Kiingereza
Kiingereza ni lugha ya jamii ya Kijerumaniki cha Magharibi iliyokua nchini Uingereza kwa muda wa miaka 1,400.
Leo, zaidi ya wasemaji milioni mia nne duniani wanazumgumza Kiingereza kama lugha ya kwanza. Watu wengi zaidi wanazumgumza Kiingereza kama lugha ya pili, kwa sababu ni muhimu sana kwenye nyanja za mawasiliano, sayansi na uchumi wa kimataifa.
Historia ya Kiingereza
haririMwanzo wa lugha
haririLugha ya Kiingereza ilianzia huko Uingereza kutokana na kuingiliana kwa lugha mbalimbali, hasa lugha za kale za Ujerumani, Denmark na Ufaransa.
Sehemu ya kusini ya kisiwa cha Britania ilikuwa ndani ya Dola la Roma hadi mwanzo wa karne ya 5. Wenyeji walitumia lugha ya Kikelti pamoja na Kilatini cha Waroma, hasa mjini.
Uvamizi wa Waanglia-Saksoni: kuja kwa Kigermanik
haririBaada ya Waroma makabila kutoka Ujerumani ya kaskazini na Denmark walianza kuvamia kisiwa hicho. Katika mwendo wa karne mbili waliteka sehemu kubwa ya Uingereza ya leo isipokuwa sehemu za magharibi kama vile Cornwall na Wales na sehemu za kaskazini walipoishi Waskoti.
Wavamizi walileta lugha zao za Kisaksoni na Kianglia (Ujerumani ya Kaskazini) zilizounganika kuwa lugha ya Kiingereza cha Kale ambacho kilikuwa karibu sana na Kijerumani cha Kale. Inaonekana ya kwamba wenyeji Wakelti walio wengi walianza polepole kutumia lugha ya watawala wapya[1], wengine waliuawa au walihamia sehemu zisizo chini ya Waanglia-Saksoni.
Lugha hii iliathiriwa mara mbili. Kwanza Wadenmark ndio waliojaribu kujenga ufalme wao kisiwani. Waliteka sehemu za Uingereza ya Magharibi. Kiasi cha maneno kutoka lugha yao kimeingia Kiingereza cha kale kama Wales.
Mwaka 1066 jeshi la Wanormani kutoka Ufaransa ya Kaskazini walivamia na kuteka Uingereza. Wanormani walikuwa wa asili ya Skandinavia lakini walikuwa wameshaanza kutumia lugha ya Kifaransa cha kale. Wanajeshi hao walikuwa mabwana wapya wa Uingereza wakitumia Kifaransa chao.
Kwa karne kadhaa lugha mbili zilitumika kandokando: Kiingereza cha Kianglia-Saksoni cha watu wa kawaida na kile Kifaransa cha Kinormandy cha tabaka la watawala. Kwa jumla watawala walianza kutumia lugha ya raia lakini lugha hii ilibadilika pia kwa kupokea maneno mengi kutoka Kifaransa. Kuna makadirio ya kwamba zaidi ya theluthi moja ya maneno yote ya Kiingereza yana asili ya Kifaransa.
Kuingiliana kwa lugha zote mbili: Kiingereza cha Kati
haririKipindi hiki cha kuingiliana kati ya Kifaransa cha mabwana na lugha ya kawaida kilileta Kiingereza cha Kati. Hadi leo asili ya maneno kutoka Kijerumani na Kifaransa ni wazi kabisa.
Mfano mzuri ni maneno tofauti kwa wanyama kadhaa na nyama yao: ng'ombe huitwa "cow" (sawa na Kijerumani wa Kaskazini "Kau") lakini nyama yake ni "beef" (kutokana na neno la Kifaransa kwa ng'ombe "boeuf"); vilevile "sheep" kwa mnyama kondoo na "mutton" kwa nyama yake (Kijerumani ya Kaskazini: "Schaap" - Kifaransa: "mutton"), vilevile swine=mnyama – pork=nyama (nguruwe) na calf=mnyama – veal=nyama (ndama).
Wakulima wafugaji walitumia lugha yao kwa mnyama - mabwana wasiogusa mnyama lakini hula nyama yake waliendelea kutumia neno la Kifaransa kwa ajili ya mnyama yuleyule. Maneno yote mawili yaliingia katika Kiingereza cha Kisasa lakini kwa mambo mawili tofauti.
Kiingereza cha Kisasa
haririKiingereza cha Kisasa kimeanza na tafsiri ya Biblia ya William Tyndale; baadaye na washairi muhimu kama William Shakespeare.
Teknolojia ya uchapaji vitabu ilisambaza lugha hii nchini kote na kupunguza athira ya lahaja mbalimbali.
Wakati ule Kiingereza kilipokea pia maneno mengi kutoka lugha za Kilatini na Kigiriki zilizokuwa lugha za taaluma na sayansi hadi karne ya 18 kote Ulaya.
Kiingereza cha Kisasa kimeendelea kurahisisha lugha. Lakini urekebisho wa tahajia umeshindikana hadi leo hata kama kulikuwa na majaribio mbalimbali. Kutokana na historia yake Kiingereza kimebaki na tahajia isiyolingana na matamshi ya maneno.
Mwandishi George Bernhard Shaw alionyesha tatizo hilo kwa pendekezo la dhihaka kwamba neno "fish" (samaki) liandikwe "ghoti": gh kama sauti ya "f" katika "cough", o kama sauti ya "i" katika "women", na ti kama sauti ya "sh" katika "nation".
Pamoja na hayo, lahaja za Kiingereza zinazidi kutofautiana, zile muhimu zaidi zikiwa zile za Britania na Marekani.
Uenezi wa Kiingereza duniani
haririPamoja na Dola la Uingereza na makoloni yake, lugha ilienea duniani kati ya karne ya 17 na 19.
Tangu karne ya 19 idadi kubwa ya wasemaji wa Kiingereza hawaishi tena Uingerezea bali Marekani. Katika karne ileile Kiingereza kilikuwa lugha ya utawala katika maeneo makubwa ya makoloni ya Dola la Uingereza.
Baada ya makoloni kuwa nchi huru mara nyingi Kiingereza kimeendelea kuwa lugha rasmi za nchi hizo.
Kutokana na matukio hayo yote, na Marekani kujitokeza katikati ya karne ya 20 kama nchi tawala kisiasa, kiuchumi na kiteknolojia, Kiingereza kimekuwa leo lugha ya kwanza ya mawasiliano duniani hata kama si lugha yenye wasemaji wengi wa lugha ya kwanza.
Pia aina nyingi za Krioli na Pijini zimetokana na Kiingereza na kudumu hadi leo.
Kiingereza ni lugha rasmi pekee katika nchi za Uingereza, Marekani, Australia, Nyuzilandi, Jamaica, na nchi nyingine.
Kiingereza ni lugha rasmi pamoja na lugha nyingine katika nchi nyingi, kwa mfano Kanada (pamoja na Kifaransa), India (pamoja na Kihindi na lugha za majimbo), Ireland (pamoja na Kigaelik), Philippines (pamoja na Kitagalog).
Kwa jumla ni lugha rasmi katika nchi karibu 60, mbali ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya.
Kiingereza barani Afrika
haririNchi nyingi za Afrika zinatumia Kiingereza kama lugha rasmi, lakini ni Waafrika wachache (isipokuwa Waafrika Kusini) wanaoitaja kuwa lugha ya kwanza kwao. Nchi hizo ni Afrika Kusini, Eswatini, Ghana, Kamerun, Kenya, Lesotho, Liberia, Namibia, Nigeria, Sierra Leone, Zambia na Zimbabwe.
Kiingereza kinazumgumzwa pia katika nchi nyingine za Afrika ambapo si lugha rasmi. Lugha nyingi za Afrika zimekopa maneno ya Kiingereza. Maneno hayo yamerekebishwa kulingana na sauti ya lugha nyingine, kwa mfano: Kiingereza: train --> Kiswahili: treni.
Marejeo
hariri- ↑ Celtic and the History of the English Language, blogu ya Jonathan Owen kuhusu athira za Kikelti katika Kiingereza cha Kale
Viungo vya nje
hariri- makala za OLAC kuhusu Kiingereza Ilihifadhiwa 29 Juni 2015 kwenye Wayback Machine.
- lugha ya Kiingereza katika Glottolog
- (en) Muhtasari kuhusu Kiingereza kwenye Ethnologue
- Kamusi Hai Ilihifadhiwa 15 Novemba 2007 kwenye Wayback Machine. ya Kiingereza - Kiswahili - Kiingereza
- (en) More than 20000 English words recorded by a native speaker
- (en) Re-Romanization of EnglishIlihifadhiwa 11 Agosti 2011 kwenye Wayback Machine.