Dajaja (kundinyota)
Dajaja (kwa Kilatini na Kiingereza Cygnus) [1] ni jina la kundinyota kwenye angakaskazi ya Dunia yetu. Humo ipo Dhanabu ya Dajaja (Deneb)[2] ambayo ni kati ya nyota angavu zaidi kwenye anga ya usiku na hii ni nyota moja ya Pembetatu ya Kiangazi kwenye angakaskazi.
Nyota za α - β na ε - δ zimelinganishwa na umbo la msalaba na hivyo zinaitwa pia "Salibu ya Kaskazini".
Jina
Dajaja (Cygnus) ilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu wanaosema الدجاجة ad-dajaaja wakimtaja ndege wa aina ya kuku. [3]. Waarabu walipokea jina hili kutoka kwa Ptolemaio aliyeiita Ορνις ornis yaani ndege au kuku[4]. Wagiriki wa Kale kwa jumla waliona hapa ndege waliotaja kwa majina tofauti[5] .
Katika mapokeo ya baadaye hasa wakati wa Kiroma ndege ilichukuliwa kumaanisha bata-maji au “kyknos” (lat. Cygnus) iliyounganishwa na ndege huyu wa angani kati ya Wagiriki na Waroma wa Kale. Katika mitholojia ya Kigiriki "kyknos"inaweza kurejelea masimulizi ya mungu mkuu Zeus aliyechukua umbo la bata maji akitembea duniani na kutafuta mapenzi na mabinti wa kibinadamu[6]. Kwa mapokeo tofauti jina la “kyknos” linarejelea masimulizi ya mungu Phaeton aliyekuwa mwana wa Helios mungu wa jua. Phaeton aliwahi kuendesha gari la jua la babaye angani kwa kasi kubwa mno akasababisha hatari ya kuchomwa kwa mbingu na Dunia. Hapo baba wa miungu Zeus alipaswa kurusha radi dhidi ya gari la jua na kumwua Phaeton. Phaeton akaanguka chini katika mto Nahari (Eridanus) na kwa muda mrefu rafiki yake Kyknos alitafuta mifupa yake katika vilindi vya mto ili aweze kumpatia mazishi halisi. Miugu kwa jumla waliguswa na upendo alionyesha wakamgeuza kuwa kyknos = bata-maji na kumweka angani kati ya nyota. Kwa hiyo Waarabu walitumia hapa jina la kale zaidi la Wagiriki kwa kundinyota hili. Katika mapokeo ya kimagharibi kuna pia mifano ambako “Gallina” (=Kuku) ilitumiwa badala ya Cygnus hadi karne ya 18.[7].
Cygnus - Dajaja ni kati ya makundinyota yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio (kwake kama ornis - ndege) katika karne ya 2 BK. Iko pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [8] kwa jina la Cygnus. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Cyg'.[9]
Mahali pake
Dajaja - Cygnus inaonekana katika kanda ya Njia Nyeupe. Inapakana na kundinyota jirani za Kifausi (Cepheus), Tinini (Draco), Kinubi (Lyra), Farasi (Pegasus), Mjusi (Lacerta) na Mbweha (Vulpecula)
Nyota
Dhanabu ya Dajaja[10] au α Cygni (Deneb) ni nyota angavu zaidi. Ina mwangaza unaoonekana wa mag 1.25; umbali wake na Dunia bado unajadiliwa kuna makadirio kati ya miakanuru 1,425 hadi 3,200[11][12].
Jina la (Bayer) |
Namba ya Flamsteed |
Jina (Ukia) |
Mwangaza unaoonekana |
Umbali (miakanuru) |
Aina ya spektra |
---|---|---|---|---|---|
α | 50 | Deneb (Dhanabu ya Dajaja) | 1,25m | 3200 | A2 Ia |
γ | 37 | Sadr | 2,23m | 750 | F8 |
ε | 53 | Gienah | 2,48m | 72 | K0 III |
β | 6 | Albireo | 2,9m | 385 | K2 + B9 V |
δ | 18 | 2,86m | 150 | B9 + F1 | |
34 | 3,0 bis 6,0m | 5000 | B2 Ia | ||
ζ | 64 | 3,21m | 200 | G8 III | |
χ | 3,62 bis 15,0m | 345 | K0 III | ||
ξ | 62 | 3,72m | 1000 | K5 Ib | |
τ | 65 | 3,74m | 70 | F1 IV | |
ι | 10 | 3,76m | 100 | A5 V | |
κ | 1 | 3,80m | 150 | K0 III | |
ο1 | 31 | 3,80m | 500 | K2 + B6 | |
η | 21 | 3,89m | 200 | K0 III | |
ν | 58 | 3,94m | 150 | A0 V | |
ο2 | 32 | 3,96m | 1000 | K3 ib | |
ρ | 73 | 3,98m | 200 | G8 III | |
41 | 4,01m | 500 | F5 II | ||
61 | 61 Cygni | 4.8m | 11.4 | K5 + K7 | |
Tanbihi
- ↑ Uhusika milikishi (en:genitive) ya "Cygnus" katika lugha ya Kilatini ni "Cygni" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Cygni, nk.
- ↑ Naming Stars, tovuti ya Umoja wa Kimataifa ya Astronomia, iliangaliwa Oktoba 2017
- ↑ ling. Knappert 1993
- ↑ Kwa Kigiriki cha Kale neno Ορνις ornis iliweza kumaanisha ndege kwa jumla au pia kuku kwa maana ya pekee. Linganisha Paul Kunitzsch, Almagest uk.179
- ↑ Allen uk 192 anataja Ornis kama jina la kawaida; ni Eratosthenes aliyewahi kutumia jina “kyknos”. Allen anaona Wagiriki walipokea kundinyota hili kutoka kwa Wababeli bila kukumbuka hao walimaanisha ndege gani.
- ↑ Linganisha mitholojia la kundinyota Jauza!
- ↑ Allen uk. 194
- ↑ The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
- ↑ Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
- ↑ Knappert anataja hapa "Dhanabu ya Ukabu" (Mkia wa Tai); lakini hii ni jina la ε na ζ Aquilae (Allen uk. 61), angalia pia Kaler; α Cygni inatajwa kwa Allen uk. 195 kuwa "Al Dhanab al Dajajah", linganisha pia tafsiri za Kiarabu za Almagesti ya Klaudio Ptolemaio zinazotumia "dajajah", Kunitzsch uk.179 na "PAL-Glossary" ya mradi wa Ptolemaeus Arabus et Latinus (tafuta "Cyg")
- ↑ Cygnus], tovuti ya Constellation Guide, iliangaliwa Oktoba 2017
- ↑ Deneb (Alpha Cygni), tovuti ya Prof. Jim Kaler
Viungo vya Nje
- Constellation Guide: Cygnus constellation
- Cygnus, "Stars" Ilihifadhiwa 2 Novemba 2017 kwenye Wayback Machine., kwenye tovuti ya Prof Jim Kaler, University of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017
- Star Tales – Cygnus, tovuti ya Ian Ridpath, iliangaliwa Oktoba 2017
- The Deep Photographic Guide to the Constellations: Cygnus
Marejeo
- Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, “Argo Navis” ukurasa 374 ff (online hapa kwenye archive.org)
- Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
- Paul Kunitzsch: Der Almagest: die Syntaxis mathematica des Claudius Ptolemäus in arab. -latein. Überlieferung, Otto Harrassowitz Verlag, 1974, kisehemu online hapa kwa google books, uk. 179
- PAL - Glossary, tovuti ya mradi wa "Ptolemaeus Arabus et Latinus (PAL)" wa Bavarian Academy of Sciences and Humanities, iliangaliwa Oktoba 2017