Jumapili

moja ya siku saba za wiki

Jumapili ni siku ya kwanza katika juma (wiki) ya siku saba yenye asili ya Kiyahudi-Kikristo. Iko kati ya siku za Jumamosi na Jumatatu.

Kwa Wakristo walio wengi ni siku ya sala za pamoja kanisani.

Kiswahili, Kiarabu na utamaduni wa Kiislamu

hariri

Katika lugha ya Kiswahili jina la siku lina namba "2" ndani yake. Hili ni dokezo la asili ya Kiswahili katika utamaduni ya Kiislamu pasipo athira ya Uyahudi unaoanza hesabu baada ya sikukuu ya Kiislamu ya Ijumaa, siku ya sala ya pamoja: Jumamosi kama siku ya kwanza baada ya Ijumaa, Jumapili kama siku ya pili, Jumatatu kama siku ya tatu n.k.

Tabia hii katika Kiswahili ni ya pekee, hasa kwa sababu Kiarabu, ambacho ni lugha ya Korani takatifu na lugha ya kimataifa ya Waislamu, kinafuata hesabu ya Kiyahudi na kuiita siku "al-ahad" yaani "ya kwanza".

Siku ya jua, siku ya Bwana, siku ya ufufuo

hariri

Katika lugha za Kigermanik siku hii ina jina la "jua". Lugha hizo, kama Kiingereza na Kijerumani, zinaendeleza urithi wa Roma ya Kale na zaidi wa Babiloni ambako kila siku ya wiki ilikuwa chini ya mungu fulani aliyeonekana kama nyota au sayari.

Kundi lingine la lugha linatumia msamiati "siku ya Bwana" yaani "Bwana Yesu Kristo". Ni hasa lugha za Kirumi kama Kifaransa (dimanche), Kiitalia (domenica), Kihispania (domingo) na kadhalika.

Lugha ya Kirusi inaita siku hii "voskresenye" yaani siku ya ufufuko.

Uzoefu wa Kikristo

hariri

Wakristo wa madhehebu mengi (isipokuwa Wasabato) wanatazama Jumapili kama siku ya mapumziko iliyochukua nafasi ya Sabato iliyotajwa kwenye Amri Kumi za Agano la Kale.

Sababu ya badiliko hilo lilitokea tangu karne ya 1 ni umuhimu wa ufufuko wa Yesu uliotokea kwenye siku ya kwanza ya juma kufuatana na habari za Agano Jipya.

Kadiri Wakristo wa mwanzo walivyozidi kushindana na Wayahudi wasiomuamini Yesu, walizidi kuzingatia Jumapili kuliko Jumamosi, hasa baada ya kufukuzwa kutoka masinagogi katika miaka ya 80 BK.

Jumapili katika lugha mbalimbali

hariri
Majina ya Jumapili katika tamaduni mbalimbali
Lugha Jina/Matamshi Maana Maelezo
Kiebrania יום ראשון
jom rishon
siku ya mwanzo
Kigiriki Κυριακή
kiriaki
(siku ya) Bwana
Kiarabu أحد
al-ahad
(siku) ya kwanza
Kiajemi :یکشنبه
yek-schanbe
(siku ya) kwanza
Kireno Domingo
(siku ya) Bwana
Kilatini dies solis Siku ya jua
Kiitalia domenica (siku ya) Bwana
Kihispania Domingo (siku ya) Bwana
Kifaransa dimanche (siku ya) Bwana
Kijerumani Sonntag siku ya jua
Kiingereza Sunday siku ya jua
Siku za juma (wiki)
Jumapili - Jumatatu - Jumanne - Jumatano - Alhamisi - Ijumaa - Jumamosi