Muungano wa Afrika Kusini
Muungano wa Afrika Kusini lilikuwa jina la Afrika Kusini kuanzia 1910 hadi 1961. Kwa lugha rasmi za nchi jina lilikuwa "Union of South Africa" (Ing.) na "Unie van Zuid-Afrika" (Afr.).
Ilianzishwa kama muungano wa koloni 4 za Kiingereza zilizokuwa Koloni ya Rasi, Natal, Transvaal na Dola Huru la Oranje. Nchi mpya iliundwa kama dominion ya milki ya Uingereza na kupewa serikali yake pamoja na mamlaka ya kujiamulia katika siasa ya ndani na kuwa na jeshi la kitaifa.
Waafrika, chotara na wenye asili ya Asia hawakuwa na haki za kiraia kwenye ngazi ya muungano; jimbo la Rasi pekee ilikubali haki za kupiga kura kwa wakazi wote waliokuwa na kiwango fulani cha Mali wakilipa kodi za kutosha; hapa idadi ndogo ya Waafrika ilikuwa na haki za kiraia kamili kabla ya siasa ya apartheid iliyofuta haki hizi.
Ofisi kuu za dola zilizambazwa katika majimbo mbalimbali kwa sababu viongozi walishindwa kuelewana juu ya mji mkuu mmoja. Makao ya serikali ilikuwa mjini Pretoria (Transvaal), makao ya bunge mjini Cape Town (Jimbo la Rasi) na mahakama kuu katika Bloemfontein (Dola Huru la Orange). Muundo huu unaendelea hadi leo.
Siasa ya apartheid tangu 1948 ilisababisha hali gumu kati ya Uingereza, nchi mpya za Afrika na Maungano ya Afrika Kusini. Hapo bunge liliamua kujitenga kabisa na Uingereza na kutangaza jamhuri nje ya Jumuiya ya Madola.
Tarehe 31 Mei 1961 nchi ilitangaza uhuru wake kama Jamhuri ya Afrika Kusini.