Nyotamkia
Nyotamkia (kometi, pia nyota msafiri, shihabu, Kiing. comet)[1] ni gimba dogo la angani linalozunguka Jua kwa njia ya duaradufu yenye sehemu kubwa mbali na Jua na sehemu ndogo karibu na Jua. Pale inapokaribia Jua inaotesha "mkia" unaoipa jina lake la "nyota yenye mkia". Mkia huu ni hasa mvuke unaong'aa kutokana na nuru inayoakisiwa.
Mwili wa nyotamkia ni mchanganyiko wa mawe, vumbi na barafu. Nyotamkia hutokea katika sehemu za mbali za mfumo wa Jua, ng'ambo ya obiti ya Uranus, katika Wingu la Oort. Ukubwa hauzidi kipenyo cha kilomita kadhaa zikiwa na maumbo tofauti tofauti. Muda mwingi nyotamkia iko mbali na Jua pengine haionekani kwa darubini. Ikifuata njia ya mzunguko na kukaribia Jua kiasi cha kutosha inaanza kuonekana kama nyota ikiakisi nuru ya Jua. Ikikaribia Jua zaidi sehemu ya barafu yake inaanza kuyeyuka kuwa mvuke na mvuke huu ni kama angahewa ya muda. Sehemu nyingine ya mvuke huachana na nyotamkia yenyewe na kuonekana kama "mkia". Mkia huu unaelekea kila wakati upande usio wa Jua kwa sababu upepo wa Jua unasukuma mvuke upande ule.
Kati ya nyotamkia ni chache tu zinazokaribia kiasi cha kutosha hadi zinaonekana kuwa na mkia kwa macho tu kwa muda wa wiki hadi miezi kadhaa. Zamani ziliaminiwa kuwa ishara kutoka mbinguni au kutoka kwa Mungu zikisababisha wasiwasi na hofu.
Historia
Kataka tamaduni nyingi za dunia Nyotamkia zilitazamiwa kama tukio nje ya utaratibu wa kawaida na hivyo kama ishara ya balaa fulani inayokaribia. Tangu karne ya 16 Nyotamkia zimetambuliwa kuwa magimba yanayorudi baada ya muda fulani. Mara ya kwanza nyotamkia ya Halley ilitambuliwa na Mwingereza Edmond Halley mwaka 1705 ya kuwa inarudi. Halley alitambua ya kwamba nyotamkia aliyoiona mwaka 1705 ilikuwa ileile iliyowahi kuonekana mwaka 1682. Alitabiri ya kwamba nyotamkia hii itaonekana tena mwaka 1759 ikawa hivyo. Nyotamkia hii iliyopewa jina la "Halley" imeendelea kurudi kila baada ya miaka 76. Wanahistoria waliweza kuthibitisha ya kwamba taarifa mbalimbali katika historia kuhusu nyotamkia tangu mwaka 240 BK ziliihusu "Halley". Ilipoonekana mwaka 1985/1986 nuru yake ilikuwa imepungua kulingana na ziara za awali kutokana na kupungua kwa maada yake iliyopotea katika "mkia".
Leo kuna nyotamkia takriban 170 zilizothibitishwa ya kuwa zimerudi. Kuna pia nyotamkia chache zilizoonekana kwa darubini jinsi zilivyopasuka na kuisha wakati wa kupita karibu na Jua.
Kutokana na habari hizo zote wataalamu hufikiri ya kwamba kuna nyotamkia nyingi katika mfumo wa Jua letu lakini idadi inaendelea kupungua polepole zikikwisha kutokana na kupungua kwa maada au kukaribia mno Jua au hata kugongana na magimba mengine. Haiwezekani kujua idadi kwa sababu muda wa kuzunguka Jua ambao ni sawa na muda wa kuonekana tena unaweza kuwa miaka mamia, hivyo nyingine hazikuonekana bado tangu mwanzo wa astronomia ya kisayansi.
Maendeleo ya utafiti
Tarehe 11 Novemba 2014 kifaa cha kutua(lander) ya chomboanga Rosetta ilitua juu ya nyotamkia Churyumov–Gerasimenko baada ya safari ya miaka 10 (zaidi ya kilometa bilioni 6). Ndiyo mara ya kwanza ya chombo kilichotengenezwa na binadamu kutua juu ya nyotamkia yoyote.
Hatua hiyo itawezesha kuelewa zaidi hulka na historia ya ulimwengu.
Tazama pia
Tanbihi
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Nyotamkia kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |