Apostolicam Actuositatem
Mtaguso wa pili wa Vatikano uliwaongelea walei katika hati mbalimbali ukionyesha nafasi yao katika maisha ya Kanisa (liturujia, upashanaji habari, ekumeni n.k.).
Hata hivyo uliona umuhimu wa kuwaandikia hati maalumu iwaongoze hasa katika utume ili watimize wajibu wao kwa wokovu wa ulimwengu.
Karibu waamini wote wa Yesu ni walei, tena ndio wanaoshirikiana zaidi na watu wowote katika yote: hivyo wasipotoa mchango wao, utume wa Kanisa utakuwa mlemavu, hasa siku hizi.
Si kwamba wanapaswa kufanya utume kutokana na uhaba wa mapadri na watawa, bali kutokana na wito walioupata katika ubatizo na kipaimara.
Hati hiyo, ilitolewa tarehe 18 Novemba 1965 kwa kura 2340 dhidi ya 2 tu, inaanza na maneno "Apostolicam Actuositatem" (katika Kilatini yana maana ya "Utendaji wa Kitume").
Sura ya kwanza
haririSura ya kwanza inaeleza wito huo katika Kanisa na roho itakayowawezesha kuutimiza kitakatifu, kwa sababu wito wao ni tofauti na ule wa mapadri na watawa, hivyo maisha ya Kiroho pia yanapaswa kuwa tofauti.
Sura ya pili
haririSura ya pili inaeleza malengo makuu ya utume wa walei, kwamba sio tu kueneza ujumbe wa Yesu Kristo, bali pia kuratibu malimwengu yafuate matakwa ya Mungu, kutimiza matendo ya huruma na kushuhudia upendo.
Sura ya tatu
haririSura ya tatu inafafanua zaidi nafasi mbalimbali za utume wao: jumuia za Kikanisa, familia, vijana, jamii, taratibu za kitaifa na za kimataifa.
Sura ya nne
haririSura ya nne inaeleza namna za kutimiza utume, kuanzia ule wa mtu mmojammoja hadi ule wa pamoja katika vyama mbalimbali ambavyo walei wana haki ya kujiundia, na katika miundo maalumu iliyoanzishwa na wachungaji wao.
Sura ya tano
haririSura ya tano inaeleza utaratibu wa kufuatwa katika utume ili ufanyike si kwa wivu na mashindano bali kwa upendo na ushirikiano, kwanza na maaskofu, mapadri na wahudumu wengine mpaka na Wakristo wa madhehebu tofauti na wasio Wakristo. Kwa ajili hiyo katika ngazi zote iwepo halmashauri.
Sura ya sita
haririHatimaye sura ya sita inasisitiza haja ya [[malezi bora kuanzia utoto na ujana na katika nyanja zote zinazohusu utu na Ukristo. Halafu yawepo malezi maalumu kwa ajili ya shughuli maalumu.