King's African Rifles

(Elekezwa kutoka King`s African Rifles)

King's African Rifles (kifupi KAR, pia huitwa Askari Kea) ilikuwa jeshi la kikoloni la Uingereza katika Afrika ya Mashariki kati ya mwaka 1902 hadi uhuru wa mataifa ya Kiafrika. Vikosi vyake vilianzishwa Kenya na kupanuka baadaye hadi koloni kwenye maeneo ya Uganda, Tanzania, na Malawi ya leo.

Baada ya uhuru vikosi vya KAR katika kila koloni vilikuwa jeshi la nchi huru vikaendelea mwanzoni kwa majina kama Uganda Rifles, Kenya Rifles. Tanganyika Rifles na Malawi Rifles.

Kikosi cha KAR huko Kenya mwaka 1902

Kuanzishwa kwa KAR

hariri

Lilianzishwa mnamo 1902 kutoka vikosi vya askari Waafrika kwenye utumishi wa kikoloni katika Afrika ya Mashariki ya Kiingereza (baadaye Kenya), Uganda na Unyasa (leo Malawi). Shabaha ilikuwa kusanifisha mafunzo na kazi ya askari hao na kuweka msingi kwa ushirikiano wao. Vikosi vya KRA vilifanywa na askari Waafrika chini ya amri ya maafisa Wazungu.

Mwanzoni kulikuwa na batalioni 6

  • 1st (Nyasaland) Battalion [1902–1964]
  • 2nd (Nyasaland) Battalion [1902–1963]

Batalioni katika Unyasa ziliitwa pia vikosi vya Afrika ya Kati (Central African Battalions)

  • 3rd (Kenya) Battalion [1902–1963]
  • 4th (Uganda) Battalion [1902–1962]
  • 5th (Uganda) Battalion [1902–1904]—the Senior Battalion as it was the first to be raised.
  • 6th (Somaliland) Battalion [1902–1910] ikahudumia katika Somalia ya Kiingereza

Jumla walikuwa mwaka 1902 Wazungu 104 na Waafrika 4,579. Idadi ya vikosi ilipungukiwa baadaye kwa sababu walowezi Waingereza katika Kenya walipinga kuwepo kwa jeshi kubwa la Waafrika wenye elimu ya kutumia silaha za kisasa.

KAR katika Vita Kuu ya Kwanza

hariri

Mnamo mwaka 1914 KAR ilikuwa na batalioni 3 zilizogawiwa kwa kombania ndogo 21. Jumla walikuwepo maafisa Waingereza 70 na askari Waafrika 2335. Waafrika waliweza kupanda cheo hadi sajanti meja.

Katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia idadi ya askari wa KAR iliongezeka hadi kufikia Waafrika 30,658 na maafisa Wazungu 2,700. Mwanzoni wa vita Uingereza ilitegemea zaidi askari Wahindi walioshindwa mara kadhaa na Jeshi la Ulinzi la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani lililotegemea zaidi askari Waafrika. Baada ya kubadilisha mfumo kwa kutumia askari Wazungu kutoka Afrika Kusini maendeleo hayakuridhisha dhidi jeshi la Kijerumani hadi Waingereza waliamua kutumia hasa Waafrika wa KAR waliofaulu kuwalazimisha upande wa Kijerumani kukimbia Msumbiji.

Baada ya Vita Kuu ya Kwanza idadi ya askari ilipunguzwa tena na kwa jumla walipangwa kwa brigedi mbili za kaskazini na kusini. Eneolao lilijumlisha sasa pia Tanganyika jinsi eneo la Kijerumani la awali likaitwa sasa.

 
Askari wa KAR wanakusanya silaha ya Waitalia walioshindwa huko Ethiopia mwaka 1941

Vita Kuu ya Pili

hariri

Baada ya kuanzishwa kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia koloni ya Uingereza ilipakana na eneo la adui iliyokuwa Italia katika Somalia na Ethiopia. Idadi ya askari iliongezeka tena na mnamo 1940 walifikia Waafrika 20,000 na Wazungu mnamo 2450, kati yao maafisa 883. [1]

Vikosi vya KAR vilipigania Waitalia katika Somalia na Ethiopia, dhidi jeshi la Ufaransa- Vichy huko Madagaska na la Japani katika Burma.

 
Kikosi cha KAR huko Burma wakati wa Vita Kuu II

Baada ya vita vikosi vya KAR vilipunguzwa tena maana pasipo na vita jeshi hili liligharamiwa kutokana na mapato ya kila koloni. Upande wa Tanganyika vilibaki vikosi viwili tu, kimoja kwenye kambi la Kolito (Colito Barracks) mjini Dar es Salaam na nyingine kwenye kambi la Kalewa (Kalewa Barracks) huko Tabora. Jina la "Colito" lilitunza kumbukubu ya ushindi wa kikosi kutoka Tanganyika juu ya Waitalia katika mapigano ya Alaba Kulito pale Ethiopia tarehe 19 Mei 1941.[2] Jina la "Kalewa" ni makumbusho ya mapigano ya Kalewa huko Burma kwenye Desemba 1944 ambako vikosi kutoka Afrika ya Mashariki vilivuka mto Chindwin katika vita dhidi ya Japani[3].

Baada ya Vita Kuu hadi Uhuru

hariri

Askari Waafrika waliona sehemu kubwa za dunia. Hasa huko Kenya askari wa awali wa KAR walijiunga baadaye na harakati ya Mau Mau na kutumia elimu yao ya vita dhidi ya wakoloni na Waafrika wenzao walioshirikiana na Waingereza.

Baada ya Vita Kuu KAR ilitumiwa na Uingereza kupigania vita za wenyewe kwa wenyewe huko Kenya dhidi wapiganaji wa Mau Mau na pia katika Shirikisho la Malay (leo: Malaysia).

Kuanzia 1961 nchi za Afrika ya Mashariki zilianza kupata uhuru. KAR ilivunjika kieneo na kuwa chanzo cha jeshi za kitaifa katika kila nchi:

Tanganyika rifles zilivunjwa baada ya uasi wa mwaka 1964. Huko Kenya na Malawi majina ya "Kenya Rifles" na "Malawi Rifles" hutumiwa hadi leo kwa sehemu za jeshi la kitaifa.

Marejeo

hariri
  1. The King's African Rifles - Volume 2, by Lieutenant-Colonel H. Moyse-Bartlett, p. 479 (google books, ilitazamiwa Juni 2015)
  2. "Kuhusu sajenti Leakey aliyekufa siku ile katika mapigano". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2018-07-06. Iliwekwa mnamo 2018-06-13.
  3. John Grehan, Martin Mac: The Battle for Burma 1943-1945: From Kohima & Imphal Through to Victory, kupitia google books, ilitazamiwa Juni 2018