Kuni

Kuni ni ubao unaotumiwa kama fueli ikichomwa motoni ya kupikia au pia ya kupashia nyumba moto. Kwa kawaida kuni inakusanywa penye miti kwa kutafuta sehemu ziliokauka au kwa kukata miti inayopasuliwa kuwa vipande vya ukubwa unaofaa. Kwa kutumia teknolojia kuna pia kuni inayopitishwa kwenye mashine na kupewa umbo maalumu unaofaa majiko ya kisasa.

Watu wengi duniani kwenye nchi za joto hutumia kuni kwa kupikia chakula na kuchemsha maji ya kuoga au kuosha nguo. Tangu karne ya 19 na hasa 20 watu wengi wamehamia kutumia fueli nyingine kama makaa mawe, gesi na madawa yanayotengenezwa kutokana na mafuta ya petroli au pia umeme.

Lakini hata katika nchi baridi zilizoendelea kuna watu wengi kidogo katika mazingira ya misitu wanaopendelea kuendelea kutumia kuni kama mababu zao. Wengine wanafanya hivyo kwa sababu wana maeneo ya miti au msitu hivyo kuni kwao ni bure; wengine wamefuata majadiliano juu ya ekolojia na wanaona ni bora kimaadili kutumia fueli ya nishati mbadala kuliko fueli ya kisukuku‎; wengine wameona ya kwamba ubao ni fueli nafuu kama wanakaa karibu na misitu na wana uwezo wa kununua majiko ya kisasa kwa nyumba yao. ►Soma zaidi