Utume
Utume unatokana na fukuto la Kiroho zaidi ndani ya mtu lenye kuigusa nafsi yake, kama kwa kusikia sauti rohoni inayomfanya aitikie kwa kutumika sawasawa na kusudio la Neno la Muumbaji.
Katika Ukristo
haririKatika Ukristo ni wito wa kumtaka mtu kutumikia ufalme wa Mungu kama Yesu Kristo alivyofanya wakati wa uhai wake akiwa na wanafunzi wake (Mitume wa Yesu). Aliwachagua na kuwatuma wawiliwawili ama 12 na mara nyingine 70 au 72. Waliitika sauti wakaenda huko na huko na waliporejea walitoa taarifa ya kazi waliyoifanya: "...hata pepo wametutii kwa jina lako (Yesu)."
Chemchemi ya juu ya utume
haririKatika hotuba ya Mtume Petro siku ya Pentekoste, na katika barua za Mtume Paulo, tunakuta Neno la moto likiongozwa na uvuvio wa Mungu. Mababu wa Kanisa ili wawaokoe watu waliwalisha matunda ya sala waliyomiminiwa. Kuzama kwa upendo katika mafumbo ni bora kuliko vitendo vya toba na kuliko masomo: ndiyo roho ya utume. Mtume yeyote awe anashirikisha mang’amuzi yake ya sala ya kumiminiwa ili kuwatakasa na kuwaokoa watu, kadiri ya maneno ya Thoma wa Akwino: “Kuzama katika mafumbo na kuwashirikisha wengine yaliyotazamwa hivyo”.
Ili maisha hayo yadumu kuwa na umoja, sala ya kumiminiwa na utendaji haviwezi kuwemo katika msingi wa usawa; ni lazima kimoja kiwe chini ya kingine, la sivyo vitadhuriana na hatimaye itabidi kuchagua kimojawapo tu. Wengi, wajue wasijue, wanapotosha fundisho la mapokeo, wakisema maisha ya kitume lengo lake kuu ni utendaji wa kitume, ila yanalenga pia sala kama chombo cha lazima kwa ajili ya utendaji. Lakini je, kweli mitume na wamisionari watakatifu, k.mf. Fransisko Saveri, waliona kuzama kwa upendo katika mafumbo ya imani ni chombo tu kinacholenga utendaji? Je, kweli Yohane Maria Vianney alitazama hivyo sala na misa? Kudhani hivyo ni kupunguza umuhimu wa muungano na Mungu, ulio chemchemi ya utume wowote. Kwa mtazamo huo, ambao pengine hautokezwi wazi, ungefikiwa uzushi wa kupindua mpangilio wa upendo kwa kusema ule kwa jirani ni wa juu kuliko ule kwa Mungu.
Kuzama katika mafumbo yake na hivyo kuungana naye hakuwezi kuwa njia ya kulenga utendaji, kwa sababu ni jambo la juu zaidi. Duniani hakuna lolote la juu kuliko kuungana na Mungu kwa sala ya kumiminiwa na upendo: “Kwa umbile lake maisha ya sala hasa yanatangulia yale ya utendaji, kwa sababu yanalenga mambo makuu na bora, halafu yanasukuma na kuongoza katika maisha ya utendaji” (Thoma wa Akwino). Utume hauna thamani kubwa usipotokana na chemchemi hiyo kama sababu ya juu. Tena wenyewe ni njia inayolenga muungano na Mungu tunaotaka kuwafikishia watu. Kwa hiyo tunapaswa kulenga hasa kuzama katika mafumbo ambako kunazaa utume.
Yesu Kristo hakuridhika na maisha ya sala tu, bali alichagua yale ambayo yanatokana na utajiri wa sala ya kumiminiwa na yanashuka kuwashirikisha watu kwa njia ya mahubiri. Uhusiano wa kuzama katika mafumbo na kutenda unafanana na ule wa umwilisho na ukombozi. Umwilisho wa Neno hauhusiani na ukombozi wetu kama njia ya chini inavyolenga shabaha ya juu, bali kama sababu ya juu inayoleta tokeo la chini. Tangu milele Mungu alipanga umwilisho si kwa kulenga ukombozi bali kwamba uzae ukombozi. Vivyo hivyo alipanga maisha ya kitume yawe na sala ya kumiminiwa na muungano na Mungu si kwa kulenga utendaji, bali kwamba vizae matunda katika utume.
Ni lazima utume utokane na kuzama katika mafumbo ya wokovu ili mahubiri na uongozi wa kiroho viwe viangavu, hai, sahili, vyenye hakika ya dhati ambayo inachoma na kuvutia mioyo. “Anayewaletea wengine neno la Mungu anatakiwa kuwaelimisha, kuivuta mioyo yao kwa Mungu na kuchochea utashi wao watekeleze sheria yake” (Thoma wa Akwino). Inatakiwa iwe hivyo ili mahubiri yasishirikishe herufi tu, bali roho ya Neno la Mungu, ya mafumbo yapitayo maumbile, ya amri na ya mashauri. Si suala la miguso ya juujuu, bali la uvuvio wa ukweli wa Mungu unaotokana na imani kubwa na upendo motomoto kwa Mungu na kwa watu.
Ili tuelewe mahubiri ya Injili yanavyotakiwa kuwa, tukumbuke kwamba sheria mpya si Maandiko kwanza, bali sheria iliyomiminwa rohoni, yaani neema ya Roho Mtakatifu. Ili tuishi kwa neema hiyo ilibidi tuelimishwe kwa maneno ambayo yalitamkwa na kuandikwa kuhusu mafumbo ya kusadikiwa na amri za kutekelezwa. Mahubiri ya Injili yanatakiwa kuwa roho na uzima; ili mtume asikate tamaa katika mapingamizi yote anayopambana nayo ni lazima awe na njaa na kiu ya haki ya Mungu, awe na kipaji cha nguvu aweze kudumu mpaka mwisho na kuvuta watu. Hizo njaa na kiu zinakua katika liturujia na sala ya moyo. Hasa adhimisho la misa, pamoja na muungano na Mungu unaopatikana humo, ndio kilele ambapo ububujike mto wa mahubiri hai ya Neno la Mungu. Ili awe “Kristo mwingine”, padri anatarajiwa kuzama katika sadaka ya msalaba inayodumu kutolewa altareni. Huko kuzama kuwe roho yenyewe ya utume inayofanana na chemchemi hai daima zinazotiririsha mito mikubwa. Kifupi ni kwamba, ili tuwalete wengine kwa Mungu ni lazima kwanza tuwe tumeungana naye kwa dhati.
Masharti na matunda ya utume
haririMatunda ya utume yanatakiwa kuwa uongofu wa wasio Wakristo na wa waamini wakosefu pamoja na maendeleo ya waadilifu: kwa jumla, ni wokovu wa roho. Lakini kwa ajili hiyo Bwana hakuridhika kuhubiri ukweli, bali alikufa msalabani. Vivyo hivyo mitume hawawezi kuokoa watu kwa mahubiri tu, bila kuteseka kwa ajili yao. “Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; sikuzote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu” (2Kor 4:8-10). Mwenyewe, alipowaahidia mara mia wale wanaomfuata aliwatabiria dhuluma za namna hiyo (taz. Mk 10:30).
“Kama vile Bwana wetu alivyotimiza ukombozi wa ulimwengu kwa msalaba wake tu… hata watenda kazi ya Injili wanagawa tu neema za ukombozi kwa msalaba wao na kwa dhuluma zinazowatesa. Kwa hiyo hakuna cha kutumainia kutokana na huduma yao isipoendana na mapingamizi, masingizio, matusi na mateso. Baadhi wanadhani kutenda maajabu kwa sababu mahubiri yao yametungwa vizuri, wanayatoa kwa ufasaha, wanasifiwa na kupokewa vema kila mahali. Lo! Wanavyodanganyika! Njia wanazozitegemea si zile ambazo Mungu anazitumia ili kutenda makuu. Ili kuokoa ulimwengu inahitajika misalaba. Mungu anaongoza katika njia ya msalaba wale anaowatumia kuokoa watu” (Alois Lallemant).
Wamisionari wengi waliuawa kikatili, na damu yao ikawa mbegu ya Wakristo wapya! Uhai wa Kanisa, kama ule wa mwanzilishi wake umepitia mautini na hivyo unadumu kuwa na nguvu na kuzaa matunda yasiyoisha. Kwamba utume unatakiwa “utokane na utimilifu wa sala ya kumiminiwa” (Thoma wa Akwino) ni uthibitisho mwingine wa kwamba, kuzama katika mafumbo kwa imani hai iliyoangazwa na vipaji vya Roho Mtakatifu ni katika njia ya kawaida ya utakatifu, hasa kwa padri anayetakiwa kuongoza watu, kuwaangaza na kuwafikisha kwenye ukamilifu.
Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |