Mfupa
Mfupa ni tishu ngumu katika mwili mwa binadamu na wanyama wenye uti wa mgongo. Mifupa inahimili ogani nyingine mwilini na kuuwezesha kusimama. Mifupa ni pia kinga kwa sehemu muhimu sana kama vile mifupa ya fuvu inakinga ubongo na ubavu wa kifua unaokinga moyo na mapafu.
Kiunzi cha mifupa
Mifupa inaunganishwa katika kiunzi cha mifupa. Mwili wa binadamu huwa na mifupa zaidi ya 200, idadi inayojulikana kwa wataalamu ni 270, lakini wakati wa maisha mifupa mingi inaungana kuwa mmoja, hivyo kwa kawaida mtu mzima huwa na mifupa 206.
Muundo wa mfupa
Mwili unajenga mifupa hasa kwa minerali ya fosfati ya kalisi. Minerali hii inafanya ile ganda gumu la nje la mfupa. Ndani yake mfupa huwa na muundo unaofanana na matriki au nyavu ya ufumwele na muundo huu unapunguza uzito wa mfupa pamoja na kuufanya imara.
Kwa nje mfupa hufunikwa na ngozi ya pekee (periosteum). Ndani ya mfupa kuna neva, mishipa ya damu na uboho. Uboho ni mahali pa kuzalisha seli za damu. Katika umri wa mtoto karibu kila mfupa huwa na uboho ndani yake, kwa mtu mzima ni mifupa mikubwa na minene zaidi tu.
Magonjwa ya mifupa
Kuna magonjwa mbalimbali yanayoweza kuathiri mifupa.
Kuvunjwa kwa mfupa ni tatizo linalotokea mara nyingi baada ya kuanguka vibaya au kupigwa kwa nguvu. Hapo ni lazima vipande vilivyovunjika vishikwe pamoja bila kuchezacheza hadi tishu mpya ya kimfupa iunganishe pande zote mbili.
Ugonjwa unaotokea kwa wazee na pia kwa watu wenye utapiamlo, hasa wakikosa kalisi katika chakula, ni kudhoofika kwa mifupa, yaani osteoporosi. Maziwa au jibini huingiza kalisi mwilini. Osteoporosi husababisha kuvunjika kwa mifupa kirahisi.
Viungo vya mifupa kama vile kiwiko au goti vinafunikwa na gegedu kwa kuzuia msuguano kati ya mifupa miwili. Gegedu hii inaathiriwa na ugonjwa wa baridi yabisi au arthritis.
Kansa ndani ya mifupa inaweza kusababisha maumivu makali.
Ngozi inayofunika mfupa inaweza kuambukizwa na hali hii huitwa periostitisi, hutibiwa kwa madawa kiua vijasumu (antibiotics).
Makala hii kuhusu mambo ya anatomia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mfupa kama matumizi yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |