Somalia ya Kiingereza

Somalia ya Kiingereza (kwa Kiingereza: British Somali Coast Protectorate; kifupi: Somaliland) ilikuwa eneo lindwa la Uingereza katika Somalia ya Kaskazini.

Mahali pa Somalia ya Kiingereza.

Eneo lake lilikuwa tangu 1961 sehemu ya Jamhuri ya Somalia na tangu 1991 limekuwa kwa kiasi kikubwa Jamhuri ya Somaliland, nchi isiyotambuliwa na umma wa kimataifa lakini yenye tabia zote za nchi huru.

HistoriaEdit

Koloni mwaka 1884/1885Edit

Uingereza uliingia katika eneo hili baada ya Misri kuondoka mwaka 1885 kwa kushindwa na jeshi la Mahdi huko Sudan. Uingereza uliingia kwa sababu iliona umuhimu wa kutawala pande zote mbili za Bab el Mandeb ikihofia uenezaji wa nchi nyingine za Ulaya, hasa Ufaransa iliyokuwa na koloni la kwanza ya Ubuk (Obok) katika Jibuti ya leo tangu 1862. Pamoja na hayo Waingereza walitegemea kununua nyama kwa ajili ya mji wa Aden na meli zilizopita hapo kati ya Uhindi na Ulaya.

Somaliland ilitawaliwa awali kama mkoa wa Uhindi wa Kiingereza ikawa baadaye chini ya wizara ya makoloni huko London.

Upinzani wa Diiriye GuureEdit

Hata kama Uingereza haukuwa na nia ya kuingilia mno maisha ya wenyeji ulikutana na upinzani mkali kuanzia mwaka 1899 kutoka kwa kiongozi wa dini Diiriye Guure, aliyeitwa na Waingereza "Mullah majununi". Waingereza walijibu kwa ukatili katika vita vya miaka 20 iliyoua takriban theluthi moja ya wakazi wote wa eneo.

Mwishowe Uingereza iliweza kumaliza upinzani kwa teknolojia mpya ya eropleni za kijeshi zilizotumia mabomu na bunduki za mtombo kutoka angani kwa mara ya kwanza katika Afrika.

Vita Kuu ya Pili ya DuniaEdit

Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia eneo likatwaliwa na Italia katika Agosti 1940 lakini lilichukuliwa tena na Uingereza katika Machi 1941.

Uhuru na muunganoEdit

Uhuru ulipatikana tarehe 26 Juni 1960, lakini tarehe 1 Julai kulitokea muungano na Somalia ya Kiitalia iliyokuwa imepata uhuru wake pia.

Nchi ya pekeeEdit

Baada ya kuporomoka kwa serikali ya Somalia, sehemu kubwa ya eneo la Somalia ya Kiingereza la awali ikatangaza uhuru wake mnamo 18 Mei 1991 kama Jamhuri ya Somaliland.

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Somalia ya Kiingereza kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.