Asteroidi (kutoka Kigiriki ἀστήρ aster = nyota na είδες -eides= ya kufanana) ni kiolwa cha angani kinachozunguka jua jinsi inavyofanya sayari. Ni ndogo kuliko sayari kibete lakini kubwa kushinda kimondo-anga. Mara nyingi huitwa pia "planetoidi" kwa sababu tabia zao zinalingana katika mengi na sayari.

253 Mathilde ni asteroidi yenye vipimo vya 66×48×46 km
Ukanda wa asteroidi katika mfumo wa jua letu

Jina

Istilahi ya asteroidi ilianzishwa na William Herschel mnamo mwaka 1802 kutokana na neno la Kigiriki ἀστεροειδής astero-eides inayomaanisha "ya kuonekana kama nyota". Tangu siku zake neno hili lilitumiwa kutaja violwa vidogo kwenye anga la nje vinavyoakisia nuru ya kutosha ili kuonekana kwenye darubini. Kutokana na maendeleo ya teknolojia idadi ya magimba yanayoweza kuangaliwa iliongezeka.

Asteroidi zinazovumbuliwa na wanaastronomia hupokea jina linaloweza kupendekezwa na mvumbuzi wake pamoja na namba mbele ya jina hili. Asteroidi ya kwanza iliyogunduliwa ilikuwa Ceres[1]. Namba zinatolewa mfululizo na zinaonyesha nafasi yake katika historia ya uvumbuzi wa asteroidi. Leo hii takriban lakhi 2.5 zimepewa majina ya aina hii kati ya lakhi saba na nusu zinazojulikana[2].

Asteroidi, kimondo, sayari kibete

Ukubwa wa asteroidi ni kati ya kipenyo cha kilomita 1,000 hadi mita kadhaa. Hakuna tofauti ya kimsingi kati ya asteroidi na kimondo isipokuwa ukubwa na mpaka kati yao unachorwa na watazamaji wa kibinadamu. Ufafanuzi wa mpaka huu haukusanifishwa bado; ukubwa wa takribani mita 10 ulipendekezwa kuwa kipimo cha kutofautisha kimondo (kipenyo chini ya mita 10) na asteroidi (juu ya mita 10)[3].

Tangu mwaka 2006 umoja wa kimataifa wa wanaastronomia umeamua kutofautisha kati ya asteroidi na sayari kibete. Sayari kibete ni gimba mango kubwa lenye masi ya kutosha kufikia umbo la tufe. Kutokana na mapatano haya violwa vilivyohesabiwa kama asteroidi kubwa kama Ceres siku hizi huitwa sayari kibete. Hakuna ufafanuzi rasmi wa kimondo (meteoridi) bado.

Ukanda wa asteroidi

Katika mfumo wa jua letu kuna angalau asteroidi 338,000 zilizotambuliwa hadi leo na wanaastronomia. Nyingi zinazunguka katika ukanda wa asteroidi kati ya njia za Mirihi (Mars) na Mshtarii (Jupiter). Wataalamu hutofautiana kati yao kama hizi ni ama mabaki ya sayari iliyopasuliwa baada ya kugongana na magimba mengine au vipande vya visayari ambavyo havikuendelea kukua.

Makundi mengine ya asteroidi hufuatana na Mshtarii zikizunguka kwenye obiti yake, huitwa "Watroia" na "Wagiriki". Hupokea majina ya wahusika kutoka utenzi wa Iliadi kuhusu vita ya Wagiriki dhidi ya Troia.

Hatari kutokana na asteroidi zinazokaribia dunia

Katika historia ya dunia asterodi zimewahi kugonga dunia yetu mara kadhaa. Kama asteroidi inaelekea karibu na obiti ya dunia inaitwa kiolwa cha kukaribia dunia. Katika historia ya dunia migongano ilikuwa na athari kubwa na kusababisha mara kadhaa vifo vya spishi nyingi. Kutoweka kwa dinosauri inaaminiwa lilisababishwa na asteroidi kubwa iliyogonga uso wa dunia katika eneo la Yucatan huko Meksiko.

Katika historia ya kisasa tukio la Tunguska kwenye mwaka 1908 nchini Urusi lilitazamiwa kama pigo la kimondo kikubwa au asteroidi ndogo. Tangu 2014 siku ya asteroidi ilianza kukumbukwa duniani kwenye tarehe ya Juni 30 ambayo ni tarehe ya tukio la Tunguska kwa shabaha ya kuunda ufahamu wa changamoto ya kujiandaa.

Katika miaka iliyopita taasisi za usafiri wa anga-nje kama NASA na ESA zimeanza utafiti wa undani kuhusu hatari hiyo na kupanga majaribio jinsi gani kulenga asteroidi mbali na dunia. [4]

Tazama pia

Marejeo

  1. Ceres inatazamiwa siku hizi kama sayari kibete
  2. How Many Solar System Bodies, tovuti ya NASA, iliangaliwa Aprili 2018
  3. Beech, M. & Steel, D.: On the Definition of the Term Meteoroid, Quarterly Journal of the Royal Astronomical Society, Vol. 36, NO. 3/SEP, P. 281, 1995,
  4. How to stop an asteroid hitting earth Archived 8 Machi 2016 at the Wayback Machine., Guardian Tuesday 30 June 2015
  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Asteroidi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.