi. Mwaka 1964 Mzee Mapili akachaguliwa kuanzisha bendi ya TANU Youth League ya Tunduru. Mwaka mmoja baadaye alihamia Kilwa Masoko na kujiunga na Lucky Star Jazz Band ya mji huo.

Baada ya hapo ndipo Kassim Mapili akatua katika jiji la Dar es Salaam na kujiunga na Kilwa Jazz Band iliyokuwa ikiongozwa na Ahmed Kipande. Kama ilivyokuwa sera ya wakati ule ya kuanzisha vikundi vya sanaa katika sehemu za kazi, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nalo likaanzisha bendi na Mzee Mapili alikuwa mmoja ya waanzilishi wa bendi ya JKT Kimbunga Stereo mwaka 1965. Polisi nayo pia ikaanzisha bendi na Mzee Mapili akajiunga na Police Jazz Band, 15 Desemba 1965. Mzee Mapili ndiye aliyekuwa mwalimu wa bendi ya kwanza ya wanawake nchini Women Jazz Band iliyoanzishwa mwishoni mwa mwaka 1965.

Mapili na uanzishwaji wa Chama cha Mziki wa Dansi Tanzania

hariri

Mwaka 1982 baada ya semina ya wanamziki iliyofanyika Bagamoyo, Mzee Mapili alikuwa mmoja wapo wa wanamziki walioanzisha Chama Cha Mziki wa dansi Tanzania, na akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho. Akiwa Mwenyekiti wa chama hicho mwaka 1986, aliweza kukusanya kundi la wanamziki 57 ambao walitengeneza kund lililoitwa Tanzania All Stars. Kundi hili lilirekodi mziki ambao mpaka leo umekuwa katika kipimo cha juu ambacho hakijafikiwa na wanamziki wa sasa.

Wakati wa uongozi wa Mzee mapili kwa kushirikiana na Umoja wa Vijana wa CCM, Radio Tanzania, BASATA na CHAMDATA waliweza kufanya shindano la bendi ambalo aina yake haijawahi kurudiwa tena, shindano hili lililoitwa Top Ten Show lilishirikisha bendi kutoka karibu kila wilaya nchini Tanzania. Uongozi huu aliendelea mpaka mwaka 1990.

Mapili na Shikamoo Jazz Band, Super Matimila, Gold All Stars na Volcano Stars

hariri

Mwaka 1993 alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Shikamoo Jazz Band na katika bendi hii alitunga wimbo wa Eva uliokuwemo katika albamu ya kwanza ya bendi hii. Alipoacha bendi hii Mzee mapili alipitia Super Matimila, Gold All Stars, na hata kujiunga na binti wa Mbaraka Mwinshehe katika bendi yake ya Volcano Stars, na kipindi cha karibuni alikuwa akishirikiana na Mrisho Mpoto na wasanii mbalimbali katika muziki. Mzee Mapili ameacha watoto watatu. Hakika Mzee Mapili alikuwa mtu wa watu.

Umauti na usia wake juu ya mazishi yake

hariri

Enzi za uhai wake alipata kumwachia usia mwanamuziki mwenzake maarufu Mzee John Kitime juu ya maziko yake. Kitime alieleza ya kwamba:

Miezi michache iliyopita Mzee Kassim Mapili alinambia huku anacheka kuwa siku akifariki, maiti yake iagwe katika uwanja wa Mnazi Mmoja na kisha jeneza lake libebwe na wapenzi wake bila kutumia gari hadi Kisutu ambapo ndipo azikwe.

Haikuwezekana kufanya shughuli ya kwanza ya kuaga lakini hakika Mzee Mapili amezikwa makaburi ya Kisutu kama alivyowahi kusema mara kadhaa. Jambo lililofanya Mzee Mapili asiagwe ni kutokana na mazingira ya kifo chake. Siku ya Jumanne usiku alipotoka kuangalia mechi ya Arsenal na Barcelona aliingia chumbani kwake na ni kwa wakati huo alipofikwa na mauti.

Bahati mbaya baada ya kufikwa na mauti ilifikia mpaka Alhamisi jioni, ndipo maiti yake ilipogundulika na taratibu za mazishi zilipoanza kufanyika. Bahati mbaya tayari mwili ulishanza kuharibika hivyo haikuwezekana kutimiza nia ya marehemu ya kuagwa Mnazi Mmoja.

Tazama pia

hariri
  Makala hii kuhusu mwanamuziki/wanamuziki fulani wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kassim Mapili kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.