Nunc dimittis
Nunc dimittis (kwa Kilatini "Sasa ruhusu") ni maneno ya kwanza ya wimbo wa mzee Simeoni (Lk 2:29-32) katika tafsiri ya Kilatini. Ndiyo sababu yanatumika kama jina la wimbo huo, mmojawapo kati ya zile nne zinazopatikana mwanzoni mwa Injili ya Luka.
Nafasi asili ya wimbo huo ni kwamba Yosefu na Bikira Maria walikwenda hekaluni Yerusalemu kwa ajili ya utakaso uliotakiwa na sheria ya Musa kwa kila mwanamke aliyejifungua.
Ilikuwa siku 40 baada ya Maria kumzaa Yesu na kwa kuwa mtoto huyo alikuwa wa kiume na wa kwanza kwa mama yake ilibidi atolewe kwa Mungu halafu kukombolewa kwa sadaka ya kondoo au, kwa mafukara, njiwa wawili (Kut 13:12-15; Law 12:1-8).
Kumbe, walipoingia hekaluni, mzee Simeoni, akiongozwa na Roho Mtakatifu, aliwalaki, akamtambua mtoto kuwa ndiye Masiya aliyetarajiwa, akampakata ili kumbariki, akamuomba kwa furaha Mungu amruhusu afe, mradi amemuona aliye wokovu wa mataifa yote.
Maneno yake yalivyoripotiwa na Luka mwinjili ndiyo yanayotumika katika liturujia ya madhehebu mbalimbali ya Ukristo, hasa katika Sala ya mwisho kabla ya kwenda kulala.
Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Nunc dimittis kama historia yake au athari wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |