Hayya (kundinyota)
Hayya (kwa Kilatini na Kiingereza Serpens) [1]. ni jina la kundinyota kwenye angakaskazi ya Dunia yetu.
Mahali pake
Hayya - Serpens iko katika ukanda wa Njia Nyeupe.
Hili ni kundinyota la pekee linalopatikana angani kwa sehemu mbili za pekee zinazotengwa na kundinyota la Hawaa (Ophiuchus). Sehemu mbili zinaitwa Serpens Caput (kichwa cha Hayya au nyoka) upande wa magharibi na Serpens Cauda (Mkia wa Hayya au nyoka) upande wa mashariki. Katikati ya pande hizi mili iko Hayya au Ophiuchus anayetazamia kuwa anabeba nyoka.
Sehemu ya Kichwa cha Hayya (Serpens Caput) linapakana na makundinyota jirani ya Mizani (Libra), Mashuke (Virgo), Bakari (Bootes), Kasi ya Masakini (Corona Borealis), Hawaa (Ophiuchus) na Rakisi (Hercules).
Ng'ambo ya Hawaa ipo sehemu ya pili Mkia wa Hayya na hii linapakana na Mshale (pia Kausi na lat. Sagittarius), Ngao (Scutum), Ukabu (Aquila) na Hawaa (Ophiuchus).
Jina
Hayya (Kiarabu: حية ḥayya; Kilatini: Serpens) lilijulikana vile kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. [2].
Serpens - Hayya ni kati ya makundinyota yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika karne ya 2 BK. “Serpens” au Hayya inantaja nyoka mkubwa anayeshikwa na Hawaa (Ophiuchus). Katika mitholojia ya Kigiriki huyu alikuwa Asklepios, mungu wa tiba na nyoka ilikuwa ishara ya nguvu ya dawa linaloweza kuua na kupona.
Hayya iko pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa kimataifa wa astronomia [3] kwa jina la Serpens. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Ser'.[4]
Nyota
Hayya - Serpens ni kundinyota kubwa yenye nyota nyingi. Unukalhai au α Serpentis ni nyota angavu zaidi iliopo katika sehemu za Caput Serpentis. Ni jitu jekundu lenye mwangaza unaoonekana wa mag 2.6 ikiwa umbali wa mwakanuru 73 na Dunia[5][6].
Jina la (Bayer) |
Namba ya Flamsteed |
Jina (Ukia) |
Mwangaza unaoonekana |
Umbali (miakanuru) |
Aina ya spektra |
---|---|---|---|---|---|
α | 24 | Unukalhai, Unuk al Hay, Unuk, Cor Serpentis | 2,63m | 73 | K2 III |
η | 58 | 3,23m | 62 | K0 III-IV | |
μ | 32 | 3,54m | 156 | A0 V | |
ξ | 55 | 3,54m | 105 | F0 IIIp | |
β | 28 | Beta Serpentis au Chow | 3,65m | 153 | A3 V |
ε | 37 | 3,71m | 70 | A2 Vm | |
γ | 41 | 3,85m | 36 | F6 V | |
θ1,2 | 63 | Alya | 4,03m | 132 | A5 V |
Tanbihi
- ↑ Uhusika milikishi (en:genitive) ya "Serpens" katika lugha ya Kilatini ni "Serpentis" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Serpentis, nk.
- ↑ ling. Knappert 1993
- ↑ The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
- ↑ Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
- ↑ Serpens], tovuti ya Constellation Guide, iliangaliwa Oktoba 2017
- ↑ Unukalhai (Alpha Serpentis), Tovuti ya Prof. Jim Kaler
Viungo vya Nje
- Constellation Guide: Serpens constellation
- Serpens & Ophiuchus, "Stars", kwenye tovuti ya Prof Jim Kaler, University of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017
- Star Tales – Serpens, tovuti ya Ian Ridpath, iliangaliwa Oktoba 2017
- The Deep Photographic Guide to the Constellations: Serpens
Marejeo
- Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, “Argo Navis” ukurasa 63 ff (online hapa kwenye archive.org)
- Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331