Kwa habari za sayari (wakati mwingine kwa kosa huitwa pia "Kausi") angalia hapa Neptuni; kwa matumizi mengine ya jina "Sagittarius" angalia hapa Sagittarius

Nyota za Mahale au Kausi angani (mistari imeongezwa kwenye picha tu)
Mshale jinsi inavyochorwa na msanii

Mshale (pia Kausi, kwa Kilatini/Kiingereza: Sagittarius[1]) ni jina la kundinyota kwenye zodiaki.

Nyota za Mshale huwa haziko pamoja kihalisi lakini zinaonekana tu vile kutoka duniani. Kwa uhalisi kuna umbali mkubwa kati yao, kama ziko mbali au jirani nasi. Kwa hiyo kundinyota "Mshale" linaonyesha eneo la angani jinsi tunavyoiona kutoka Duniani.

Jina

Mabaharia Waswahili wamejua nyota hizi kwa muda mrefu kwa jina la "Kausi" linalotokana na neno la Kiarabu Qaws قوس linalomaanisha "upinde". Maana hii ni karibu sawa na jina la Kilatini "Sagittarius" (mpiga upinde). Wataalamu wa kale waliona katika nyota zake picha ya mtu anayekalia juu ya farasi akishika pinde na kulenga mshale.

Jina la "Kaus" limetumiwa pia katika elimuanga ya kimagharibi kutaja nyota kadhaa zilizomo hapa kama vile Kaus Australis, Kaus Medius na Kaus Borealis.

Katika vitabu kadhaa vya shule za msingi nchini Tanzania "Kausi" imetumiwa kwa kosa kutaja sayari ya nane katika Mfumo wa Jua letu yaani Neptuni.

Katika unajimu wa kisasa jina la Kausi limeshasahauliwa na nyota hizi zinajulikana zaidi kwa “Mshale” ambayo inarejelea picha inayotumiwa kama ishara yake.

Kuonekana

Mshale inaonekana pale angani ambako Njia Nyeupe inang'aa zaidi yaani kuelekea kitovu cha majarra yetu.

Mshale ni kati ya makundinyota yaliyojulikana tangu karne nyingi zikitumiwa hasa na mabaharia kutafuta njia baharini wakati wa usiku.

Nyota na magimba ya anga

Katika eneo la Mshale wataalamu wa anga walitambua magimba ya angani kadhaa ya maana. Hizi ni pamoja na

Jina
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(UKIA)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miaka nuru)
Aina ya spektra
ε 20 Kaus Australis 1,9m 143 B9.5 III
σ Nunki 2,05m 224 B2.5 V
ζ 38 Ascella 2,60m 89 A3 IV
δ 19 Kaus Media 2,72m ca. 350 K3 III
λ 22 Kaus Borealis 2,82m 78 K0 IV
π 41 Albaldah 2,88m 440 F2 II/III
γ 10 Alnasl 2,98m 96 K0 III
η 3,10m 149 M2 III
φ 27 3,17m 231 B8.5 III
τ 40 3,31m 120 K1 / K2III
ξ2 37 3,52m 372 G8 / K0II/III
ο 39 3,76m 139 K0 III
μ 13 Polis 3,84m 3912 B2 III
ρ1 44 3,92m 122 F0 III/IV
β1 Arkab Prior 3,96m 378 B9 V
α Rukuba ya Rami (α Sgr) 3,97m 170 B8 V
ι 4,12m 189 K0 III
β2 Arkab Posterior 4,27m 139 F2 III

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Sagittarius" katika lugha ya Kilatini ni "Sagittarii" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Sagittarii, nk.

Marejeo

  • kuhusu jina: Jan Knappert, The Swahili names of stars, planets and constellations; makala katika jarida la The Indian Ocean Review, Perth, Australia September 1993, uk. 7
  Makundinyota ya Zodiaki
Majina ya kisasa yanafuatwa kwa mabano na jina la mabaharia na jina la Kilatini (la kimataifa)
 

Kaa (Saratani – Cancer  )Kondoo (Hamali – Aries  )Mapacha (Jauza – Gemini  )Mashuke (Nadhifa – Virgo  )Mbuzi (Jadi – Capricornus  )MizaniLibra  )Mshale (Kausi – Sagittarius  )Ndoo (Dalu – Aquarius  )Nge (Akarabu – Scorpius  )Ng'ombe (Tauri – Taurus  )Samaki (Hutu – Pisces  )Simba (Asadi – Leo  )