Shaliaki (kundinyota)

(Elekezwa kutoka Kinubi (kundinyota))

Kwa maana mengine ya jina hili angalia hapa Kinubi

Nyota za kundinyota Shaliaki (Lyra) katika sehemu yao ya angani

Shaliaki (kwa Kilatini na Kiingereza Lyra) [1] ni jina la kundinyota kwenye angakaskazi ya Dunia yetu. Nyota ya Vega ambayo ni kati ya nyota angavu zaidi kwenye anga ya usiku lipo katika Shaliaki na hii ni nyota moja ya Pembetatu ya Kiangazi kwenye nusutufe ya Kaskazini.

Jina

Shaliaki (Lyra) ilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. Walitumia jina la Shaliaki kutokana na Kiarabu شلیاق shalyak inayomaanisha ala ya muziki kama kinubi[2].

Lyra - Shaliaki ni kati ya makundinyota yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika karne ya 2 BK. Lipo pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [3] kwa jina la Lyra. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Lyr'.[4]


“Lyra” au Shaliaki katika mitholojia ya Kigiriki inarejelea habari za mwimbaji Orfeo aliyetumia ala hii ya muziki mara ya kwanza na kwa muziki yake aliweza kufanya hata miti na mawe kucheza na kubadilisha mwendo wa mito. Mke wake alipokufa Orfeo aliingia kuzimuni akamshawishi Hades mungu wa mauti kwa nguvu ya muziki kumruhusu arudishe mke wake katika dunia ya wenye uhai.

Mahali pake

Shaliaki - Lyra inapakana na makundinyota jirani ya Mbweha (Vulpecula), Rakisi (Hercules), Tinini (Draco) na Dajaja (Cygnus).


Nyota

Vega au α Lyrae ni nyota angavu zaidi. Ina mwangaza unaoonekana wa mag 0.03 ikiwa na umbali wa miakanuru 25.3 na Dunia[5][6].

Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miakanuru)
Aina ya spektra
α 3 Vega 0,03m 25,3 A0 V
γ 14 Sulafat 3,24m 635 B9 III
β 10 Sheliak 3,25 bis 4,36m 882 A8
13 R 3,9 bis 5,0m 350 M5 III
δ2 12 4,22m 899 M4 II
ζ1 6 4,34m 154 Am
κ 1 4,33m 238 K2 III
θ 21 4,34m 769 K0 III
η 20 Aladfar 4,43m 1042 B2 IV

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya "Lyra" katika lugha ya Kilatini ni "" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Lyrae, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  4. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R. 
  5. Lyra], tovuti ya Constellation Guide, iliangaliwa Oktoba 2017
  6. Vega (Alpha Lyrae), Tovuti ya Prof. Jim Kaler

Viungo vya Nje

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, “Argo Navis” ukurasa 374 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331