Mafumu Bilal Bombenga (1958[1] - 11 Mei, 2020[2][3]) maarufu kama Super Sax, alikuwa mwanamuziki wa muziki wa dansi kutoka jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Mafumu Bilali
Taarifa za awali
Jina la kuzaliwaMafumu Bilali Bombenga
Pia anajulikana kamaVumbi
AmezaliwaKigoma, Tanzania
Kazi yakeMpiga sax
Ameshirikiana naMorogoro Jazz Band, Western Jazz Band, Twanga Pepeta, Kiliamanjaro Connection

Historia hariri

Maisha na muziki hariri

African Beat ilianzishwa mwaka 1998, baada ya Mafumu Bilali Bombenga kujiengua kutoka katika bendi ya African Stars ambayo nayo ilianzishwa mnamo mwaka 1994 kwenye Hoteli ya Bahari Beach, jijini Dar es Salaam, huku yeye akiwa ndiye muanzilishi.

Bombenga anakumbuka kuwa, wakati akiwa na African Stars ambayo hata jina lake alilibuni yeye, walitamba na vibao kama ‘Sakatu Sakatu’, ‘Mayanga’, ‘Maya’, ‘Afrika’ na ‘Dance Dance’. Baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakiunda kundi hilo la African Stars linalojulikana zaidi hivi sasa kama ‘Twanga Pepeta’, ni Bob Gady, Andy Swebe, Alfa Nyuki, Palmena Mahalu, Pamela pamoja na Kayumbu ‘Amigolas’.

Safari ya kwenda mabendi mbalimbali hariri

Historia kamili ya kimuziki ya Mafumu, inaanzia mwaka 1972 nilipojiunga na bendi ya Morogoro Jazz Band, wakati huo akitokea jeshini Makutupola. Mwaka 1973 alijiunga na Western Jazz Band alioshiriki nao kupiga Saxophone, kwenye vibao kadhaa vya bendi hiyo, vikiwamo ‘Hakika’, ‘Kazi ni Kazi’ na ‘Sadaka’, kabla ya mwaka 1978 kutimkia Dar International.

Pamoja na kupuliza kiustadi Saxophone pamoja na kuimba kwenye nyimbo kemkemu, zikiwamo ‘Mayasa’ na ‘Zuena’, lakini pia Bombenga alishiriki kucharaza gitaa la Solo katika kibao Vicky.

Mwaka 1979 alibeba mabegi na kutua Vijana Jazz Band alikotunga kibao "Taabu" na pia kushiriki kukiimba, huku kadhalika akipuliza Saxophone kwenye vibao kama Chiku na Matata Ndani ya Nyumba.

Mwaka 1980 alihamia Maquis ambapo alitesa kwa kupuliza Saxophone kwenye vibao viiingi, baadhi yake ni Zoa, Sina Ndugu, Noel pamoja na Maige.

Alikaa Maquis hadi mwaka 1984 alipochomoka tena na kuhamia Bima Lee alikokutana na wakali kama Jerry Nashon Dudumizi, Shaaban Dede Super Motisha, Joseph Mulenga Spoiller.

Mwaka 1985 Bombenga alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa bendi ya MK Group Ngoma za Maghorofani, kabla ya mwaka 1986 kuwa tena mmoja wa waanzilishi wa Tancut Almas ya Iringa.

Mwaka 1987 alirejea tena MK Group ambapo nyimbo yake ya kwanza kupuliza Saxophone awamu hii ya pili ilikuwa ni ‘Utakuja Kuanguka Kwenye Matope’.

Mwaka 1989, kaka yake Adam Kinguti alirudi nchini akitokea Sudan alipokuwa akifanyakazi kwenye ofisi za ubalozi, wakaanzisha Bicco Stars na yeye kushiriki kupuliza Saxophone kwenye vibao kadhaa kama vile; Magret Mage, Wapangaji na Kisamvu.

Mwaka 1991 alitoka Bicco akiwa na mpapasaji kinanda mahiri wa kike ambaye kwa sasa ni marehemu, Asia Daruweshi, baada ya kutokea hali ya kutoelewana kati yake na Kinguti, wakaanzisha Zanzibar Sound.

Akiwa na Zanzibar Sound, walipata mkataba katika Hoteli ya Mount Meru, Arusha na mwaka mmoja baadaye mwanamuziki mwenzao kwenye bendi hiyo, Kanku Kerry alipata mkataba Japan wakaondoka naye kwa sharti la sasa kujiita Kilimanjaro Connection.

Walizunguka nchi nyingi za bara la Asia wakiwa na Kilimanjaro Connection, waliporudi mwaka 1994 alijitoa na baadaye kidogo Asia naye alijitoa na kurudisha upya bendi yake ya Zanzibar Sound na kurejea mkataba wake Bahari Beach Hotel.

Bombenga wakati huu akabaki bila bendi, ambapo muda si muda Asia alipata kazi nchini Bahrain na kumuachia Bombenga mkataba wa Bahari Beach.

Baada ya kuona ameachiwa mkataba wakati hana bendi, Bombenga ndipo alipomfuata Baraka Msirwa na kumuomba vyombo vya muziki ambapo alimpa kwavile havikuwa na kazi kutokana na kufa kwa bendi za MK Group, MK Beat na MK Sound zilizokuwa zikivitumia.

Hicho ndio kilikuwa chanzo cha bendi ya African Stars aliyoibuni mwenyewe hadi jina, iliyomletea uhasama mkubwa na dada yangu Asha Baraka baada ya kujitoa Bombenga.

Maisha binafsi, harakati za kuachana na muziki, urithi wake hariri

Mafumu ni mtoto wa tano katika familia ya mzee Bilali Mafumu, aliyepata elimu yake ya msingi katika shule ya H.H Agakhan, Kigoma ambako alifaulu na kujiunga na shule ya sekondari Kazima, Tabora alisoma hadi kidato cha nne.

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, Bombenga aliyesoma shule moja ya sekondari na mbunge wa Tabora, Ismail Aden Rage, anasema kuwa 1972 alijiunga na JKT kwa mujibu wa sheria ya enzi hizo, alikojifunza kuimba na kupuliza Saxophone.

Anaishi Vingunguti, jijini Dar es Salaam na familia yake ambayo ni mkewe na watoto saba.

Kwa upande wa warithi, Bombenga ana wanawe wawili wanaoonekana kufuata vema nyayo zake, ambao ni Feruzi (22) anayepapasa kinanda na Aziza (19) ambaye ni mwimbaji.

Bombenga mwenye miaka 40 katika muziki na aliyejifunza mengi kupitia sanaa hiyo, anavutiwa na waimbaji; [[Isha Mashauzi, Nasseeb Abdul Diamond, Flora Mbasha na Hassan Bitchuka.

Tazama pia hariri

Marejeo hariri

  1. "Mafumu nguli wa ‘midomo ya bata’". Mwananchi (kwa Kiingereza). 2021-03-13. Iliwekwa mnamo 2022-02-13. 
  2. Tanzania Standard Newspapers Ltd. "Bombenga afariki, azikwa Vingunguti". www.habarileo.co.tz (kwa Kiingereza). Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2022-02-13. Iliwekwa mnamo 2022-02-13. 
  3. "Tanzia: Mwamuziki Mafumu Bilal Afariki Dunia". Global Publishers. 2020-05-12. Iliwekwa mnamo 2022-02-13. 

Viungo vya Nje hariri

  Makala hii kuhusu mwanamuziki/wanamuziki fulani wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mafumu Bilali kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.