Alhamisi
Alhamisi ni siku ya tano katika juma (wiki) ya siku saba yenye asili ya kiyahudi-kikristo. Iko kati ya siku za Jumatano na Ijumaa. Katika hesabu ya kimataifa ya ISO 8601 ni siku ya nne.
Wikendi katika nchi za Kiislamu
haririNchi kadhaa za Waislamu huanza mapumziko ya wikendi kwenye Alhamisi kama Ijumaa ni siku ya mapumziko. Hii si nchi zote za Kiislamu. Kwa mfano Misri wafanyakazi huanza wikendi Alhamisi na kuendelea Ijumaa; Uturuki inatumia wikendi ya magharibi yaani Jumamosi-Jumapili.
Siku ya tano au siku ya nne?
haririKatika muundo wa juma wa kibiblia Alhamisi ni siku ya tano. Kanuni ya ISO 8601 ilibadilisha hesabu ya juma kufuatana na kawaida ya mapumziko ya "wikendi" kwenye siku za Jumamosi/Jumapili. Katika muundo huu Jumatatu hutazamiwa kama siku ya kwanza katika juma ya kazi hivyo inahesabiwa kama siku namba "1" ya wiki katika kalenda hivyo Alhamisi ni namba 4. Jumuiya za kidini zinasisitiza hesabu ya kibiblia na kawaida katika tamaduni nyingi inaendelea hesabu ya kale.
Jina la siku kwa Kiswahili na kwa lugha mbalimbali
haririKatika lugha ya Kiswahili jina la siku lina namba "5" ndani yake lakini haieleweki kirahisi kwa sababu Alhamisi ina asili ya lugha ya Kiarabu. خميس (khamis) ni namba tano tu. Kiswahili chenyewe chatumia namba hii katika jina la siku ya Jumatano inayotangulia Alhamisi. Pamoja na Ijumaa ni siku ya pekee yenye jina la Kiarabu katika lugha ya Kiswahili.
Majina ya siku zingine yameanzishwa upya katika Kiswahili kuanzia siku ya sala ya pamoja ya Waislamu kwenye Ijumaa kuzitaja kama Juma-mosi, Juma-pili n.k.
Tabia hii katika Kiswahili ni ya pekee hasa kwa sababu Kiarabu ambacho ni lugha ya Korani takatifu na lugha ya kimataifa ya Waislamu kinafuata hesabu ya Kiyahudi na kuita siku hiyo kwa namba "tano". Lugha nyingi za nchi za Kiislamu zafuata kawaida ya Kiarabu na kuiita "siku ya tano", kwa mfano Kiindonesia (Kamis - ya tano) au Kiajemi (Farsi) (پنجشنبه - panch shanbe - siku ya tano).
Katika lugha nyingi za Ulaya jina la siku hutunza kumbukumbu ya miungu iliyoabudiwa zamani za dini za Kiroma au Kigermanik kama vile Kifaransa "Jeudi" (siku ya Jovi au Jupiter) au Kiingereza "Thursday" (siku ya Thor).
Siku za juma (wiki) |
---|
Jumapili - Jumatatu - Jumanne - Jumatano - Alhamisi - Ijumaa - Jumamosi |