Ellen Evangelistic Singers

Ellen Evangelistic Singers (kifupi: ELLES; kwa Kiswahili: Waimbaji wa Kiinjilisti wa Ellen) ni kwaya ya kanisa la Wasabato inayolenga kutoa huduma kwa jamii na kueneza Injili ndani na nje ya Tanzania.

Jina la kikundi

hariri

Ellen Evangelistic Singers ni kikundi cha familia ya Malangwa Buziku Ng’wengonogaga na Ellen Minza Kalabaga (marehemu wote), ambayo ilikuwa familia ya wakulima na wafugaji. Familia hii asili yao ni Bariadi, mkoa wa Simiyu, katika Mtaa wa Kanadi. Wengi wa wanafamilia wamezaliwa na kukulia Simiyu, ijapokuwa hawakuzaliwa katika imani ya Kiadventista. Imani ya Kiadventista waliipokea wakiwa katika umri mkubwa, ukiachilia mbali wajukuu na vitukuu vya familia hii. Mama yao (yaani, Ellen Minza) alibatizwa miaka ya 1990 na wakati anabatizwa alichagua jina jipya la ubatizo la Ellen, jina la mwinjilisti na nabii mashuhuri Ellen G. White. Hii ni kutokana na ukweli kwamba alipenda sana matendo ya kiinjilisti ya mama huyu. Kwa kifupi jina la Ellen katika kikundi hiki, ni jina la mama mzazi wa familia hii na ambalo pia lina uhusiano sana na jina la nabii na mwinjilisti Ellen G. White. Kwa hiyo, Huduma ya Uinjilisti ya Ellen inaweza kuhusishwa na watu hao wawili bila shaka yoyote.

Historia

hariri

Ellen Evangelistic Singers ni huduma za uinjilisti zinazotolewa na kikundi kinachojishungulisha na utoaji wa huduma za kijamii nchini Tanzania, uimbaji wa nyimbo za Injili pamoja na kuhubiri injili katika maeneo ambayo haijahubiriwa vizuri.

Kikundi cha ELLES kilianzishwa mwaka 2013 jijini Dar es Salaam, Tanzania. Huduma za kikundi hiki ambacho wanachama wake wengi ni ndugu wa familia moja, zilianzia pale ambapo maisha ya mama yao, Ellen Minza Kalabaga, yalipokoma. Katika uhai wake na katika maisha yake ya Kikristo, mama Ellen Minza alikuwa mkarimu sana na alifurahia kuwakaribisha na kuwahudumia wachungaji na wainjilisti wengi ambao walikuwa wakitembelea maeneo ya Bariadi kwa shughuli za kimisionari. Nyumba ya Ellen Minza katika kijiji cha Nyangokolwa, Wilaya ya Bariadi, ilikuwa kituo na kambi ya watumishi wa Mungu. Aidha, hata kabla ya kujiunga na kanisa la Waadventista wa Sabato, mama huyo alikuwa mji wa makimbilio kwa ndugu kutoka ukoo wake na ukoo wa mume wake.[1][2] Mama Ellen alipojiunga na Kanisa la Waadventista wa Sabato alipenda sana kuimba, kuinjilisha na kutoa huduma mbalimbali kanisani kama vile za ushemasi.[3] Kutokana na moyo wake wa kupenda kazi ya Mungu, alipofariki mwaka 2012 watoto wake waliamua kutumia rambirambi ya msiba wake kufanya uinjilisti katika eneo alilokuwa anaishi. Kupitia fedha hiyo familia hiyo ilifanikiwa kununua Biblia 100, vitabu vya Nyimbo za Kristo 100 na vitabu vya Roho ya Unabii (vya mafundisho ya Biblia) zaidi ya 500.[4] [5]

Baada ya kukamilisha ununuzi wa vitabu hivyo, mwaka 2013 waliwasiliana na uongozi wa wakati huo wa kanisa la Waadventista wa Sabato Mtaa wa Kanadi kwa ajili ya kwenda kuvigawa bure. Uongozi wa kanisa uliwashauri waendeshe mahubiri ya ndani (maarufu kama uamsho) kwa muda wa wiki moja na kama watatokea watu watakaoamini na kubatizwa au kuamini tu hao ndio wawagawie machapisho hayo. ELLES walikubaliana na ushauri huo. Katika mahubiri hayo ya wiki moja, jumla ya watu 98 walimpokea Yesu na kubatizwa.[6] Baada ya kuona matokeo haya makubwa, wakaamua kuendelea na kazi hii kwa kujiongezea malengo mengine.

Huduma za uinjilisti za ELLES

hariri

Matokeo ya uinjilisti wa wiki moja ya mwaka 2013 yaliwasisimua sana ELLES. Kanisa mahalia la Nyangokolwa Wilayani Bariadi pia likawaomba warudie kuendesha mahubiri kama hayo kwa wiki tatu mwaka uliofuata (yaani, 2014). Wazo hili walilipenda pia lakini changamoto ikawa watapata wapi hela za kufanya kazi hii kwa wiki tatu! Mungu aliwapatia njozi ya kuanza kudunduliza fedha kidogokidogo kutoka kwenye vyanzo vyao binafsi. Hivyo, mwaka 2014 walifanikiwa kuandaa Biblia 200, vitabu vya Nyimbo za Kristo 200 na vitabu vya mafundisho ya Biblia zaidi 500 na kuendesha mahubiri ya wiki 3 na watu zaidi ya 200 walimpokea Yesu na kubatizwa. Kuanzia hapo, wakawa kama wameonja asali. ELLES wakaamua kuendelea kutoa huduma mbalimbali za kiinjilisti kila mwaka kwa gharama zao pamoja na kuwashirikisha wadau mbalimbali. Huduma ambazo wamekuwa wakizitoa sambamba na kuhubiri injili kwa gharama zao wenyewe ni pamoja na:

  1. Kupima watu afya na kuwapatia huduma za ushauri wa kiafya bure
  2. Kutoa dawa bure kwa wagonjwa ambao wanawapima, zikiwamo dawa za malaria, minyoo, kisukari, presha na kadhalika
  3. Kutoa ushauri wa kifamilia kwa wanandoa, vijana na wajane
  4. Kuhubiri neno la Mungu kwa watoto, vijana na watu wazima
  5. Kununua maeneo na kujenga makanisa kwa ajili ya waumini wapya
  6. Kugawa Biblia na vitabu mbalimbali vya kuielimisha jamii bure
  7. Kugawa nguo na chakula bure kwa wahitaji
  8. Kutoa mafundisho ya ujasiriamali bure
  9. Kuimba, kurekodi na kusambaza CD, DVD na vinyonyi vyenye nyimbo mbalimbali
  10. Kutembelea shule mbalimbali kwa lengo la kugawa madaftari na kalamu pamoja na kuwahamasisha wanafunzi kuzingatia elimu na kujiepusha na ngono.

Malengo

hariri

Kikundi hicho kilianzishwa kwa malengo mahsusi yafuatayo:

  • Kutangaza injili nchini Tanzania, Afrika Mashariki na duniani kote kwa njia ya nyimbo, mahubiri na huduma za kijamii.
  • Kuielimisha jamii kupitia mafundisho mbalimbali kama vile masomo ya afya, mahusiano katika ndoa/familia, maisha ya vijana, ujasiriamali, nk.
  • Kugawa nguo na chakula bure kwa wahitaji wanaokutana nao katika kutekeleza majukumu yao ya kiinjlisti.
  • Kugawa bure machapisho mbalimbali ya kuwajenga watu kiroho, kiakili na kijamii.
  • Kurekodi nyimbo za injili katika muundo wa sauti na video na kuzisambaza kwa njia ya CD, DVD, vinyonyi, mtandaoni na katika vyombo mbalimbali vya habari kama redio na TV.
  • Kushiriki katika uimbaji kwenye mikutano ya injili, makongamano, semina, warasha, matamasha, n.k.
  • Kuanzisha kituo cha mawasiliano na kuwasaidia vijana na jamii kwa ujumla kurekodi nyimbo zao.
  • Kutoa huduma za ushauri kwa watu mbalimbali kulingana na changamoto za kijamii, kuwafariji watu wanaoonekana kupoteza matumaini au kukata tamaa, nk.
  • Kuanzisha shughuli mbalimbali za kiujasiriamali kwa ajili ya kupata fedha za kuendeleza shughuli za uinjilisti na kusaidia wahitaji au jamii kwa ujumla.
  • Kuwawezesha na kuwalea wanakikundi kiroho, kielimu, kimwili, kiuchumi, n.k.

Ubatizo na ujenzi wa makanisa

hariri

Katika kipindi cha miaka mitano tu (2013-2018), ELLES waliwaleta watu zaidi ya elfu mbili (2000) kwa Kristo kwa njia ya ubatizo. Ili kuhakikisha kwamba wale wanaobatizwa wanaendelea kupata huduma za kiroho vizuri, ELLES walisaidiana na wenyeji kununua maeneo na kuwajengea makanisa kwa ajili ya kuabudia. ELLES pia waliajiri wainjilisti walei kwa ajili ya kuwahudumia kiroho waumini hao wapya. Sambamba na hayo, katika makanisa hayo kukaanzishwa kwaya nzuri za kiinjili ambazo zinayahudumia makanisa hayo katika suala la uimbaji.

Huduma za kijamii

hariri

ELLES wanajihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii hasa katika maeneo ya vijijini. Kila mwaka wamekuwa wakifanya safari za kwenda katika vijiji mbalimbali vya Tanzania na kugawa vitabu bure kwa wananchi wengi wanaohitaji vitabu vizuri vya kujisomea. Tangu kikundi cha ELLES kianzishwe kwa kushirikana na wataalamu wa afya, wameendesha kampeni ya kupima afya za maelfu ya Watanzania vijijini ambako huduma za kijamii kama vile hospitali hazitoshelezi mahitaji yaliyopo. Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pia ELLES wamekuwa wakigawa nguo bure kwa familia zenye mahitaji.[7]

Nyimbo za Injili

hariri

ELLES wamekuwa na kikundi kikubwa cha uimbaji chenye waimbaji zaidi ya ishirini. ELLES wameweza kuimba na kurekodi nyimbo za injili zaidi ya hamsini (50). Nyimbo hizo wamezirekodi na kuziweka katika Santuri Sauti (CDs), Santuri Mwonekano (DVDs) na vinyonyi. Nyimbo zao pia zinapatikana YouTube kwenye channel yao inayoenda kwa jina la Ellen Singers katika [8], na zimekuwa na watazamaji wengi wanaofuatilia kila siku.

Lugha wanazotumia katika uimbaji

hariri

Kwa sasa lugha ambazo wamezitumia zaidi katika utunzi wa nyimbo zao ni Kiswahili na Kisukuma. Pamoja na kwamba Kiswahili ni lugha ya Taifa la Tanzania, Afrika Mashariki na watu wengi duniani, lakini mashabiki wa nyimbo za ELLES hupendelea sana kusikiliza na kufuatilia nyimbo za Kisukuma, kabila mojawapo la Tanzania. Katika matamasha mbalimbali na makongamano au mikutano ambayo ELLES hualikuwa kuimba, mashabiki hudai nyimbo za Kisukuma zirudiwe mara kadhaa. Baadhi ya nyimbo zinazotamba sana ni Kalugendo (Maarufu kama “Zigi”), Farao na Nzengo.[9]

Huduma nyingine za ELLES

hariri

Kuendesha masomo mbalimbali redioni, kwenye televisheni na YouTube. Kwa mfano, mwaka 2018 ELLES walirusha masomo mbashara katika redio ya Maisha FM, iliyopo Bunda mkoani Mara. ELLES pia wamefanya yafuatayo:

  • Kurusha matangazo pamoja na kuandaa makala maalum kupitia Morning Star Redio na TV ya Hope Chanel Tanzania na baadhi ya makala hizi zinapatikana katika Chaneli ya YouTube ya Ellen Singers.
  • Kuwa na mawasilisho maalum kwenye TV na Redio mbalimbali – kama vile TBC1, Chanel Ten, Hope Chanel Tanzania, Morning Star Redio, n.k. Mahojiano haya yamekuwa yakileta hamasa kwa familia na watu binafsi waweze kuiga kile kinachofanywa na ELLES.[10]
  • Kuwaunganisha wanafamilia na kuwaongoza katika kumjua Mungu. Baadhi ya wanafamilia wa ELLES ambao hawakuwa wanasali sasa wamemjua Mungu kupitia wenzao na wamebatizwa.

Vyanzo vya mapato

hariri

Baada ya ELLES kuamua kuendelea na utoaji wa huduma kama ilivyoelezwa hapo juu, waliamua kubuni na kusimamia miradi mbalimbali ambayo inaendelea kuwasaidia kuendesha shughuli zao kwa mafanikio. Miradi hiyo ni pamoja na biashara za maduka, usafiri wa umma na nyingine kadha wa kadha ambazo wanaendelea kubuni.[11] Wanakikundi pia wamekuwa wakielimishana kuhusu kuanzisha miradi binafsi na kuchangia katika maendeleo ya kikundi.

Marejeo

hariri
  1. Hesabu 35:5-6
  2. 1Nyakati 6:67
  3. 1Timotheo 3:8-10
  4. Tanzania SDA Media, 2020, pp.16
  5. https://www.youtube.com/channel/UCeucppjO2rhdIxXUFQOo-Tw
  6. https//www.jw.org/sw/mafundisho-biblia/ubatizo-ni-nini/
  7. Tanzania SDA Media, 2020, pp.16 Injilileo, 2017, Channel ya Hallelujah Family Choir, 2020
  8. https://www.youtube.com/channel/UCeucppjO2rhdIxXUFQOo-Tw
  9. https://www.youtube.com/channel/UCeucppjO2rhdIxXUFQOo-Tw
  10. https://www.youtube.com/channel/UCeucppjO2rhdIxXUFQOo-Tw
  11. Tanzania SDA Media, 2020, uk. 16.
  Makala hii kuhusu mambo ya muziki bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ellen Evangelistic Singers kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.