Kiolwa cha kukaribia Dunia

(Elekezwa kutoka Kiolwa cha kukaribia dunia)

Kiolwa cha kukaribia Dunia (Ing. Near Earth Object) ni kiolwa cha angani kama vile asteroidi, nyotamkia, kimondo kinachoweza kukaribia Dunia yaani sayari yetu tunapoishi.

Njia ya asteroidi 2012 DA14 iliyokaribia dunia mwezi wa Februari 2013
Katikati: Dunia (earth) yetu; duara ya kijani: njia ya satelaiti zinazozunguka dunia; mstari buluu: njia ya asteroidi 2012DA12; mstari wa kijivu: mzingo wa mwezi ukizunguka dunia

Hali halisi violwa hivi hufuata obiti za kuzunguka Jua zinazokaribia Dunia yetu. Hapa kuna uwezekano wa mgongano wa gimba la angani na Dunia. Migongano ya vimondo vidogo hutokea kila siku lakini kama kiolwa ni kikubwa kiasi kuna hatari. Tangu wataalamu wa astronomia wametambua hatari hii kuna jitihada za kutambua na kujua violwa vinavyoweza kuunda hatari ya aina hii.

Hatari kutokana na violwa vya kukaribia dunia

Sehemu kubwa ya violwa vinavyokaribia dunia si hatari kwa sababu ni vidogo sana vikiwaka mara baada ya kusuguana na molekuli za angahewa.

Hadi juzi wataalamu wa Marekani walitazama violwa vyenye kipenyo cha mita 100 na zaidi kuwa na hatari.

Lakini tar. 15 Februari 2013 mlipuko wa kimondo kilichokadiriwa kuwa na kipenyo cha mita 17 pekee kilisababisha uharibifu katika eneo la mji wa Chelyabinsk nchini Urusi. Kimondo kikubwa kilichoharibu eneo la kilomita za mraba 2000 huko Tunguska mwaka 1908 imekadiriwa kuwa na kipenyo chini ya mita 100. Kama tukio kama Tunguska lingetokea juu ya mji mkubwa lingeua watu wengi sana.

Uharibifu unaoweza kutokea kwa anguko la kimondo au asteroidi hutegemea masi yake, kipenyo, muundo wake na kiwango cha pembe jinsi kinavyoingia katika angahewa. Sehemu kubwa ya masi ya vimondo inaweza kuwaka hewani, au kimondo kupasuka kilomita nyingi juu ya uso wa dunia. Kadri jinsi kupasuka kunatokea kwenye kimo kikubwa au karibu zaidi na uso wa dunia uwezo wa uharibifu unaongezeka.

Asteroidi na vimondo vingi vinaanguka juu ya maeneo pasipo na watu kama baharini (bahari hufunika zaidi ya 2/3 ya uso wa dunia) au porini. Lakini asteroidi kubwa ni hatari hata kwa bindamu na maisha yote duniani. Asteroidi kubwa inayojulikana kuwa njiani ya kukaribia dunia ni (29075) 1950 DA yenye kipenyo cha kilomita moja ambayo itakaribia Dunia kiasi kisichojulikana bado kikamilifu kwenye mwaka 2280.

Wataalamu wa biolojia na jiolojia huamini ya kwamba kupotea kwa Dinosauri kulisababishwa na pigo la asteroidi kubwa iliyogonga Dunia kwenye pwani la Meksiko. Mgongano huu ulisababisha kutokea kwa kasoko ya Chicxulub na kurusha vumbi na moshi mwingi kwenye anagahewa. Hivyo nuru ya Jua ilishindwa kufika kwenye uso wa Dunia, halijoto ikapoa ghafla na baridi iliangamiza mimea na wanyama wengi duniani, pamoja na dinosauri.

Tazama pia

Viungo vya Nje

Marejeo