Obiti (kutoka neno la Kiingereza orbit lenye asili ya Kilatini orbita "njia, mzunguko"; pia: njia mzingo) ni njia inayotumiwa na gimba la angani linalozunguka gimba kubwa zaidi katika anga ya ulimwengu ilhali inashikwa na mvuto wa graviti. Mfano wake ni mwendo wa sayari inayozunguka jua, au mwezi unaozunguka sayari yake, au satelaiti inayozunguka dunia.

Obiti ya gimba dogo (kama satelaiti) linalozunguka gimba kubwa (kama Dunia);
kani ya velositi "v" inataka kulipeleka mbele mbali na mahali pake; kani ya graviti "a" inalivuta kuelekea gimba kubwa; tokeo lake ni obiti ya kuzunguka.
Mfano wa "Mzinga wa Newton"

Uwiano wa kani katika obiti

Fizikia ya obiti inatazama kani au nguvu mbili.

  • Ya kwanza ni velositi ya gimba dogo inayoelekea kwenda mbele mbali na mahali pake.
  • Ya pili ni graviti inayovuta gimba dogo kuelekea gimba kubwa. Obiti ipo pale ambako nguvu hizi mbili zinalingana. Kama kasi ya velositi ikiwa kubwa zaidi gimba dogo lisingezunguka bali ingetoka. Kama kani ya graviti inakuwa kubwa zaidi gimba dogo litaanguka kwenye gimba.

Mfano wa "Mzinga wa Newton"

Mwanafizikia Isaac Newton aliwaza mfano unaoeleza vizuri kani zinazoathiri obiti. Aliwaza mfano wa mzinga uliowekwa juu ya mlima mrefu. Mzinga huu unaweza kurusha risasi kwa mwelekeo wa ulalo kwa kasi mbalimbali. Athari ya msuguano wa hewa kupunguza kasi dhidi ya risasi aliacha kando au kuwaza mlima mrefu kiasi cha kupenya juu ya angahewa ya dunia.

  • Kama mzinga unarusha risasi yake kwa velositi ndogo itaenda mbele kiasi halafu kuanguka chini (A).
  • Kama kasi au velositi inaongezwa itaanguka mbali zaidi(B).
  • Kasi ya risasi ikiongezeka zaidi kuna hali ambapo risasi haianguki tena inazunguka dunia na kumailisha obiti ya duara (C).
  • Kama kasi inaongezeka tena obiti inachukua umbo la duaradufu. Mahali pa periheli ambapo obiti ipo jirani zaid na dunia ni mahali pa kufyatuliwa na 180° kinyume chake upande wa pili ni afeli ambapo obiti iko mbali na Dunia. (D)
  • Kasi ya risasi ikiongezwa zaidi inafikia velositi ya kuweza kutoka katika graviti ya Dunia. (E).

Kwa hali halisi makadirio ya makombora ya kurusha satelaiti na vyombo vya angani vinafuata maelezo hapo juu. Kama kombora linatakiwa kubeba satelaiti kama vile satelaiti ya televisheni au ya mawasiliano ni lazima kukadiria velositi ya kombora kulingana na uzito wake na mahali panapotakiwa kufikia angani ili kuweza kupeleka satelaiti katika obiti aina ya (C) au (D).

Chombo cha angani kinapotakiwa kupelekwa safari ya kwenda mwezi au sayari nyingine sharti kufikia "velositi ya kutoka" katika graviti ya Dunia.

Historia ya utafiti wa obiti

Zamani watu walifikiri ya kwamba jua lina obiti ya kuizunguka dunia kila siku jinsi inavyoonekana kwa macho: Jua linachomoza upande mmoja wa upeo wa anga wakati wa asubuhi na kuzama chini upande wa pili wakati wa jioni.

Kwa hiyo wataalamu Wagiriki wa Kale kama Klaudio Ptolemaio waliwaza obiti za jua na sayari za kuzunguka dunia na obiti hizi zilikuwa na umbo la duara kamili.

Kuanzia utafiti wa akina Koperniko na Galilei ilitambuliwa ya kwamba dunia ndiyo inayozunguka Jua pamoja na sayari nyingine, kila moja kwenye obiti yake. Ilionekana pia ya kwamba obiti hizo si duara kamili lakini zinalingana zaidi na duaradufu.

Kipindi cha obiti

Kipindi cha obiti ni muda unaotumiwa na gimba kama satelaiti, mwezi au sayari kuzunguka gimba mama.

Kwa mfano kipindi cha obiti ya obiti ya Dunia yetu kuzunguka Jua ni siku 365.25 na kipindi hiki tunaita "mwaka".

Kipindicha obiti ya mwezi wetu ni siku 1; wakati huohuo unazunguka mara moja kwenye mhimili wake na hii ndiyo sababu sisi tunaona upande uleule wa mwezi wetu muda wote.

  Makala hii kuhusu mambo ya fizikia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Obiti kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Mradi wa Astronomia Makala hii imewahi kukaguliwa na kuboreshwa kwenye warsha ya pamoja ya Jenga Wikipedia ya Kiswahili, Wikimedia Community User Group Tanzania na ASSAT. Imepewa hali ya ulinzi. Tunaomba mapendekezo yote ya usahihisho na nyongeza zipelekwe kwanza kwenye ukurasa wa majadiliano