Visiwa vya Kirimba (Kireno: Quirimbas, Ilhas de Querimba) ni funguvisiwa katika Bahari Hindi mbele ya mwambao wa Msumbiji wa kaskazini, kusini ya rasi ya Delgado. Inafuata mwendo wa pwani kwa umbali wa 180 km hadi mji wa Pemba. Umbali na pwani ni kati ya 12 na 20 km.

Visiwa vya Kirimba mbele ya mwambao wa Msumbiji ya Kaskazini

Idadi ya visiwa ni takriban 50. Vingi ni vidogo havikaliwi na watu. Kisiwa kikuu ni Ibo penye makao ya utawala wa Wilaya ya Ibo inayotawala funguvisiwa yote. Visiwa ni sehemu ya jimbo la Cabo Delgado. Wilaya ina wakazi 7.061 na eneo la nchi kavu visiwani la 48 km². Kati ya visiwa ni Ibo, Kirimba (Quirimba), Matemo, Quilaluia, Quisiva na Rolas.

Sehemu ya kusini ya funguvisiwa pamoja na nchi ya bara karibu nayo imekuwa hifadhi ya taifa ya Kirimba.

Visiwani kuna lahaja ya Kiswahili ya pekee kinaitwa Kimwani.

Historia

hariri

Kihistoria kisiwa cha Kerimba (Quirimba) kilikuwa muhimu zaidi na kulipa jina lake kwa funguvisiwa. Funguvisiwa ilikuwa chini ya athira ya kisiasa ya Kilwa ikiwa na sultani yake ya pekee. Uislamu ulifika zamani visiwani lakini tarehe haijulikani.

Wareno walivamia visiwa mnamo mwaka 1522 kwa sababu ya biashara ya meno ya ndovu. Padre João dos Santos alifika kuhubiri Ukristo mwaka 1593 alikuta tabaka ya juu walikuwa Waislamu na watu wa kawaida wakifuata dini za jadi. Kuna taarifa ya mwaka 1769 juu ya malamiko ya Wareno dhidi ya Waarabu na Waswahili wa visiwa kuwa walifanya biashara ya watumwa na meno ya ndovu na Waswahili waislamu wa kaskazini badala ya Wareno wenyewe wa Msumbiji.

Hadi karne ya 19 visiwa vya Kirimba vilikuwa kituo muhimu cha biashara ya watumwa. Kuna kubukumbu ya mwaka 1860 kuhusu mzigo wa watumwa 846 waliofika Mauritius kutoka visiwa vya Kirimba.

Jina la visiwa liliwahi kuandikwa na Wareno kama: Queriba, Quiriba, Querimba, Quirimba, Carimba, Cerimba, Corimba, Querimbas au Quirimbas

Viungo vya nje

hariri
  • (Kireno) C.L. Bento: Ilhas de Querimba, situaçaõ colonial, resitencias e mudanca ftn17