Nyuki-bungu mkubwa
Nyuki-bungu mkubwa | ||||||||||||||||||||||||||
---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|
Bungu njano (Xylocopa caffra)
| ||||||||||||||||||||||||||
Uainishaji wa kisayansi | ||||||||||||||||||||||||||
| ||||||||||||||||||||||||||
Ngazi za chini | ||||||||||||||||||||||||||
Spishi ±500, 52 katika Afrika ya Mashariki |
Nyuki-bungu wakubwa, bungu wakubwa au nyuki-mbao (kutoka kwa Kijerumani holzbienen) ni nyuki wakubwa wa jenasi Xylocopa ya nusufamilia Xylocopinae katika family Apidae wanaojenga viota vyao ndani ya ubao. Spishi kadhaa huonyesha viwango mbalimbali vya kuwa na viota katika jamii, lakini hakuna hata mmoja wao ambaye ni ya kijamii kama nyuki-asali. Wanatokea katika mabara yote isipokuwa Antakitiki.
Spishi za makabila mengine ya Xylocopinae huitwa nyuki-bungu wadogo.
Maelezo
haririUrefu wa nyuki hawa ni mm 19-25 na mwili ni imara. Wana nywele nyingi ambazo ni nyeusi mara nyingi pamoja na nyeupe, maziwa, njano, machungwa au nyekundu kwenye mgongo wa thoraksi na/au fumbatio, ingawa nywele za madume mara nyingi ni aina ya njano (njanokijani hadi dhahabu). Nywele za miguu ya nyuma ni ndefu na zimegawanyika katika vijitawi ili kukusanya na kushikilia chavua (skopa). Pingili ya kwanza ya fumbatio ina shimo ya kina kidogo au kirefu ambamo matitiri wa kiufaano (symbiotic) wanaishi (acarinarium) ambao hula kuvu na vidusia kwenye kiota cha nyuki.
Majike wana kichomaji lakini hawashambuli watu na kuchoma tu wakati wa kushikwa au kunaswa chini ya nguo.
Biolojia
haririNyuki-bungu huchimba katika mbao ambazo si ngumu sana ili kutengeneza kiota chao, isipokuwa spishi za nusujenasi Proxylocopa, ambazo hutengeneza viota vyao katika udongo mwenye kinamu. Ingawa nyuki hufanya mwingilio mmoja tu, kunaweza kuwa na zaidi ya handaki moja ambazo ni sambamba kwa kadiri fulani. Ndani ya handaki, kuanzia mwishoni, vijumba vya kizazi hugawanywa kwa kuta zilizotengenezwa kwa chembe za ubao na mate. Donge la mchanganyiko wa chavua na mbochi huwekwa katika kila seli na yai kutagwa juu yake. Mayai ni makubwa kuliko yale ya nyuki wengine na ni baina ya mayai makubwa kabisa miongoni mwa wadudu. Handaki za viota pia hutumika kustahimili msimu usiofaa, kama majira ya baridi au kiangazi. Maandalizi ya chavua na mbochi huhifadhiwa kwa wakati kwa sababu hiyo.
Kiasilia nyuki-bungu huchimba katika miti hai au iliyokufa. Walakini, mara nyingi huchimba kwenye miundo ya mbao. Uharibifu kwa kawaida ni mdogo kwa sababu handaki ziko karibu na uso, lakini unaweza kuwa mkubwa ikiwa nyuki hazizuiliwi. Uharibifu zaidi unaweza kusababishwa na vigong'ota wanaochimba kwenye handaki ili kupata majana na mabundo ndani.
Ingawa nyuki-bungu wengi wako wapweke, spishi kadhaa ni za kijamii na pia zinaweza kuwa mpweke au za kijamii. Majike wanaohusiana wanaweza kushiriki kiota na kila mmoja kutunza majana yake. Vinginevyo, jike mmoja huenda kutafuta chakula huku wengine wakiendelea na kazi ya kulinda. Kutengeneza kiota ni shughuli ya pamoja. Hii inatofautiana na nyuki wa hali ya juu ya kijamii ambao wana malkia mmoja au kadhaa na nyuki wengi wafanyikazi katika kila kiota. Mfano wa nyuki-bungu wa kijamii kwa chaguo katika Afrika ya Mashariki ni Xylocopa pubescens.
Nyuki-bungu ni wachavushaji muhimu na maua fulani kutegemea kabisa nyuki hawa. Kwa kuwa wana ndimi fupi, hutembelea maua ya kina kifupi. Walakini, wanaweza kuiba mbochi kutoka kwa maua ya neli kwa kung'ata tundu katika chini ya neli ili kufikia mbochi. Mfano wa ua ambalo linategemea nyuki-bungu kwa uchavushaji, ni Orphium frutescens ya Afrika Kusini.
Spishi za Afrika ya Mashariki
hariri
|
|
Picha
hariri-
Xylocopa erythrina
-
Xylocopa flavorufa
-
Xylocopa inconstans
-
Xylocopa lugubris
-
Xylocopa olivacea
-
Xylocopa pubescens