Dola Huru la Oranje

Dola Huru la Oranje (Ing.: Orange Free State; Afr.: Oranje-Vrystaat) lilikuwa jamhuri ya makaburu katika Afrika Kusini wakati wa nusu ya pili ya karne ya 19 iliyoundwa na mavoortrekker. Baadaye ilikuwa koloni ya Uingereza na jimbo la Afrika Kusini, tangu 1995 kwa jina "Free State Province" (jimbo la Dola Huru).

Dola Huru la Oranje mnamo 1885 kati ya Koloni ya Rasi (kusini) na Transvaal (South African Republic - kaskazini)
Bendera ya Dola Huru la Oranje
stempu ya posta ya Dola Huru la Oranje

Jina la jamhuri lilichaguliwa kutokana na Mto Oranje uliokuwa mpaka wake.

Historia

hariri

Baada ya kutwaliwa kwa Koloni ya Rasi na Uingereza kutoka Uholanzi wakazi makaburu wengi walisikitika mabwana wapya hasa matumizi ya Kiingereza katika utawala, mahakamani na shuleni, pia sheria za Uingereza. Walowezi wakulima waliokaa karibu na mpaka wa koloni walijisikia hawalindwi na serikali ya Waingereza dhidi ya mashambulio ya Waxhosa waliokuja mara kwa mara kuchukua mifugo yao. 1834 utumwa ulipigwa marufuku katika Milki ya Uingereza na wenye watumwa walitakiwa kuwachisha watumwa wao. Makaburu wengi hawakuridhika malipo ya fidia yaliyopatikana.

Hivyo makundi ya voortrekker walianza kuondoka katika koloni na kuingia katika maeneo ya kaskazini walipotafuta ardhi ya kulimia. Walikuta maeneo mengi penye watu wachache kwa sababu vita za mfecane zilizotangulia ziliua watu wengi na kusababisha uhamisho wa makabila mengi. Makundi ya Wazulu waliwahi kufyeka nchi kwa kushambulia vijiji, kuchoma mashamba na nyumba, kuchukua mifugo na kuua watu wote iipokuwa watoto na vijana waliochukuliwa kama wake au askari wapya katika impi (vikosi vya kijeshi vya Kizulu) zao.

Baada ya mapigano na Wazulu kundi la kwanza la mavoortrekker chini ya uongozi wa Andries Hendrik Potgieter walipatana na Watswana chini ya chifu Moroka wa Wabarolong ya kwamba watawalinda Wabarolong dhidi ya Wazulu wa Matebele na kwa kazi hii walipewa maeneo makubwa ya mashamba. Walikaa katika eneo kati ya Wasotho na Watswana.

Baada ya jamhuri ndogondogo zilizotangulia Dola Huru la Oranje liliundwa mwaka 1842 katika eneo kati ya mito Oranje na Vaal. Lakini Waingereza kutoka Koloni ya Rasi walingia kati na kutangaza eneo la Oranje kuwa chini ya mamlaka yao. Katika miaka 10 iliyofuata sehemu za walowezi walisimama upande wa Uingereza lakini wengine waliendesha mapigano na Waingereza na makabila ya Waafrika walishikamana nao hasa Wasotho. Baada ya mwaka 1850 serikali ya Uingereza hakutaka tena kugharamia utawala katika eneo la Oranje na gavana mpya wa Rasi alipatana na viongozi wa mweleko wa jamhuri na kuitambua kama nchi huru katika mkataba wa 17 Februari 1854. Lugha rasmi katika jamhuri ilikuwa Kiholanzi.

Tangu mwaka 1870 almasi zilipatikana kwa wingi katika eneo la kukutana kwam mito ya Vaal na Oranje (mji wa Kimberley ya leo) na wachimbaji almasi wengi walifika hapa kutoka Koloni ya Rasi waliokuwa zaidi Waingereza si Makaburu. Hii ilileta matatizo lakini serikali za Dola Huru na Koloni ya Rasi ziliweza kupatana. Uhusiano mzuri ulidumu ingawa makaburu kadhaa wa Dola Huru walishiriki katika mapigano kati ya Uingereza na jamhuri ya Transvaal iliyokuwa jamhuri jirani ya Makaburu.

Lakini wakati vita ya pili ya Makaburu dhidi ya Uingereza ilipokaribia Dola Huru lilijiunga karibu zaidi na Transvaal na kuingia katika vita hii. Mwaka 1900 jeshi la Uingereza likuwa limeshatwaa Dola Huru yote; uhuru ukafutwa na eneo kuigizwa katika Milki ya Uingereza kama "Koloni ya Mto Oranje".

Baada ya ushindi wa Waingereza koloni hii ilipewa tena madaraka ya kujitawala na katika mapatano kati ya Wazungu wa Afrika Kusini imepandishwa ngazi kuwa moja ya majimbo nne katika Muungano wa Afrika Kusini tangu mwaka 1910.


Marejeo

hariri

Viungo vya Nje

hariri


29°00′S 26°00′E / 29.000°S 26.000°E / -29.000; 26.000