Mirihi

sayari ya nne katika mfumo wa jua


Ukitafuta mungu ya dini ya Roma ya Kale anayeitwa Mars kwa lugha ya Kiingereza tazama Mars (mungu)

Mirihi
Picha ya Mirihi, jinsi ilivyopigwa na mamlaka ya anga-nje ya Falme za Kiarabu mnamo Agosti 2021.
Picha ya Mirihi, jinsi ilivyopigwa na mamlaka ya anga-nje ya Falme za Kiarabu mnamo Agosti 2021.
Jina
Asili ya jinaKar. المريخ (al-miriikh)
Majina mengine
Murihi[1], sayari nyekundu
Mars (Kng.)
Alama♂
Tabia za mzunguko
Mkaribiokm 206,650,000
au 1.3814
Upeokm 249,261,000
au 1.66621
km 227939366
au 1.52368055
Uduaradufu0.0934
siku 686.980
miaka 1.88085
Mwinamo1.850° toka njia ya Jua
MieziFobo na Deimo
Tabia za maumbile
km 3389.5 ± 0.2
Tungamokg 6.4171×1023
g/cm3 3.9335
Uvutano wa usoni
m/s2 3.72076
siku 1.02749125
siku 1.025957
Weupe0.25 (Bond)
0.170 (jiometri)
HalijotoK 213.15 (−60°C)

Mirihi ni sayari ya nne katika Mfumo wa Jua. Hivyo ni sayari jirani ya Dunia iliyo sayari ya tatu.

Sura ya Mirihi inafanana zaidi na ile ya Dunia yetu kati ya sayari zote ilhali haina joto wala baridi kali mno.

Kutokana na rangi yake, iliyosababishwa na wingi wa kutu, imeitwa "sayari nyekundu".

Ina miezi miwili midogo inayoitwa Fobo na Deimo.

Asili ya jina

Hatuna taarifa kuhusu majina ya Kibantu kwa sayari hii. Mabaharia Waswahili waliijua wakaitumia wakitafuta njia yao baharini wakati wa usiku[2]. Walipokea jina la "Mirihi" kutoka kwa Waarabu wanaoiita المريخ al-miriikh[3] inayoweza kuchukuliwa kama tafsiri ya jina la Kigiriki Πυρόεις piroes "mwenye moto"[4]. Sababu ya jina hili ni rangi nyekundu inayoonekana tukiangalia sayari hii kwa macho matupu. Rangi nyekundu ilikuwa pia sababu ya kuona ni sayari ya damu na hivyo kuiona kama mwakilishi wa mabaya, jinsi walivyofanya Wababeli. Wagiriki waliona Mirihi pia kama mwakilishi wa mungu wa vita Ares na jina hili lilipokewa na Waroma wa Kale wakiitafsiri kwa mungu wao wa vita, Mars. Jina la Mars likadumu katika utamaduni wa Ulaya kutokana na umuhimu wa lugha ya Kilatini, likawa jina la kimataifa lililokubaliwa rasmi na UKIA[5].

Njia mzingo yake ya kuzunguka Jua

Mirihi inazunguka Jua kwa umbali wa kilomita milioni 206.62 hadi 249,23, ikitumia karibu miaka miwili ya kidunia (mwaka 1 siku 321 na saa 18) kwa obiti (njia mzingo) yake. Mzingo wa kuzunguka Jua imeinama 1.85° kutoka ekliptiki. Obiti yake imekaribia umbo la duara ikiwa afeli yake ina umbali wa vizio astronomia 1.666 na periheli ina umbali wa vizio astronomia 1.3814 kutoka Jua.

Tabia za kifisikia

 
Ulinganisho wa ukubwa: Picha zenye skeli ileile za Dunia na Mirihi kandokando

Kipenyo cha Mirihi ni km 6.794 (takriban nusu kipenyo cha Dunia); eneo la uso wake ni nusu ya eneo la uso wa Dunia; masi yake ni sehemu ya kumi tu ya masi ya Dunia.

Mirihi inazunguka kwenye kipenyo chake katika saa 24 na dakika 37 za kidunia. Kipenyo cha mzunguko kimenama 25° 12' dhidi ya njia ya mzingo wa kuzunguka Jua. Hali hii inasababisha majira ya joto na ya baridi inayofanana na Dunia, lakini kutokana na muda wa mwaka hata muda wa majira ni mrefu kuliko duniani.

Angahewa

Angahewa ya Mirihi ni haba sana, yenye shinikizo la Pascal 750 tu, yaani 0.75% ya shinikizo la hewa duniani.

Hewa yake ni hasa dioksidi ya kaboni (95%), nitrogeni (3%), argoni (1.6%) ikionyesha pia dalili hafifu za oksijeni na maji.

Kutokana na uhaba wa hewa joto lililopokewa kutoka Jua linapotea haraka sana, hivyo kuna baridi wakati wa usiku. Halijoto karibu na ikweta wakati wa majira ya joto ni kati ya 20°C wakati wa mchana na hadi –85°C wakati wa usiku.

Mirihi ina upepo na mawingu. Nchani pana barafu ya daioksidi ya kaboni pia barafu ya maji inayoyeyuka wakati wa joto na kusababisha mawingu. Majira kati ya baridi na joto hutokea dhoruba kali zinazotupa vumbi nyingi hewani ya kufunika sehemu kubwa za uso wa sayari.

Uso wa Mirihi

 
Eneo lilipotelemka chombo cha angani cha NASA Vikinglander

Uso wa sayari inaonyesha tofauti kubwa kati ya kizio cha kaskazini na kizio cha kusini. Kaskazini pana hasa tambarare, kusini kuna hasa milima na nyanda za juu. Kutokana na uhaba wa maji hakuna bahari au mito lakini kuna dalili kama mabonde makavu yanayoonyesha ya kwamba zamani mito ilikuwepo.

Tambarare za kaskazini zina mchanga na vumbi nyingi. Maeneo haya yana rangi tofauti: mengine yanaonekana meusimeusi kwa darubini. Maeneo haya yaliaminiwa zamani ndiyo bahari, hivyo yaliitwa kwa jina la Kilatini "mare" (bahari) kama vile Mare Erythraeum au Mare Sirenum.

Katika kizio cha kusini ndipo milima mikubwa inayojulikana ulimwenguni hadi leo. Mlima mkubwa kabisa, wenye kimo cha km 26 (zaidi ya mara nne urefu wa Kilimanjaro), ndio Olympus Mons (Mlima wa Olimpiki), volkeno , ambayo ni kubwa kuliko zote za Mfumo wa Jua. Mazingira yake mengine yenye milima mikubwa huitwa Tharsis kuna pia volkeno.

Ncha za kaskazini na kusini zina vilele vya barafu. Sehemu kubwa ya barafu hii ni daioksaidi ya kaboni iliyoganda, sehemu ndogo ni barafu ya maji. Kilele cha barafu cha kaskazini kina kipenyo cha km 1000 wakati wa majira ya joto; unene wa barafu hukadiriwa kuwa km 5. Kilele cha barafu cha kusini ni kidogo: kipenyo chake ni km 350 tu, unene wake takriban km 1.5.

Katika eneo la ikweta ya Mirihi kuna bonde la ufa kubwa sana, lenye urefu wa km 4000 na kina hadi m 7000.

Vyombo vya angani vimefika Mirihi na kutuma picha. Hali halisi uso wa sayari ni jangwa kubwa sana.

 
Dhoruba ya vumbi Mirihini (picha zilipigwa na chombo cha NASA mwaka 2004)

Mifereji

Mirihi ni sayari iliyoaminika kuwa na uhai hata aina ya wanadamu. Tofauti na sayari nyingine jirani na Dunia yetu, ambayo ni Zuhura (au Ng'andu), uso wa Mirihi unaonekana kwa darubini. Katika karne ya 19 BK wanaastronomia, hasa Mwitalia Giovanni Schiaparelli, waliona alama kama mistari kwenye uso wa Mirihi. Schiaparelli aliita mistari hii kwa neno la Kiitalia "canali" yaani mifereji. Jina hili lilisababisha watu wengi kujiuliza: mifereji imepatikana namna gani? Halafu katika eneo la mistari hii mabadiliko ya rangi ilionekana. Haya yote yamesababisha dhana na makadirio ya kuwa mifereji imechimbwa kwa kusudi la kupeleka maji maeneo makavu yanayomwagiliwa na kuonyesha rangi ya mazao kimajira. Kumbe lazima kuwe na wachimbaji, kwa hiyo wako aina ya watu wenye utamaduni. Watu hao waliozaliwa katika fikra za wanaastronomia na waandishi wa vitabu walijulikana kote duniani; baadaye imani ilianza ya kuwa wanatutembelea duniani.

Leo imegunduliwa ya kwamba sehemu kubwa ya mistari iliyoripotiwa na Schiaparelli haiko, tena si mifereji. Sababu ya kuiona ilikuwa hali ya darubini ya zamani pamoja na kuchoka kwa macho ya watazamaji. Mistari kadhaa iko kweli, lakini si mifereji iliyochimbwa, bali mabaki ya mito ya kale kutoka zamani Mirihi ilipokuwa bado na maji. Mabadiliko katika rangi kwenye sehemu ya uso za Mirihi yamejulikana ni kutokana na dhoruba kubwa yanayorusha vumbi kwenye angahewa.

Tanbihi

  1. Knappert, Jan. The Cosmology of Swahili Islamic Literature, in: Swahili Islamic poetry, Brill 1971, v. 1, uk 96 [1]
  2. Knappert, Jan. "The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations." In: The Indian Ocean Review, Perth, Australia, v. 6 n. 3, September 1993, uk 5-7
  3. Zizi مرخ m-r-kh kwa Kiarabu cha kisasa inamaanisha "kujipakia" (kamusi ya Wehr); lakini Lane inataja kichaka cha مرخ "A certain kind of tree that quickly emits fire" (Lane,Edward William,An Arabic‐English Lexicon:Derived from the Best and the Most Copious Eastern Sources, uk 5802)
  4. πυρόεις, Liddell, Scott, Jones Ancient Greek Lexicon (LSJ), tovuti ya lsj.gr
  5. Naming of Astronomical Objects, major planets and Moon, tovuti ya UKIA, iliangaliwa Mei 2019