Leo duniani kuna watu wengi sana wanaojinasibisha na Waarabu wakiwa wanaishi Bara Arabu au Mashariki ya Kati au kwengineko ulimwenguni. Watu hawa ambao wanatafautiana baina yao kirangi na kimaumbile na kisura wote wanadai kuwa ni Waarabu au asli zao ni za Kiarabu. Walakini, ni nani hasa hawa Waarabu na nini asli yao?

Wanachama za Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
Kijani nyeusi: wakazi wengi hutumia Kiarabu
Kijani nyeupe: maeneo ya nchi wanachama ambako wenyeji hawatumii Kiarabu kama lugha ya kwanza
kijani milia:wasemaji wa Kiarabu ni wachache; katika Jibuti, Somalia na Komori si lugha rasmi ya serikali

Asli ya Waarabu:Edit

Waarabu wote ulimwenguni wanatokana na jadi moja ambaye ni mtoto wa Nabii Nuh aitwaye Sam, lakini baadaye waligawanyika katika makundi matatu:

1- Waarabu (Al-Baida):

Nao ni Waarabu ambao leo hawako tena ulimwenguni kwa sababu ni kaumu zilizoangamizwa na Mwenyezi Mungu baada ya kukataa kufuata maamrisho yake na kwenda kinyume na Mitume yao, nao ni: Kaumu ya Hud ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la A'ad, na kaumu ya Saleh ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Thamud. Kaumu mbili hizi ziliangamizwa na Mwenyezi Mungu kwa kumuasi na kutofuata amri na maelekezo ya Mitume yao, na waliobakia katika makundi haya mawili ndio waliokuja kufanya makundi ya Waarabu wanaojulikana kwa jina la Waarabu (Al-A'ariba).

2- Waarabu (Al-A'ariba):

Nao ni Waarabu waliotokana na mtoto wa Nabii Hud (AS) ajulikanaye kwa jina la Qahttaan na kutokana na kizazi chake ndio hawa Waarabu wanaoitwa Al-A'ariba wakaenea kila upande. Waarabu hawa ambao makabila yao makubwa wakati huo yalikuwa ni Himyar na Kahlaan walikuwa wakiishi Yemen na kuwa na ufalme na ustaarabu mkubwa mpaka yalipotokea mafuriko makubwa hapo Yemen yakawatawanya na kuwasukuma kwenda sehemu nyengine mbali mbali za Bara Arabu na Shamu na Iraqi na Misri na Afrika Mashariki.

3- Waarabu (Al-Mustaariba):

Nao ni Waarabu waliotokana na Nabii Ismail (AS) ambaye aliletwa na babake Nabii Ibrahim (AS) na kuwekwa katika bonde la Makka pamoja na mamake Hajar na kuachwa hapo kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Nabii Ismail hakuwa Mwarabu lakini baada ya kukaa hapo Makka na kutifuka chemchemu ya Zamzamu, walikuja Waarabu wa Kiyemeni wa kabila la Jurhum na walipoona maji hapo waliomba kubakia hapo na ndipo Nabii Ismail akakulia kwenye kabila hilo na kujifunza Kiarabu na kuoa katika kabila hilo. Kwa hivyo, kizazi chake kiliinukia kuwa Waarabu kwa kuchanganyika na kabila la Waarabu na wakawa wanajulikana kama Waarabu Al-Mustaariba.

Maskani ya Waarabu ya asliEdit

Waarabu, kama tulivyoeleza hapo nyuma, mwanzo walikuwa wakiishi Yemen lakini baadaye wakaanza kutawanyika kwenye sehemu nyenginezo za Bara Arabu, na kwa kuwa wengi wao walikuwa wakiishi maisha ya kibedui ya kusafiri kutoka mahali pamoja kwenda kwengine kutafuta chakula na maji kwa nafsi zao na wanyama wao, waliweza kuenea sehemu zote za Bara Arabu na kufika Shamu na Iraqi na Misri na Afrika ya Mashariki na Afrika ya Kaskazini.

Kutawanyika huku kulizidi kuwa na kasi baada ya kuvunjika bwawa lao kubwa lililokuwa Maarib huko Yemen lililokuwa likilimbika maji mengi kwa ajili ya ukulima na mabustani yao na malisho ya wanyama wao, na mtawanyo mkubwa wa pili ni baada ya kuja Uislamu na kuhitajia kupeleka watu sehemu mbali mbali ulimwenguni kueneza dini hii. Hapo ndipo Waarabu walipotawanyika kila mahali ulimwenguni kueneza neno la Mwenyezi Mungu na kufikisha ujumbe wake, na ndiyo maana leo tunaona Waarabu katika kila bara la mabara ya ulimwengu.

Ulimwengu wa Waarabu leoEdit

Waarabu, leo, wako kila mahali ulimwenguni, lakini kila ukikaribia kwenye kitovu cha dunia ambacho kiko Bara Arabu, Uarabu unazidi kudhihirika zaidi na lugha yao inazidi kuwa fasihi zaidi na hapa ndipo ada na mila zao zinazidi kuhifadhiwa na kutiliwa mkazo. Aidha, Waarabu wanaishi kwenye nchi zaidi ya ishirini za Mashariki ya Kati, ikiwemo Bara Arabu na Shamu na Iraqi na nchi za Ghuba ya Uajemi (Uarabu) na Afrika ya Kaskazini na Mashariki. Kuna ushirikiano katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Idadi ya Waarabu ulimwenguniEdit

Waarabu ulimwenguni wanahesabiwa kuwa idadi yao imefikia mia tatu milioni (180,000,000), ijapokuwa kuna idadi kubwa vile vile ya watu wa makabila mengine ambao wanaishi kwenye nchi za Kiarabu kama Mairani na Wahindi na Maarmani na Mayahudi na Mabarbari na Waafrika na Mabulushi na Makurdi na Waturuki na wengineo. Kwa upande mwengine, kuna Waarabu wengi sana ambao wametawanyika katika nchi mbali mbali za dunia kwenye mabara yote ya ulimwengu.

Wajiitao Waarabu leoEdit

Leo ulimwenguni kuna watu wanaojinasibisha na Waarabu kwa sababu hizi zifuatazo:

  1. Kila anayeishi katika nchi ya Kiarabu na kuwa na uraiya wa nchi ya Kiarabu
  2. Kila anayezungumza Kiarabu na kufuata mila na ada za Kiarabu
  3. Kila ambaye anajua kuwa asli yake na ya wazee wake ni Waarabu hata ikiwa hajui Kiarabu

Dini ya WaarabuEdit

Watu wengi sana ulimwenguni wanafikiria na kuchukulia kuwa dini ya Waarabu ni Uislamu, lakini ukweli ni kwamba kuna Waarabu wengi ambao ni Wakristo, na hii ni kwa sababu kabla ya kuja Uislamu.

Waarabu walikuwa wakifuata dini mbali mbali za Kiyahudi na Kikristo na Kimajusi na wengineo walikuwa hawana dini kabisa au dini za kienyeji, na juu ya kuwa wengi waliingia kwenye dini ya Uislamu baada ya kuja Mtume Muhammad (SAW), lakini wale walioamua kubakia kwenye dini zao hawakulazimishwa kuingia kwenye Uislamu na ndio maana leo tunaona kuna Waarabu Wakristo sehemu za Syria na Lubnani na Iraqi na Misri na kwengineko.

Lugha ya KiarabuEdit

Lugha ya Kiarabu ilienea baada ya kuja Uislamu na kufika sehemu nyingi duniani kwa sababu ya watu kutaka kujua dini yao na kuweza kusoma Qurani Tukufu na kujua maneno ya Mtume wao Muhammad (SAW), na kwa kuwa imetawanyika sehemu nyingi za Mashariki ya Kati kumezuka lahaja mbali mbali ambazo mara nyengine ni taabu kufahamika baina ya watu wa sehemu fulani na wengineo wa nchi nyenginezo. Juu ya hivyo, kuna lahaja zilizo karibu kama lahaja za Shamu na lahaja za Ghuba na za Bara Arabu na lahaja za Afrika ya Kaskazini na lahaja ya Misri na Sudani.