Picha ya Xerxes kwenye mwamba wa nguzo huko Persepolis

Xerxes I alikuwa Shah (mfalme) wa Uajemi ya Kale kuanzia 485 KK hadi 465 KK. Alikuwa mtawala wa 10 katika nasaba ya Waakhameni. Xerxes alikuwa mwana wa Dario I na Atossa, binti ya Koreshi Mkuu . Baada ya kifo cha Dario, Xerxes akawa Shah wa Uajemi . Alichukua cheo cha Shahanshah ( Mfalme wa Wafalme ).

Xerxes (Ξέρξης) ni umbo la Kigiriki la jina lake. Kwa Kiajemi ya Kale lilikuwa Xšaya-ṛšā. Mataifa mengine katika ufalme wake yalitafsiri jina hili kwa namna tofauti Inaaminiwa umbo la Kibabeli Akšiwaršu lilipokelewa katika Kiebrania kama Ahasverus[1].

Vita ya Ugiriki

hariri

Xerxes alikuwa mfalme wakati baba yake Dareio alikuwa akiandaa vita dhidi ya Ugiriki baada ya kupigwa na Waathens katika Mapigano ya Marathon. Alikusanya jeshi kubwa kutoka pande zote za milki yake akavuka mlangobahari wa Dardaneli kwa kujenga daraja. Katika Mapigano ya Thermopylae, Xerxes alishinda kikosi cha jeshi la Sparta na kuteka sehemu za Ugiriki . Baada ya ushindi huko Thermopylae, Xerxes alivamia pia mji wa Athens akaichoma. Lakini watu wa Athens waliwahi kujiokoa kwenye kisiwa cha Salamia. Manowari za Wagiriki zilishambulia Waajemi katika mapigano ya baharini ya Salamis mnamo mwaka 480 KK zikashinda. Xerxes aliamua kurudi upande wa Asia akiacha jeshi katika Ugiriki lakini pia jeshi hilo lilipigwa na wagiriki katika mapigano ya Plataia mwaka 479 KK[2].

Utawala

hariri

Baada ya vita ya Ugiriki, Xerxes alirudi Uajemi akashughulika kukamilisha miradi ya ujenzi iliyoanzishwa na baba yake Dareio I hasa katika miji mikuu ya Shushani na Persepolis. Mapambo mengi yanayoonekana huko Persepolis hadi leo yaliumbwa wakati wa Xerxes. Huko Shuhani alitengeneza ikulu kubwa.

Alitengeneza pia barabara ya kifalme kutoka Shushani hadi Sardis katika Asia Ndogo.

Xerxes na Ahasuero

hariri

Katika Kitabu cha Esta cha Biblia kuna simulizi ya binti Myahudi Esta anayeolewa na mfalme wa Uajemi anayeitwa Ahasuero katika tafsiri ya Kiswahili (Kiebrania אֲחַשְׁוֵרֹ֑ושׁ Ahasverus) . Kitabu hiki kinasimulia habari zilizotokea katika mji mkuu Shushani. Ahasuero ni umbo tofauti la "Xerxes", maana wafalme wote waliotawala milki ya mataifa mengi walijulikana kwa majina tofautitofauti.

Mwaka 465 KK mfalme Xerxes pamoja na mwanawe Dario waliuawa na mkuu wa walinzi wake, Artabanus.

Mwana wake wa pili Artaxerxes alimfuata katika ufalme.

Marejeo

hariri
  1. https://iranicaonline.org/articles/ahasureus W. S. McCullough, “AHASUREUS,” Encyclopædia Iranica, I/6, pp. 634-635; online hapa http://www.iranicaonline.org/articles/ahasureus (accessed on 16 March 2014).
  2.   "Xerxes". Encyclopædia Britannica (11th ed.). 1911.

Vyanzo vya kale

hariri

Viungo vya Nje

hariri
 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu: