Nywele za Berenike (kwa Kilatini na Kiingereza Coma Berenices) [1] ni jina la kundinyota dogo lililopo kwenye nusutufe ya kaskazini ya Dunia.

Nyota za kundinyota Nywele za Berenike (Coma Berenices) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Nywele za Berenike - Coma Berenices jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini

Mahali pake hariri

Nywele za Berenike (Coma Berenices) inapatikana angani karibu na nyota angavu za Simaki (Arcturus) na Sumbula (Spica). Inapakana na kundinyota jirani za Nadhifa (Mashuke) (Virgo), Bakari (Bootes), Mbwa wawindaji (Canes Venatici), Dubu Mkubwa (Ursus Major) na Asadi (Simba) (Leo).

Jina hariri

Nywele za Berenike (Coma Berenices) haikujulikana kama kundinyota ya pekee kwa mabaharia Waswahili. Ni dhaifu na ndogo sana hivyo haikuwa sehemu ya kundinyota zilizoorodheshwa na Ptolemaio katika Almagesti . Wagiriki wa Kale waliona nyota zake kuwa sehemu ya Asadi (Leo).

Hata hivyo kundinyota hili lilianzishwa nyakati za kale huko Misri. Mnamo mwaka 246 KK mfalme Ptolemaio II aliondoka Misri akavamia Syria. Mke wake malkia Berenike alikata nywele zake kama sadaka kwa miungu ili aweze kurudi salama akaacha nywele katika hekalu. Baadaye ilionekana ya kwamba nywele hazikupatikana tena hekaluni. Hapo Konon mwanaastronomia wa mfalme alitoa maelezo kuwa miungu walihamisha nywele za malkia angani kama kundinyota akabuni kundinyota “Nywele za Berenike”. Kwa hiyo Nywele za Berenike ilijulikana ingawa haikuwa kawaida. Wakati wa kutambuliwa upya kwa elimu ya kale katika Ulaya ya karne ya 16 Tycho Brahe aliingiza “Nywele za Berenike” katika ramani yake ya nyota.

Iko pia katika orodha ya kundinyota 88 zinazoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [2] kwa jina la Coma Berenices. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Com'.[3]

Nyota hariri

Nyota angavu zaidi ni Beta Comae Berenices au Diadem[4]. Ina mwangaza unaoonekana wa mag 4.25 ikiwa na umbali wake unakadiriwa 29.8 kutoka Duniani[5][6].

Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miaka nuru)
Aina ya spektra
β 43 4,25m 29,78 F9.5 V
α 42 4,3m 60 F5 V
γ 15 4,36m 250 K1 III
Habari za mwangaza na umbali vinaweza kubadilika kutokana na vipimo vipya

Tanbihi hariri

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya "Coma Berenices" katika lugha ya Kilatini ni "Comae Berenices" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Comae Berenices, nk.
  2. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  3. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R. 
  4. Diadem - Naming Stars , tovuti ya Ukia, iliangaliwa Novemba 2017
  5. Berenices-constellation/ Coma Berenices, tovuti ya Constellation Guide, iliangaliwa Oktoba 2017
  6. BETACOM (Beta Comae Berenices), tovuti ya Prof. Jim Kaler

Viungo vya Nje hariri

Marejeo hariri

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, “Argo Navis” ukurasa 168 ff (online hapa kwenye archive.org)