Kanisa la Moravian Kusini Magharibi Tanzania

Kanisa la Moravian Kusini Magharibi Tanzania (KMKMT) (kwa Kiingereza: Moravian Church in Tanzania - South West Province MCTSWP) ni jimbo la Kanisa la Moravian Tanzania hasa katika wilaya za Mbeya, Mbozi, Chunya na Mbarali wa mikoa ya Mbeya na Songwe. Pia shirika mpya za Moravian kaskazini mwa Tanzania ziko chini ya jimbo hili ambazo ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dodoma na Manyara.

Historia

hariri

Jimbo hili lilianza rasmi tarehe 18 Desemba 1976 kutokana na kuongezeka kwa shirika na kazi ya uenezi wa Injili. Kabla ya kuanza kwa Jimbo hili Wamoravian wa Mbeya, Chunya, Mbozi , Mbarali walikuwa wakihudumiwa na Jimbo la Kusini lenye makao yake makuu Rungwe. Jimbo la Kusini Magharibi Makao yake makuu yako Mbeya.

Viongozi wa kwanza wa Jimbo hili waliochaguliwa mwaka huohuo 1976 walikuwa Mchungaji Tulinawo Msinjili - Mwenyekiti, Mchungaji Yohana Wavenza - Makamu wa Mwenyekiti na Mchungaji Hezron Mwalupembe - Katibu Mkuu. Wajumbe wa Halmashauri Kuu wa Kwanza walikuwa ni Mwinjilisti L. Sikana, Mchungaji Tenson Sikaponda, Mchungaji Philip Cheyo, Ndugu Zebedayo Mkisi na Ndugu Yoram Mtemi.

Askofu wa kwanza Yohana Wavenza aliwekwa wakfu kuwa askofu wa jimbo hili tarehe 24 Julai 1983. Askofu wa pili wa Jimbo hili Alinikisa Cheyo aliwekwa wakfu tarehe 12 Agosti 2001 katika uwanja wa mpira Sokoine Mbeya.

Utawala

hariri

Kama majimbo yote ya kanisa la Moravian, jimbo hili linaongozwa na Kamati ya Utendaji inayochaguliwa na sinodi ya kanisa. Watendaji wakuu ni mwenyekiti, makamu wake na katibu mkuu. Wanatoa taarifa kwa halmashauri kuu inayochaguliwa pia na sinodi ikikutana kati ya mikutano ya ile bodi kuu. Watendaji wakuu wanasaidiana na makatibu wa idara mbalimbali wanaoteuliwa na halmashauri ya kanisa.

Jimbo hili tangu mwaka 2008 linaongozwa na watendaji wafuatao: Mchungaji Nosigwe Buya - Mwenyekiti, Mchungaji Zakaria Sichone - Makamu Mwenyekiti na Mchungaji Daudi Nsweve Katibu Mkuu.

Pamoja na kazi ndani ya kanisa kama vile Vijana, Wanawake, Elimu ya Kikristo, jimbo hili lina miradi na huduma zifuatazo:

  • Taasisi za Elimu[1]: Chuo cha Mafunzo ya Ufundi cha Moravian - MVTC (Mbeya mjini), Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Chunya, Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Ilindi, Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Sadock Simwanza Tunduma), Shule ya Sekondari ya Mbozi, Chuo cha Ualimu Mbeya Moravian, Chuo cha Theolojia Utengule, Taasisi ya Afya Yohana Wavenza - Yohana Wavenza Health Institute
  • Taasisi za Afya[2]: Hospitali ya Misheni ya Mbozi, Kituo cha afya cha Nkanga, Zahanati ya Kapele, Zahanati ya Iyendwe
  • Miradi ya kijamii[3]: Mradi wa Watoto Yatima na wenye maisha magumu - Nsalaga, Dawati la VVU, Idara ya Gereza na Hospitali
  • Miradi mingine kama vile Kituo cha Baraka FM Redio na Studio, Msaada wa Kisheria (hasa kwa wanawake mkoani Songwe), Hosteli ya Vijana wa Moravian Mbeya, Moravian SACCOS

Tanbihi

hariri

Viungo vya Nje

hariri