Mshtarii (alama: ♃; pia Mshiteri, Mushtarii au Mshatira[1], kutokana na Kiarabu المشتري al-mushtari; na hata Jupita kutokana na Kiingereza Jupiter[2]) ni sayari ya tano toka kwenye jua katika Mfumo wa jua na sayari zake.

Picha ya Mshtarii iliyopigwa na chombo cha angani Cassini
Ulinganishi wa ukubwa wa Dunia yetu (kushoto) na Mshtarii pamoja na "doa jekundu" inayozunguka katika angahewa ya Mshtarii.

Mshtarii ni sayari kubwa kabisa ya jua letu. Masi yake inazidi mara mbili na nusu masi ya sayari zingine zote pamoja.

Angahewa

Mshtarii haina uso unaoonekana. Sehemu kubwa ya masi ya sayari ni elementi nyepesi kama hidrojeni na heli ambazo ni gesi katika mazingira ya duniani. Hii ndiyo sababu ya kwamba sayari kubwa za Mshtarii pamoja na Zohali huitwa "sayari jitu za gesi".

Kadiri gesi hizo zinavyopatikana chini zaidi (yaani kuelekea ndani) uzito wa matabaka ya juu unaongeza shinikizo katika vilindi vyake na kusababisha gesi za angahewa kuingia katika hali ya giligili (majimaji) inayobadilika kuwa mango (imara) ndani zaidi. Zamani iliaminika ya kwamba sayari yote ni ya gesi iliyoganda lakini siku hizi wataalamu wa astronomia huamini kwamba kuna kiini cha mwamba au metali.

Doa jekundu linaloonekana usoni mwa angahewa ni dhoruba ya tufani kubwa sana iliyotazamwa tangu darubini za kwanza zilipopatikana. Duniani tufani zinapotea kwa kawaida baada ya wiki kadhaa lakini doa jekundu limeendelea bila kusimama kwa miaka 300.

Miezi

Mshtarii ina miezi 79 iliyotambuliwa hadi mwaka 2018[3].

Miezi minne mikubwa ilitambuliwa mwaka 1610 na Galileo Galilei aliyekuwa kati ya wanaastronomia wa kwanza kutumia darubini. Ndiyo Io, Europa, Ganimedi na Kallisto. Ukubwa wa Ganimedi unakaribia kipenyo cha Utaridi ukipita kile cha Pluto. Miezi 63 huwa na kipenyo chini ya kilomita 10. Mwezi mdogo kabisa wa Mshtarii unajulikana kwa namba tu na una kipenyo cha km 1.

Tanbihi

  1. kuhusu majina ya sayari zilizojulikana kwa Waswahili na hivyo kuwa na majina ya asilia linganisha Jan Knappert, Swahili Islamic poetry, Brill 1971, Vol 1 uk 96-97 - taz google booksearch [1]
  2. Umbo lingine ni Sumbula linalotumiwa kimakosa na vitabu kadhaa vya shule pia na kamusi chache. Sumbula ni jina la Kiswahili la nyota Alfa Virginis au en:Spica, si la sayari yoyote
  3. Sheppard, Scott S.. The Giant Planet Satellite and Moon Page. Department of Terrestrial Magnetism at Carnegie Institution for Science. Jalada kutoka ya awali juu ya June 7, 2009. Iliwekwa mnamo December 19, 2014.
  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mshtarii kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.