Kasi ya Masakini (kundinyota)

(Elekezwa kutoka Corona Borealis)

Kasi ya Masakini (Corona Borealis kwa Kilatini na Kiingereza) [1] ni jina la kundinyota kwenye angakaskazi ya Dunia.

Nyota za Kasi ya Masakini (Corona Borealis) katika mazingira yao angani
Ramani ya kundinyota Kasi ya Masakini (Corona Borealis) jinsi inavyoonekana kwenye angakaskazi

Mahali pake

Kasi ya Masakini ni kundinyota dogo linapakana na Bakari (en:Boötes) upande wa kaskazini, Hayya (en:Serpens) upande wa kusini na Rakisi (en:Hercules) upande wa mashariki.

Jina

Kasi ya Masakini lilijulikana kwa jina hili kwa miaka mingi kati ya mabaharia Waswahili waliotumia nyota kutafuta njia baharini wakati wa usiku.[2]

Jina la Kasi ya Masakini limepokelewa kutoka kwa Waarabu walioona hapa “bakuli ya maskini” قصعة المساكين qaṣʿa(t) al-masaakiin[3]yaani bakuli inayotumiwa na waombaomba kupokea chakula kutoka kwa wenye huruma. Jina nyingine kati ya Waarabu ilikuwa pia al-fakka yaani "iliyovunjika" wakiona bakuli iliyokatika maana duara ya nyota si kamili, lakini sasa jina hili hutumiwa kwa nyota angavu zaidi tu inayoitwa Faka kwa Kiswahili au Alphecca kwa Kilatini na Kiingereza. Jina rasmi la Corona Borealis kwa maana ya “taji ya kaskazini” ni Kilatini na tafsiri ya Kigiriki Στέφανος βόρειος stefanos borios. Wagiriki wa Kale waliona hapa shada la heshima la majani jinsi walivyowapa washindi wa michezo. Shada la heshima liliendelea baadaye kutazamiwa kama taji na hapo asili ya jina la kimataifa “Corona” linalomaanisha taji. Wagiriki walisimulia hapa hadithi ya mitholojia yao ambako mungu Dioniso alimpa Ariadne taji na baadaye kuirusha angani kama kumbukumbu ya upendo wake.

Ilhali kuna makundinyota mawili yanayoitwa Corona zinatofautishwa kwa kuitwa ya kaskazini na ya kusini, hivyo Kobe ni Corona Australis (ya kusini) na Kasi ya Masakini ni Corona Borealis (ya kaskazini).

Kasi ya Masakini ni kati ya makundinyota yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika karne ya 2 BK. Iko pia katika orodha ya kundinyota 88 ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [4] kwa jina la Corona Borealis. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'CrB'.[5]

Nyota

Kasi ya Masakini ina hasa nyota 7 zinazofanya umbo la bakuli au taji. Kwa jumla kuna nyota 37 zenye mwangaza unaoonekana wa 6.6 na zaidi yaani zinaonekana kwa macho matupu.

Nyota angavu zaidi ni Faka[6] (en:Alphecca au α Alfa Coronae Borealis) yenye mwangaza unaoonekana wa 4.3 ikiwa umbali wa miakanuru 780.

Kuna nyota badilifu kadhaa na pia nyota maradufu. T Coronae Borealis ni nyota dhaifu ambayo kwa kawaida ina mwangaza unaoonekana wa mag 10 pekee lakini imekuwa maarufu katika mwaka 1866 ilipowaka ghafla kufikia mwangaza wa mag 2 na kufifia tena. Kwa hiyo ilitambuliwa kuwa nyota nova lakini ni kati ya nyota chache zinazorudia tabia hii yaani mwaka 1946 ililipuka na kufifia tena. Kwa Kiingereza ilipewa pia jina la “Blaze Star”.

Kasi ya Masakini imetambuliwa pia kuwa na nyota zenye mifumo ya sayari.[7]

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Corona Borealis" katika lugha ya Kilatini ni "Coronae Borealis" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Coronae Borealis, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. tazama Lane, Arabic-English Lexicon, uk. 2442
  4. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  5. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
  6. Inatajwa kwa jina hili katika orodha ya Knappert, taz. chini
  7. Lee, B.-C.; Han, I.; Park, M.-G.; Mkrtichian, D. E.; Kim, K.-M. (2012). "A planetary companion around the K giant ɛ Corona Borealis". Astronomy & Astrophysics. 546: 5.

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 75 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
  • Lane, Edward William : An Arabic - English Lexicon by in eight parts – 1872 (Perseus Collection Arabic Materials Digitized Text Version v1.1 of reprint Beirut – Lebanon 1968) online hapa
  • Star Tales: Corona Borealis, tovuti ya Ian Ridpath
  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kasi ya Masakini (kundinyota) kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.