Muungano wa kifalme
Muungano wa kifalme ni hali ya kisiasa na ya kisheria ambako nchi mbili au zaidi zinachanga mtu yuleyule kama mfalme wao au mkuu wa dola.
Nchi zote hizo zinaendelea kuwa madola ya pekee lakini mfalme ni yeye yule.
Muungano wa aina hiyo hupatikana katika utaratibu wa utawala wa kifalme lakini haipatikani katika utaratibu wa kijamhuri.
Wakati wa sasa
haririMifano ya siku hizi ni hasa Jumuiya ya Madola. Nchi nyingi za jumuiya hiyo zinamtambua mfalme Charles III wa Uingereza kama mkuu wa dola kufuatana na katiba ya nchi. Mfalme anamteua gavana mkuu kama mwakilishi wake nchini. Katika utaratibu huo nchi hizo zitamtambua pia mfalme au malkia atakayemfuata Charles III kufuatana na sheria za Uingereza kuwa mkuu mpya wa nchi yao.
Nchi ndogo ya Andorra kati ya Ufaransa na Hispania ni mfano wa pekee ambako rais wa jamhuri anakuwa mkuu wa dola wa nchi nyingine. Tangu mwaka 1607 nafasi ya mkuu wa dola wa Andorra hushirikishwa kati ya askofu wa Urgel (Hispania) na mfalme wa Ufaransa. Baada ya mapinduzi ya Ufaransa mwaka 1789 rais wa jamhuri alichukua nafasi ya mfalme wa awali.
Mifano ya kihistoria
haririHistoria ina mifano mingi ya muungano wa kifalme kati ya nchi mbili zilizoendelea na taratibu zao za pekee lakini kumchanga mfalme yeye yule.
- Israel na Yuda zilichanga wafalme Sauli, Daudi na Suleimani kati ya miaka 1025 KK na 926 KK hivi
- Austria na Hungaria zilikuwa na ushirikiano wa kifalme kati ya 1867 na 1918; Kaisari wa Austria alikuwa pia mfalme wa Hungaria.
- Uingereza na Uskoti zilikuwa na muungano wa kifalme kati ya miaka 1603 na 1707. Tangu 1707 falme zote mbili ziliunganishwa kuwa "Ufalme wa Britania Kuu" yaani nchi moja.
- Vilevile muungano wa kifalme wa Uingereza (tangu 1707 Britania Kuu) na Ueire kati ya miaka 1541 na 1801; tangu 1801 pande zote ziliunganishwa katika "Ufalme wa Muungano wa Britania Kuu na Ueire" hadi 1922.
- Britania Kuu na Ufalme wa Hannover zilikuwa na muungano wa kifalme kati ya miaka 1714 na 1837 ilhali watemi wa Hannover walipokea taji la Uingereza.
- Hispania na Ureno zilikuawa na maungano ya kifalme kati ya 1580–1640
- nchi tatu za Skandinavia yaani Denmark, Uswidi na Norway zilikuwa na muungano wa kifalme chini ya mfalme wa Denmark kati ya miaka 1389 na 1521; unaitwa pia "Umoja wa Kalmar"
Makala hii kuhusu mambo ya siasa bado ni mbegu. Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari. |