Mtaguso wa pili wa Vatikani

(Elekezwa kutoka Mtaguso wa pili wa Vatikano)

Mtaguso wa pili wa Vatikani ni mtaguso mkuu wa pili wa Kanisa Katoliki kufanyika Vatikani (11 Oktoba 1962 - 8 Desemba 1965).

Basilika la Mt. Petro ambamo mtaguso ulifanyika.

Historia

 
Maandamano ya kuanzia kikao cha pili cha mtaguso yakiingia Basilika la Mt. Petro.
 
Wanamtaguso waliokaa ndani ya Basilika.

Muda mfupi baada ya kuchaguliwa, Papa Yohane XXIII alitangaza uamuzi wake wa kuitisha Mtaguso Mkuu akiamini kwamba utaweza kuandaa na kusababisha ustawi mpya wa maisha ya Kanisa.

Lengo kuu la mtaguso lilikuwa kuliamsha Kanisa Katoliki likumbuke wito wake na kwa kujifanya upya kwa ndani lipate msukumo mpya wa kimisionari ili kuwatangazia watu wote ujumbe wa milele wa wokovu, amani na umoja.

Tangazo hilo lilitolewa tarehe 25 Januari 1959. Baada ya maandalizi marefu, mtaguso wa pili wa Vatikano ulifunguliwa tarehe 11 Oktoba 1962. Vikao vinne vikafanyika mpaka ulipofungwa tarehe 8 Desemba 1965. Kila kikao kilianza Oktoba na kumalizika Desemba ya miaka hiyo.

Jina la mtaguso mkuu huo, ambao ni wa 21 kwa Kanisa Katoliki, linatokana na kwamba ni wa pili kufanyika katika mtaa wa Vatikani, ambao ni nchi huru ndani ya mji wa Roma.

Kwa kuwa Yohane XXIII alifariki tarehe 2 Juni 1963, vikao vitatu vya mwisho viliongozwa na mwandamizi wake, Papa Paulo VI, na hati zote kumi na sita zikatolewa chini yake pia kwa kupigiwa kura ya ndiyo karibu kwa kauli moja.

Maaskofu na wakuu wa mashirika kadhaa wenye haki ya kupiga kura walikuwa kama elfu tatu, wakiwakilisha karibu Kanisa lote duniani, isipokuwa nchi zile zenye kuwadhulumu Wakristo.

Orodha ya hati 16 za mtaguso

Zinaorodheshwa kwa kutaja kwanza hadhi ya hati, halafu jina rasmi la Kilatini, kifupisho chake, mada na tarehe ya kutolewa.

Katiba

1. Sacrosanctum Concilium (SC) Liturujia takatifu 4-12-1963

2. Lumen Gentium (LG) Kanisa 21-11-1964

3. Dei Verbum (DV) Ufunuo wa Kimungu 18-11-1965

4. Gaudium et Spes (GS) Kanisa katika ulimwengu wa kisasa 7-12-1965

Maagizo

1. Inter Mirifica (IM) Vyombo vya upashanaji habari 4-12-1963

2. Orientalium Ecclesiarum (OE) Makanisa katoliki ya Mashariki 21-11-1964

3. Unitatis Redintegratio (UR) Ekumeni 21-11-1964

4. Christus Dominus (CD) Huduma ya kichungaji ya maaskofu 28-10-1965

5. Perfectae Caritatis (PC) Kurekebisha upya maisha ya kitawa 28-10-1965

6. Optatam Totius (OT) Malezi ya kipadri 28-10-1965

7. Apostolicam Actuositatem (AA) Utume wa walei 18-11-1965

8. Ad Gentes (AG) Utendaji wa kimisheni wa Kanisa 7-12-1965

9. Presbyterorum Ordinis (PO) Huduma na maisha ya kipadri 7-12-1965

Matamko

1. Gravissimum Educationis (GE) Malezi ya Kikristo 28-10-1965

2. Nostra Aetate (NA) Uhusiano wa Kanisa na dini zisizo za Kikristo 28-10-1965

3. Dignitatis Humanae (DH) Uhuru wa dini 7-12-1965

Mapokezi ya mtaguso

Wakristo walio wengi walipokea kazi ya mtaguso kwa mikono miwili, na wengi nje ya Kanisa pia waliridhika sana. Kutokana nao yamepatikana matunda mengi, lakini zimejitokeza hata kasoro na shida kwa sababu mbalimbali, hasa kwa kutoelewa wala kutotekeleza sawasawa maagizo yake. Kwa vyovyote hatuwezi kusema yote yaliyotokea baada ya mtaguso yamesababishwa nao, k.mf. maovu yaliyofanywa na baadhi ya mapadri hayamo kabisa.

Pamoja na upinzani wa wazi wa mifumo kadhaa ya kisiasa (ukomunisti na ubepari) na matapo mengine (Wamasoni n.k.) dhidi ya Kanisa, hali ya jumla ya ulimwengu inazidi kuelekea anasa na kuabudu utajiri hata kuzima maisha ya kiroho. Hivyo ni vigumu kufanikisha mtaguso.

Hata ndani ya Kanisa wengi wamesoma hati zake kijuujuu, wakishikilia upande mmoja na kutojali wa pili. Wengine wamevunjika moyo kuona utekelezaji wa mtaguso unavyokwenda polepole. Wengine wameshughulikia miundo tu ya Kanisa, bila ya kujali fumbo la Kimungu lililomo ndani yake. Pengine umekosekana upambanuzi, k.mf. wengi walipofuata mitazamo ya ulimwengu uliomuasi Mungu badala ya kujadiliana nao ili kuuokoa.

Matatizo yaliyojitokeza baada ya mtaguso yamewaonyesha Wakatoliki haja ya kuupokea vizuri zaidi, kwa kupiga hatua nne zifuatazo: 1. Hati za mtaguso zijulikane na watu wengi zaidi na kwa dhati zaidi. 2. Zipokewe kwa moyo. 3. Zizingatiwe kwa upendo. 4. Zitekelezwe maishani.

Namna ya kuelewa mtaguso

Tukitaka kuelewa vizuri hati za mtaguso, ni lazima tuzizingatie zote 16 zilivyo na zinavyofungamana.

Ni lazima pia tutie maanani hasa katiba zake 4, kwa kuwa ndizo hati kuu zinazotuwezesha kuelewa maagizo 9 na matamko 3.

Tena hatutakiwi kutenganisha mtazamo wa kichungaji na msingi wa imani wa hati hizo, wala kutenganisha roho ya mtaguso na hati zenyewe.

Mwishowe mtaguso ueleweke katika mapokeo ya Kanisa kwa kuwa katika mitaguso yote Kanisa ni lilelile.

Tahadhari hizo zote zinahitajika kwa sababu katika kutekeleza mtaguso yamejitokeza maelekeo mawili ambayo yanapingana na kuvuruga hali ya Kanisa.

La kwanza linadai mabadiliko yasiyolingana na mtaguso, ingawa wenyewe wanasema ni maendeleo yanayotakiwa na roho ya mtaguso. Maendeleo ya namna hiyo hayakubaliki kwa sababu hayajali mapokeo ya mitume yanayodai imani idumu kuwa ileile.

La pili linaambatana na mambo ya zamani, bila ya kujali ishara za nyakati zetu zinazodai mambo mapya pia kwa wokovu wa watu wa leo na wa kesho.

Ni wajibu wa maaskofu chini ya Papa kutambua yapi yanajenga na yapi yanazuia ujenzi au pengine yanabomoa Kanisa. Ndiyo kazi inayofanyika hasa katika sinodi (= pamoja-njia, yaani kusafiri pamoja).

Kati ya sinodi za ngazi mbalimbali kuanzia ile ya jimbo, muhimu zaidi ni zile za kimataifa zinazofanyika mara kwa mara huko Roma (mtaa wa Vatikano), zikikusanya maaskofu wawakilishi wa nchi zote na baadhi ya wakuu wa mashirika ya kitawa.

Juhudi za kutekeleza mtaguso

Kama vile mitaguso mikuu iliyotangulia kupanga urekebisho wa hali ya Kanisa, mtaguso wa pili wa Vatikano pia ujumbe wake hautaweza kuzaa matunda isipokuwa kwa juhudi za muda mrefu.

Miaka ishirini baada ya mtaguso kumalizika, sinodi maalumu ya maaskofu iliyoitishwa ili kutathmini matokeo yake ilisema wazi kuwa kazi bado sana, kwa namna ya pekee kuhusu kulenga utakatifu kwa waamini wote.

Ndiyo maana ilihamasisha juhudi zifanyike ili ujumbe wa mtaguso usikilizwe upya katika kila jimbo.

HATI ZA MTAGUSO MKUU WA VATIKANO II – tafsiri ya Familia za Maamkio – ed. TEC – Baraza la Maaskofu Tanzania – Ndanda 2001 – ISBN 9976-63-649-0

Marejeo

  • Amerio, Romano (1996). Iota Unum. Kansas City: Sarto House. ISBN 0-9639032-1-7.
  • van Bühren, Ralf (2008). Kunst und Kirche im 20. Jahrhundert. Die Rezeption des Zweiten Vatikanischen Konzils (kwa German). Paderborn: Schöningh. ISBN 978-3-506-76388-4. {{cite book}}: Unknown parameter |trans_title= ignored (|trans-title= suggested) (help)CS1 maint: unrecognized language (link)
  • Bredeck, Michael (2007). Das Zweite Vatikanum als Konzil des Aggiornamento : zur hermeneutischen Grundlegung einer theologischen Konzilsinterpretation (kwa German). Paderborn: Schöningh. ISBN 978-3-506-76317-4. {{cite book}}: Unknown parameter |trans_title= ignored (|trans-title= suggested) (help)CS1 maint: unrecognized language (link)
  • Gherardini, Brunero (2011). "Sull'indole pastorale del Vaticano II: una valutazione". Katika Lanzetta, Serafino (mhr.). Concilio Vaticano II, un concilio pastorale. Analisi storico-filosofico-teologica (kwa Italian). Frigento, IT: Casa Mariana Editrice. ISBN 978-88-905611-2-2. {{cite book}}: Unknown parameter |trans_title= ignored (|trans-title= suggested) (help)CS1 maint: unrecognized language (link)
  • ——— (2012), Il Vaticano II. Alle radici d'un equivoco, Torino: Lindau, ISBN 978-88-7180-994-6 {{citation}}: Unknown parameter |trans_title= ignored (|trans-title= suggested) (help).
  • O'Malley, John W. (2008). What Happened at Vatican II. Harvard University Press. ISBN 978-0-674-03169-2.
  • Kelly, Joseph F. (2009). The Ecumenical Councils of the Catholic Church: a History. Collegeville: Liturgical Press. ISBN 0-8146-5376-6.
  • Likoudis, James (2006). The Pope, the Council, and the Mass. Emmaus Road Publishing. ISBN 978-1-931018-34-0.
  • Linden, Ian (2009). Global Catholicism: diversity and change since Vatican II. 41 Great Russell St, London: Hurst & Co. uk. 337. ISBN 978-1-85065-957-0.{{cite book}}: CS1 maint: location (link)
  • Orsy, Ladislas (2009). Receiving the Council: Theological and Canonical Insights and Debates. Collegeville: Liturgical Press. ISBN 0-8146-5377-4.
  • Sinke Guimarães, Atila (1997). In the Murky Waters of Vatican II. Metairie: MAETA. ISBN 1-889168-06-8.
  • Wiltgen, Ralph M. (1991). The Rhine flows into the Tiber. TAN books. ISBN 0-89555-186-1.

Viungo vya nje