Force Publique
Force Publique ilikuwa jeshi la polisi la kikoloni katika Kongo ya Kibelgiji (leo: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) na pia Ruanda-Urundi (leo Rwanda na Burundi).
Jeshi na polisi ya kikoloni
haririIlianzishwa mwaka 1885 katika koloni ya Dola Huru la Kongo ikaendelea wakati wa ukoloni wa Ubelgiji na kubadilishwa jina kuwa jeshi la kitaifa la Kongo tangu uhuru.
Force Publique ilikuwa polisi na pia jeshi. Kazi yake ilikuwa kutunza utulivu na usalama lakini pia kukandamiza makabila yaliyopinga ukoloni na kuzuia au kuvunja upinzani wote dhidi ya sheria za kikoloni.
Michango katika Vita Kuu za Dunia
haririKatika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia jeshi hili lilishirikiana na Uingereza kuvamia Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (Tanganyika, Rwanda na Burundi).
Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia koloni ya Kongo ilikuwa sehemu ya "Ubelgiji huru" kwa sababu Ubelgiji yenyewe ilivamiwa na Ujerumani. Vikosi vya Force Publique vilishiriki na Uingereza katika vita dhidi ya Waaitalia katika Ethiopia. Askari wa Force Publique walihudumia pamoja na wanajeshi Waingereza katika Misri, Palestina, Somalia, Madagaska na Burma.
Wakati wa uhuru wa Kongo
haririWakati wa uhuru wa Kongo Wabelgiji hawakufanya juhudi kuwaandaa Waafrika kwa uongozi. Hadi mwisho Force Publique ilikuwa jeshi la askari Waafrika walioongozwa na maafisa wazungu. Mara baada ya uhuru uasi wa askari waafrika ulitokea walioshambulia maafisa wazungu na uasi ulikandamizwa na wanajeshi kutoka Ubelgiji.
Sasa serikali ya Patrice Lumumba alimpandisha sajenti Joseph Mobutu kuwa jenerali mkuu wa Force Publique lakini Mobuto alishirikiana na Wabelgiji kumwua Lumumba akawa dikteta wa kijeshi hadi mwaka 1997.
Nje ya Kongo
haririKatika nchi ndogo ya Monako jeshi lenye askari 250 linaitwa pia Force Publique.
Marejeo
hariri- Peter Abbott: Armies in East Africa 1914–18. Osprey 2002. ISBN 1-84176-489-2.
- Adam Hochschild: King Leopold's Ghost; A Story of Greed, Terror and Heroism in Colonial Africa, Houghton Mifflin Company 1998
- Louis-François Vanderstraeten, De la Force Publique à l'armée nationale congolaise : Histoire d'une mutinerie, Académie royale de Belgique, Brussels, Impression decidee le 18 avril 1983, 613 p. + pl. ISBN 2-8031-0050-9.
- Bryant Shaw, Force Publique, Force Unique: The Military in the Belgian Congo 1914-1939 Ph.D dissertation, University of Wisconsin, 1984
- 'Lisolo Na Bisu: Notre histoire: le soldat congolais de la FP 1885-1960,' Royal Museum of the Armed Forces and of Military History, Brussels, Belgium, ISBN 2-87051-049-7, 2010